Tanzania ijifunze haya, mdororo wa uchumi Botswana

Kupungua kwa mauzo ya almasi kumetajwa kama moja ya sababu iliyofanya nchi ya Botswana kutangaza hali ya dharura kutokana na kushindwa kumudu baadhi ya mahitaji ikiwamo katika sekta ya afya.

Agosti 26, 2025 Botswana ilitangaza hali ya dharura ya afya ya umma kutokana na kukabiliwa kwa uhaba wa dawa muhimu na vifaa vya matibabu.

Rais Duma Boko alitoa tangazo hilo katika hotuba aliyoitoa kupitia televisheni siku ya Jumatatu, akiweka mpango wa mamilioni ya pauni kurekebisha mlolongo wa mgawo wa huduma za afya utakaosimamiwa chini ya uangalizi wa kijeshi.

Kudhibiti uhaba huo litakuwa jambo “nyeti sana kwa bei kutokana na hazina yetu ndogo,” aliliambia taifa.

Uchumi wa Botswana umekumbwa na mdororo katika soko la kimataifa la almasi, kwani ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa almasi duniani.

Tatizo hili lililochochewa zaidi na upunguzaji wa misaada ya Marekani, limewaacha Wabotswana wengi kati ya raia 2.5m wakikabiliwa na ukosefu wa ajira na viwango vya juu vya umaskini, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.

“Kazi hiyo itasalia bila kukoma hadi mlolongo mzima wa manunuzi utakapowekwa sawa,” Boko alisema katika hotuba yake, akitangaza kwamba wizara ya fedha imeidhinisha pula milioni 250 za Botswana (sawa na £13.8m) kwa ufadhili wa dharura.

Rais Boko alisisitiza kuwa shehena ya kwanza ilianza kusafirishwa mara moja kutoka Gaborone, mji mkuu, huku maeneo ya vijijini yenye uhitaji mkubwa yakipewa kipaumbele.

“Bei za sasa za dawa zimepanda mara tano hadi kumi zaidi ya kawaida. Katika hali ya sasa ya kiuchumi, hali hii haiwezi kudumu,” aliongeza Boko.

Mapema mwezi huu, wizara ya afya ya nchi hiyo ilitoa tahadhari kwamba inakabiliwa na “changamoto kubwa”, ikiwa ni pamoja na uhaba wa matibabu na madeni ya zaidi ya Pula bilioni moja (Sh187 bilioni).

Sehemu kubwa ya madeni hayo yalitokana na wagonjwa kulazwa katika hospitali za kibinafsi kwa huduma ambazo hazikupatikana kwa umma.

Uhaba uliotajwa na Waziri wa Afya, Dk Stephen Modise ni pamoja na ule wa dawa na vifaa vya kudhibiti saratani, matibabu ya VVU na kifua kikuu miongoni mwa mengine.

Kabla ya kupunguzwa kwa misaada ya Marekani iliyotolewa na Rais Donald Trump, Marekani ilifadhili theluthi moja ya udhamini wa VVU nchini Botswana, kulingana na UNAIDS.

Kiini cha kupungua kwa bajeti ya taifa kutokana na kuyumba kwa soko la kimataifa la almasi. Botswana ikiwa na idadi ya watu milioni 2.5 ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa almasi duniani na huchangia karibu asilimia 80 ya mapato yote ya fedha za kigeni nchini humo.

Botswana ni nchi ya nne barani Afrika kwa kipato kikubwa cha mtu mmoja mmoja kwa mwaka ikiwa ni Dola 7,640 (Sh19.2 milioni) nyuma ya Ushelisheli Dola 220,000 (Sh55.2 milioni) , Mauritius Dola 13,000 (Sh32.6 milioni) na Gabon Dola 9,290 (sh23.3 milioni).

Hata hivyo, mauzo ya almasi yamepungua kwa miaka ya hivi karibuni, hali iliyosababisha serikali kukosa fedha kiasi cha kusitisha baadhi ya manunuzi ya wizara mwezi uliopita.

Juni mwaka huu Kampuni kuu ya uzalishaji wa almasi ya Botswana kutangaza kusitisha uzalishaji katika baadhi ya migodi yake huku sababu kuu ikitajwa kuwa kushuka kwa muda mrefu kwa mahitaji ya almasi duniani.

Debswana ambayo ni kampuni ya ubia kati ya serikali ya Botswana na kampuni kubwa ya uchimbaji madini ya De Beers ilishuhudia mapato yake ya mauzo yakipungua kwa karibu asilimia 50 mwaka jana kwa mujibu wa shirika la habari la BBC.

Botswana ni mzalishaji mkubwa zaidi wa almasi duniani kwa thamani ambayo inachangia robo ya pato la taifa (GDP) la nchi hiyo kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Debswana ilinukuliwa na vyombo vya habari vya ndani ikisema kuwa uzalishaji wa mwaka huu utapunguzwa hadi karati milioni 15 sawa na upungufu wa takriban asilimia 40 ikilinganishwa na kiwango cha uzalishaji cha mwaka 2023.

Ripoti ya hali ya uchumi iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Julai mwaka huu inaonyesha kuwa katika mwaka ulioishia Juni 2025, dhahabu iliingiza 3,804.5 (Sh9.89 trilioni) ikiwa ni ongezeko kutoka dola bilioni 3,121.8 (Sh8.12 trilioni) mwaka uliotangulia.

Kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu kulitajwa kuchangiwa na bei nzuri katika soko la dunia na ununuzi kutoka BOT.

Ukuaji huu ndiyo pia ulichochea kukua kwa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi hadi kufikia dola za Marekani milioni 16,926.4, ikilinganishwa na dola milioni 14,380.2 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2024.

Pia Ripoti ya takwimu Msingi za Tanzania ya mwaka 2024 inaonyesha kuwa dhahabu iliingizia nchini Sh8.851 trilioni katika mwaka 2024.

Madini hayo yalibeba asilimia 69.07 ya Sh12.813 trilioni zilizopatikana katika mauzo yote ya bidhaa za asili ambayo yalipatikana katika mwaka 2024.

Mbali na dhahabu Tanzania pia iliweza kushuhudia ukuaji wa mauzo ya mazao mengine ikiwamo ya chakula hasa mahindi na mchele yaliongezeka zaidi ya mara tatu hadi kufikia dola milioni 501.3 (Sh1.25 trilioni) kutoka dola milioni 115.4 (Sh314.1 bilioni) ikichangiwa na kuongezeka kwa mahitaji kutoka nchi jirani.

Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi anasema kilichotokea kwa Botswana ni funzo kwa Tanzania na nchi nyingine kuhakikisha uchumi na biashara ya nje haitegemei kitu kimoja.

Hiyo ni kwa sababu soko la bidhaa hilo litakapoyumba uchumi wa nchi unakuwa katika hatari ya kuyumba kwa kiasi kikubwa tofauti na mauzo hayo yakitawaliwa na bidhaa tofauti.

“Sasa Botswana kwa miaka mingi uchumi wake ulikuwa ukitegemea almasi, siku za hivi karibuni ndiyo walianza kujenga sekta nyingine kama ufugaji ng’ombe na utalii lakini zilikuwa bado hazijaweza kuzaa matunda kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Amesema kwa Tanzania hali hiyo kutokea ni ngumu kwani licha ya dhahabu kuleta fedha nyingi ila yapo mapato yanayoingizwa kutokana na mauzo ya bidhaa nyingine ikiwamo za kilimo, viwandani.

“Uchumi wetu umetawanyika. Hautegemei kitu kimoja kama wao wanavyotegemea sana almasi. Labda huko mbeleni gesi ikichimbwa na kuchakatwa kwa kiasi kikubwa uchumi tukapata fedha nyingi ndiyo uchumi wetu unaweza kusema tunategemea sana gesi ni hatari kwani ikitokea mabadiliko ya bei au kuathirika kwa soko na sisi tunaathirika moja kwa moja,” amesema Dk Olomi.

Ili kutojikuta kwenye anguko kama la Botswana, Mtaalamu wa Uchumi Profesa Aurelia Kamuzora yeye anapendekeza nguvu kubwa kuongezwa katika kujenga sekta mbalimbali ikiwamo za kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa.

“Tusijione kuwa tunaweza kufanya wenyewe, tualike watu waje watusaidie kuongeza thamani mazao yetu, madini ili tuweze kutanua wigo wa kupata fedha zaidi badala ya kutegemea kitu kimoja,” amesema.

Hilo liende sambamba na kuweka mifumo mizuri inayosimamia mazao ya kilimo ikiwamo kahawa ambayo inauzwa sana katika masoko ya nje ili nchi iweze kutengeneza fedha nyingi za kigeni.

“Haya yatawezekana kwa kuwawezesha watu wenye nia ya kufanya mambo makubwa katika eneo hili, mtu akianzisha kitu kizuri kinachoweza kuleta fedha za kigeni taasisi za fedha ziangalie namna ya kumuwezesha kwa kumpa mikopo ili aweze kuwekeza zaidi katika kile anachokifanya,” amesema Profesa Kamuzora.

Amesema ili biashara ifanikiwe haipaswi kuachwa chini ya uangalizi wa mtu mmoja bali kufungamanishwa na sekta nyingine ili uwekezeshaji unaenda sambamba na kuwapo kwa mazingira mazuri.

Mitaji pia ni jambo alilogusia akisema uwezeshaji wa wananchi katika kutafuta mitaji pia ni jambo linapaswa kuangaliwa ili sekta nyingine ziweze kusonga mbele.

“Katika hili hatuwezi kukataa kuendelea kualika wageni waendelee kusimama na kufanya kazi katika maeneo ambayo hatuyamudu kwani wakiondoka inaweza kuathiri nchi badala yake tunaweza kujifunza kutoka kwao,” amesema.

Naye Mtaalamu wa Uchumi, Oscar Mkude anasema tatizo la karibu asilimia 80 ya mahitaji yao wananunua kutoka nje kwa kutegemea madini ya almasi na kile kinachopatikana katika utalii.

Amesema hali hiyo inafanya nchi zinazonunua almasi au kuleta watalii wakipata shida nchi yao nayo inakosa mapato na hata wachimbaji wakipata shida nchini mwao na uchumi wa nchi unaathirika moja kwa moja.

Amesema kitendo cha Marekani kuondoa misaada na kuongeza tozo katika baadhi ya vitu kwa pamoja kuathiri uchumi wao moja kwa moja kwa sababu ni sehemu wanazotegemea.

Amesema nchi inaweza kujilinda kwa kuwa na vyanzo vingi vya kujenga uchumi ili kimoja kinapo athiriwa unaweza kutumia vyanzo vingine kuendelea kujenga uchumi kwani ni ngumu vyote kuathiriwa kwa pamoja.

“Wakati vyanzo vingine vikiathiriwa vingine vitaendelea kujenga uchumi, wakati wa Uviko-19 utalii ulipokuwa ukitetereka shughuli kama kilimo ziliendelea kama kawaida hali iliyofanya Tanzania kuweza kujilinda katika kushuka uchumi kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na maeneo mengine,” anasema.