Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewaonya wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwapeleka watoto kwenye vilabu vya usiku, likieleza kuwa maeneo hayo yanachochea mmomonyoko wa maadili na kuwaweka watoto katika hatari ya ukatili wa kijinsia na kiafya.
Onyo hilo limetolewa Agosti 28, 2025 na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Iringa, Elizabeth Swai, kuwa vilabu vya usiku si sehemu sahihi kwa makuzi ya watoto.
Aliwakumbusha wanawake na wazazi kwa ujumla kuwa kitendo hicho kimekuwa chanzo cha ongezeko la manyanyaso ya kijinsia na mafunzo potofu kwa watoto.
“Hatushauri sana mwende na watoto vilabuni, huko wanaangalia sinema zisizo na maadili na hata kufanya biashara usiku ni marufuku kwa watoto. Hali hii inachangia ongezeko la ukatili na manyanyaso ya kijinsia,” amesema Elizabeth.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania kutoka Dodoma, Henry Mwaibambe aliyeshiriki uzinduzi wa Kituo kipya cha Polisi Tanangozi ambacho ujenzi wake umegharimu zaidi ya Sh58.1 milioni.
Katika hafla hiyo, Mwaibambe amesema Jeshi la Polisi limesaidia zaidi ya Sh8 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa muhimu vya kituo hicho, huku mfanyabiashara Sufian Mkude akijitolea Sh58.1 milioni kugharimia ujenzi mzima.
Mkude alisema mchango wake umetokana na kuguswa na changamoto za usalama katika eneo hilo.
“Nilinunua kiwanja kwa Sh15.5 milioni na kutoa Sh42.6 milioni kwa ajili ya ujenzi. Niliona ni wajibu wangu kusaidia kupunguza uhalifu, ajali na changamoto nyingine za kijamii,” amesema Mkude.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, aliyekuwa mgeni rasmi, amesema kituo hicho kitawapunguzia wananchi wa Tanangozi usumbufu wa kusafiri hadi Ifunda au Iringa mjini kutafuta huduma kwa polisi.
“Kituo hiki kitaboresha usalama na kuchochea shughuli za kibiashara. Nimewaagiza Tanroads kupanua barabara ili kuongeza fursa za biashara na kukuza uchumi wa eneo hili,” amesema James.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, amesema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa Jeshi la Polisi kuwasogezea wananchi huduma za usalama, huku akisisitiza jamii kushirikiana na polisi kulinda kituo hicho na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa sheria.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Tanangozi, Filibert Malega, pamoja na wananchi wengine walishukuru kwa mradi huo, wakisema utasaidia kupunguza ajali, kushughulikia haraka ukatili wa kijinsia na kuimarisha usalama wa eneo lao.
Mwadawa Benito, mkazi wa Tanangozi, amesema: “Tabia ya kina mama kukaa na watoto vilabuni usiku imekuwa kero kubwa hapa. Kwa kuwa sasa kuna kituo cha polisi karibu, tunaamini hali hiyo itapungua.”