Morogoro/Mwanza. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea na kampeni kikiahidi kuirejeshea Morogoro hadhi yake ya kuwa mkoa wa viwanda, huku ikieleza itakachowafanyia wananchi wa Mwanza.
Mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 29, 2025 akiwa mkoani Morogoro ameahidi kuurejesha katika hadhi yake kama mkoa wa viwanda ili kuibua fursa nyingi za ajira kwa wananchi.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa urais wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi akiwa mkoani Mwanza ameeleza CCM itakachowafanyia wananchi mkoani humo ikipewa ridhaa ya kuongoza tena dola, akizitaja sekta za elimu, afya, miundombinu ya barabara, huduma za maji na nyingine za kijamii kuwa kipaumbele.
Samia, anayetetea kiti cha urais amewasili Morogoro saa nne asubuhi kwa usafiri wa treni ya kisasa (SGR) na kufanya mikutano miwili ya kampeni akianzia Ngerengere na kuhitimisha katika uwanja wa Tumbaku, Morogoro mjini.
“Katika miaka mitano ijayo, tunakwenda kuirudisha Morogoro kuwa mkoa wa viwanda. Mtakumbuka mkoa huu ulikuwa na viwanda vingi lakini sasa havipo, tutavifufua na kuanzisha vingine,” amesema.
Amesema reli ya SGR itachochea maendeleo ya viwanda akiahidi watajenga vituo vya kupoza umeme maeneo ya viwanda ya Kilosa na Mvomero.
Pia, itajenga maghala matano wilayani Kilosa hasa kwenye ushoroba wa reli ya SGR, ambao wanalenga kuufanya kuwa wa viwanda.
Samia ameahidi kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya hasa kwa kuongeza zahanati na vituo vya afya. Vilevile, kukamilisha ujenzi wa maabara na wodi ya mama na mtoto ya Mafiga.
Ameeleza wataanza utekelezaji wa bima ya afya kwa wote kwa majaribio ndani ya siku 100 za kwanza, baada ya kuapishwa endapo atachaguliwa.
“Tutajenga soko la kisasa hapa Morogoro kwa ajili ya wajasiriamali na wamachinga,” amesema.
Ameahidi ujenzi wa kituo kikubwa cha mikutano mkoani humo ili kuuchangamsha mji huo na kuufanya kuwa wa kisasa.
“Tunataka watu waje kutembea kikazi, kibiashara au kitalii katika Mkoa wa Morogoro,” amesema.
Mbali ya hayo, ameahidi Serikali kuendelea kutoa hati za ardhi za kimila ili kumaliza migogoro ya ardhi.
Akizungumza na wananchi wa Ngerengere, Samia ameahidi ujenzi wa barabara ya Bigwa – Kisaki kwa kiwango cha lami, ujenzi wa kituo kikubwa cha afya na ghala la mazao.
Amesema kituo cha Ngerengere ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Morogoro vijijini ambao wengi ni wakulima, hivyo Wizara ya Kilimo na ile ya Uchukuzi itajenga ghala.
Kuhusu barabara amesema Serikali inajenga ya Ubena Zomozi yenye urefu wa kilomita 24 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh20 bilioni.
Mgombea ubunge jimbo la Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Samia ana uthubutu bila makeke, hayumbishwi, ni mkweli kwa anayoyaamini na amejaliwa moyo wa utu.
Profesa Kabudi amesema Morogoro ni kitovu cha nishati nchini kwa kuwa na vyanzo vikuu vya umeme kama vile Kidatu, Kihansi na Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).
“Mkoa wa Morogoro ni kitovu cha kilimo cha mazao yote; mahindi, mpunga, matunda. Pia, reli ya SGR imeleta mabadiliko mengi hasa katika Wilaya ya Kilosa ambayo ina vituo vingi katika mkoa huu,” amesema.
Amesema umeme umegusa maisha ya watu, hali zao za maisha zimebadilika na uchumi wao umeimarika kutokana na fursa zilizoletwa na nishati hiyo.
“Kwa upande wa nishati safi, Samia ni kiongozi mwanamapinduzi katika kuimarisha hali bora ya maisha ya wananchi kwa kulinda afya zao,” amesema.
Naye mgombea ubunge Morogoro Mjini, Abood Abdulaziz amesema katika miaka minne ya utawala wa Rais Samia, mambo mengi yamefanyika katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu.
Mgombea ubunge Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ amemuomba Samia kujenga barabara ya Bigwa – Kisaki kwa kiwango cha lami kwani kimekuwa ni kilio cha wananchi wa maeneo hayo.
Akihutubia mkoani Mwanza, Dk Nchimbi ameahidi kuwafuatilia na kuwawajibisha wabadhirifu wa mali za umma.
Katika mikutano ya kampeni iliyofanyika wilaya za Kwimba na Nyamagana, ambako pia wamenadiwa wagombea udiwani na ubunge wa CCM, Dk Nchimbi ameeleza yale ambayo Serikali ya chama hicho imeyafanya miaka minne chini ya Rais Samia na watakayofanya wakipewa tena ridhaa kuongoza dola.
Akiwa Kwimba, Dk Nchimbi amesema: “Tunakuja tena kuwaomba mtuchague kwa sababu tumefanya mengi zaidi ya kiwango. Ilani yetu chini ya Mama Samia imetekelezwa na kila mmoja ameona.”
“Kutokana na kazi kubwa ambayo tumeifanya, ndiyo maana zaidi ya wagombea wetu 91 wa udiwani wa Mwanza wamepita bila kupigwa,” amesema Dk Nchimbi.
Aliposimama Buhongwa, wilayani Nyamagana kusalimia akitokea Kwimba amesema watu wa Mwanza ukifanya vibaya watakupinga, ukifanya vizuri watakupongeza:
“Na hili la madiwani wetu kupita bila kupingwa na chama chochote ni ishara tumefanya mazuri na mkitupa tena ridhaa niseme Mama Samia na mimi (Dk Nchimbi) yajayo yanafurahisha,” amesema.
Huku akishangiliwa, Dk Nchimbi hadi wiki iliyopita alikuwa Katibu Mkuu wa CCM amesema: “Kasi ya miaka minne mmeiona, itakuwa mara dufu katika kuleta na kusimamia miradi ya maendeleo.”
Dk Nchimbi amesema katika kipindi cha miaka minne, hospitali mpya imejengwa Kwimba, vituo vya afya kutoka 50 hadi 61 na hilo ni katika kuzingatia afya za wananchi. Watumishi wa afya amesema walikuwa 335 na sasa wapo 513 kwa wilaya hiyo pekee.
Amesema shule za sekondari zimejengwa kutoka 34 hadi 41. Madarasa mapya yameongezeka kutoka 438 hadi 709, majisafi yameongezeka kutoka asilimia 36 hadi 77
“Yaani kila Wana-kwimba 100, wanaopata majisafi 77. Vijiji vyenye umeme vimeongezeka kutoka 60 hadi 119. Ukisema CCM haijafanya kitu huyu atakuwa na lake jambo. Yapo mambo mengi yamefanyika, viongozi wetu wa ngazi mbalimbali watayazungumza kwani tumeyafanya pamoja,” amesema.
Katika miaka mitano ijayo, Dk Nchimbi ameahidi watajenga zahanati mpya 20.
“Ukiamka unaumwa, ukitoka nje ukitizama tu unaiona. Ujenzi wa zahanati nne ambazo ziko kwenye hatua mbalimbali ili ziwe zahanati 44,” ameahidi.
Pia ameahidi kujenga vituo vipya vitano vya afya na katika hospitali ya wilaya wanakusudia kuiimarisha ili huduma za kibingwa zipatikane.
Pia, ameahidi kuongeza madarasa, walimu na mitalaa, akisema wanataka watoto kuelimishwa.
Kuhusu huduma za maji, Dk Nchimbi amesema wataongeza upatikaji wa maji ili kila Wanakwimba 100, wanaopata majisafi iwe asilimia 90.
Katika ujenzi wa barabara amesema utazingatiwa kwa kiwango cha lami. Vilevile, uboreshaji wa masoko itakuwa kipaumbele ili wakulima wanapolima wawe na uhakika wa mazoa yao kupata soko.
Awali, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge maarufu ‘smart’ amesema akiwa katibu mkuu Dk Nchimbi alifanya mambo mengi na kukifanya chama hicho kuwa imara.
Kuhusu maandalizi ya uchaguzu amesema: “Sisi Mkoa wa Mwanza tunaingia katika uchaguzi tukiwa kifua mbele kwani tuna mtaji wa kura kutoka kwa wanachama wetu waliojiandikisha zaidi ya laki saba na wengine wanaotuunga mkono.”
“Tumewaletea wagombea wazuri wa udiwani na ubunge tena vijana na tunawaomba tuendeleze umoja na amani. Niwaombe wana CCM wenzangu, tufanye kampeni za kistaarabu na zenye tija.”