Dodoma. Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Abdulla, amekabidhi kompyuta mpakato (laptop) 30 kwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi ili ziwasaidie katika kukamilisha majukumu yao kwa wakati.
Taarifa iliyotolewa na kitengo cha Habari kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, inaonyesha makabidhiano hayo yalifanyika jana Alhamisi Agosti 27,2025 katika hafla fupi ukumbi wa Wizara hiyo uliopo Mtumba Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu huyo, Abdulla amemwambia Wakili Mkuu kuwa, Wizara kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali imekabidhi vifaa hivyo vya Tehama ili kusaidia na kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo wanaamini ni chombo muhimu hasa katika kipindi cha sasa.
“Tunatambua namna ambavyo mnakabiliana na majukumu makubwa ya kiserikali na katika kutafuta haki za watu, vifaa hivi vikawe msaada kwenu ili mtimize majukumu yetu kwa haraka,” amesema.
Akipokea vifaa hivyo, Dk Possi ameishukuru Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa msaada huo, akibainisha kuwa vifaa hivyo vinakwenda kurahisisha utekelezaji wa majukumu ofisi hiyo kwa kiwango kikubwa hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa lipo katika mageuzi makubwa kwenye uchumi wa Kidijitali.
“Sisi Mawakili wa Serikali, shughuli zetu nyingi kwa takribani asilimia 90 zinafanyika mahakamani na zinategemea matumizi ya kompyuta, hivyo, hatua hii ya kutukabidhi vifaa hivi ni ya wakati mwafaka na inaendana moja kwa moja na shughuli zetu za kila siku,” alisema Dk Possi.
Wakili Possi ameitaka wizara hiyo kuendelea kuwezesha mageuzi ya kidijitali nchini, ikiwemo kuhakikisha kunakuwa na gharama nafuu za huduma za intaneti kwa wananchi na taasisi.
Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za Tehama wa wizara hiyo, Mohammed Mashaka amesema kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Serikali inaendelea kugawa vifaa vya Tehama kwa taasisi mbalimbali ili kurahisisha huduma, kuziunganisha taasisi hizo ili kuhakikisha huduma na rasilimali muhimu za kidijitali zinapatikana.