Kauli ya kwanza ya RC Makalla akitaja mikakati kukuza uchumi Arusha

Arusha. Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla ameomba ushirikiano kutoka kwa viongozi na wananchi ili kuendeleza shughuli za kiuchumi zikiwemo sekta ya utalii na kilimo cha maua na mbogamboga.

Akizungumza leo Ijumaa, Agosti 29,2025 baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwaajili ya kuanza majukumu yake baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan amesema anao uzoefu wa kutosha kutekeleza kazi aliyopewa aifanye.

“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini na kunipa nafasi za uongozi katika serikali anayoingoza, nataka nimhakikishie imani aliyonayo na matarajio kwangu sitamuangusha, nitasimamia shughuli za serikali kwenye mkoa huu kikamilifu,” amesema Makalla.

Amesema Mkoa wa Arusha ni moja ya maeneo ya kimkakati nchini na atasimamia kikamilifu maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta ya utalii ambayo inachangia pato kwa taifa na ajira kwa ujumla.

“Niwahakikishie kuwa sikuja kutangua torati, bali nimekuja kuitimiza, mazuri yote yaliyofanywa na viongozi wenzangu walionitangulia nitayaendeleza kwa maslahi mapana ya wananchi, nachukia uzembe kwenye utendaji kazi, mimi ni mtu wa “site” nitawafata wananchi walipo nikianzia na wilaya ya Ngorongoro,” amesema Makalla.

Kuhusu uzoefu wake kwenye utumishi wa umma amesema ana ufahamu mkoa wa Arusha vizuri na ameshiriki kikamilifu kwenye mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa sasa hivi wakati akiwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji na wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro alikuwa mwenyekiti wa wakuu wa mikoa ya Arusha na Manyara.

Makalla amesema atatumia uzoefu alioupata akiwa mkuu wa mikoa mitano ya Kilimanjaro, Mbeya, Katavi, Dar es Salaam na Mwanza kuhimiza shughuli za kiuchumi kwa wananchi na kuhimiza viongozi kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi huko walipo.

Ameongeza kuwa hatavumilia kuona wananchi wanabeba mabango yenye kero zao mbele ya viongozi wa juu wakati changamoto nyingi zinatoka kwenye ngazi ya vijiji, kata na halmashauri badala ya wananchi kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa kueleza kero zao.

Kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, amesema atahakikisha shughuli za kampeni na uchaguzi zinafanyika kwa amani na hatavumilia vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjivu wa amani.

Makalla amechukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi aliyeteuliwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Katibu wa Itikati, Uenezi na Mafunzo.