Aliyempinga Mpina afukuzwa ACT Wazalendo

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimemvua uanachama kada wake Monalisa Ndala ambaye hivi karibuni aliibuka kupinga uteuzi wa mgombea urais wa chama hicho Luhaga Mpina.

Monalisa amevuliwa uanachama na Kikao cha Kamati ya Uongozi wa chama hicho tawi la Mafifi, kilichofanyika Agosti 28, 2025 Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho leo Agosti 29, 2025 kupitia kwa Katibu wa tawi hilo Neema Kivamba, imeeleza kuwa kuanzia siku ya kukaa kwa kikao hicho Monalisa si mwanachama wa ACT Wazalendo.

“Uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa Katiba ya ACT Wazalendo ya mwaka 2015, Toleo la 2024, hususan Ibara ya 8(2)(a)(b), Ibara ya 13(1)(c)(d) na Ibara ya 97(b)(d),”imeeleza taarifa hiyo.

Kamati hiyo imeeleza kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 97(1)(d), imejiridhisha kuwa Monalisa ameshindwa kutekeleza matakwa ya Katiba ya chama, hivyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa mwanachama.

Taarifa hiyo ya Neema imeeleza kuwa  kuanzia siku ya kikao, jina la Monalisa limeondolewa rasmi kwenye regista ya wanachama wa tawi na kadi yake ya uanachama yenye namba 0000245 imefutwa.
Ameongeza kuwa tayari taarifa zimetumwa  Idara ya Oganaizesheni, Uchaguzi na wanachama makao makuu ya chama kwa ajili ya kupewa mwanachama mwingine.

Kufutwa uanachama kwa kada huyo kunakuja siku chache tangu alipowasilisha malalamiko ya kupinga uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea urais wa chama chake Agosti 19, 2025.
Pingamizi hilo, Monalisa aliwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa  na hatimaye Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikamuengua mgombea wa urais wa chama hicho.
 Mpina aliyeteuliwa na Chama cha ACT – Wazalendo kuwania urais alienguliwa na INEC kufuatia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kukubaliana na hoja za Monalisa.

Sababu kuu iliyoelezwa na Monalisa ni ni kwamba Mpina alipata uanachama Agosti 5, 2025, nje ya muda wa kisheria wa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, ambapo ilipaswa kuwa kabla ya Mei 25, 2025.