TANESCO RUVUMA: VIFAA VYA KISASA VYA KUPIKIA VYA UMEME NI NAFUU NA SALAMA.


Songea- Ruvuma.

Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Ruvuma, limewataka wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake watumie majiko ya umeme ya kisasa aina ya induction na pressure cooker, baada ya kubainika kuwa vifaa hivyo vinatumia umeme kidogo na ni nafuu kwa matumizi ya kila siku.

Akizungumza katika kongamano la wafanyabiashara wadogo kuhusu fursa za kiuchumi mkoani Ruvuma lililofanyika katika ukumbi wa Songea Club, leo Agosti 29, 2025, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Alan Njiro amesema tafiti zilizofanywa na shirika hilo zimeonyesha kuwa matumizi ya vifaa hivyo ni salama na yanapunguza gharama za upishi kwa kiasi kikubwa.

“Zamani watu walikuwa wanaogopa kutumia umeme kwa ajili ya kupikia kwa sababu majiko yalikuwa ghali, lakini kwa sasa teknolojia imeboreshwa, vifaa hivi vinapika kwa haraka, vinatumia umeme kidogo,” alisema Njiro.

Aidha amewahimiza wajasiriamali, hususan mama lishe, kuchangamkia fursa hiyo kwa kununua vifaa hivyo ili kurahisisha shughuli zao za kila siku, ameongeza kuwa matumizi ya umeme ni salama na rafiki kwa mazingira ikilinganishwa na kuni na mkaa.

Mbali na hayo Njiro ametoa rai kwa wananchi kuepuka ununuzi wa vifaa vya umeme vilivyopitwa na wakati kutoka kwa watu, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia vifaa vyenye teknolojia ya energy saver kama vile taa na friji ili kupunguza matumizi makubwa ya umeme majumbani na katika biashara.

Katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wote, amesema TANESCO kupitia mradi wa ujazilizi itatoa elimu kwa wakazi wa maeneo ya pembezoni, huku wakipelekewa vifaa hivyo vilivyofanyiwa utafiti wavione ili kuhakikisha wanapata manufaa ya matumizi ya umeme wa uhakika.