Dodoma. Asilimia 60 ya Watanzania wanatafuta tiba za asili, ingawa hakuna utafiti zaidi unaoeleza iwapo kundi hilo linatoka vijijini au ni wananchi waishio mijini, imeelezwa.
Takwimu hizo zimetolewa leo Ijumaa Agosti 29, 2025 na Dk Ahmad Makuwani, Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya.
Dk Makuwani amesema Serikali imeridhia na kutoa kipaumbele kwa tiba asili kwa kuwa inasaidia.
Ametoa kauli hiyo alipofungua kongamano la nne la kisayansi la tiba asili katika jijini Dodoma. Ameeleza upo utafiti wa kisayansi unaothibitisha hilo.
Amesema kuna maeneo dawa za asili zimekuwa zikifanya vizuri zaidi ya dawa za kitaalamu, akitoa mfano wakati wa janga la Uviko 19.
Hata hivyo, amesema ni muhimu wataalamu wakaenda mbele zaidi, hasa katika utafiti kuliko kuendelea kutumia vitu kwa kufuata simulizi ambazo zinaweza kuwaumiza au kuwachelewesha.
“Katika kipindi cha Covid (Uviko), tiba asili ilionekana kusimama na kutusaidia zaidi, hata wakati mwingine kuliko hizi dawa za kitaalamu, labla kinachokosekana hapa ni mifumo ya rufaa ambayo kama itakuwapo ingeweza kusaidia zaidi tukawa salama,” amesema.
Dk Makuwani aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya katika kongamano hilo, amesisitiza uwepo wa ubora wa maabara kwa ajili ya kufanya tafiti zaidi za tiba asili ili kuwa na dawa zenye ubora.
Mbali ya hayo, amewataka Watanzania wenye ujuzi kuwarithisha zaidi vijana, hatua itakayosaidia pia kuitunza misitu.
Amesema wataona namna ilivyo bora na faida ya misitu ya asili kuliko ilivyo sasa wengi hawaoni faida katika mazao ya misitu.
Profesa Said Aboud, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) amesema hadi sasa Tanzania ina hospitali 14 za rufaa ambazo zinatoa huduma jumuishi katika dawa 26.
Amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Hospitali ya Ocean Road zinaendelea kukamilisha utafiti wa tiba asili kwenye magonjwa ya saratani ya matiti na tezi dume.
Sheria ya NIMR ya mwaka 1979 inaitaka mamlaka hiyo kufanya utafiti na kuhakikisha dawa zinazotolewa haziendi kuwaumiza watumiaji.
Akizungumzia kuhusu utafiti na ucheleweshaji wa utoaji majibu, amesema waganga wa tiba za asili wengi hawapendi kupeleka sampuli zao kwenye maabara kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuhofia huenda watanyang’anywa umiliki wao. Amesema jambo hilo haliwezekani.
“Kingine muhimu watu wakajua ni kuwa, taasisi zinazoshughulika na dawa ziko tatu; tupo sisi NIMR, wapo Baraza la Tiba na yupo Mkemia Mkuu, kwa hiyo kila mmoja anatakiwa kujiridhisha ndipo tuone kama inafaa kwani kuna dawa mtu anaweza kuitumia ikasaidia na wakati huohuo ikawa inamuumiza upande mwingine,” amesema.
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili, Profesa Joseph Otieno amesema wanaendelea kufanya maboresho katika utoaji wa tiba asili kwa kushirikiana na Serikali, kwani jamii ya watu wengi inaonyesha kupenda huduma hiyo kwa sasa kuliko inavyodhaniwa.