Dar es Salaam. Katika kukuza kampuni changa nchini, Chama cha Kampuni Changa Tanzania (TSA) kimeingia makubaliano na kampuni ya uturuki ya AfrIcapital Investment Holdings Ltd, kwa lengo kusaidia na kuwezesha upatikanaji rahisi wa masoko na mitaji kwa biashara changa.
Chama hicho kimesema kina matumaini makubwa ya kupata matokeo mazuri kutokana na ushirikiano huu utakaodumu kwa miaka mitatu ambapo pamoja na mambo mengine kampuni hiyo itasaidia mbinu za kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo wamiliki wa kampuni changa nchini.
Akizungumza leo Agosti 29,2025 baada ya hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo ya kuwasaidia na kuwaendeleza waanzilishi wa biashara (startups) na wabunifu nchini Tanzania, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TSA, Zahoro Muhaji amesema, “kuna kasi ndogo ya maendeleo ya kampuni changa nchini, na hii inasababishwa zaidi na ukosefu wa fedha,” amesema.
Kwa mujibu wake, takribani kampuni changa 1,200 zimeanzishwa na mtaji wake hadi sasa ni dola za kimarekani milioni 3, sawa na Sh7.5 bilioni hali kiwango ambacho bado hakionyeshi mafanikio kufikia lengo la mwaka 2050.
Ili kuchochea mafanikio hayo, TSA imesema wana matumaini ya kupata msaada zaidi ya kukuza kiwango cha uwekezaji katika biashara changa.
Mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa AfrIcapital Ltd, Burak Buyuksarac amesema “kupitia ufadhili wa mitaji ya hisa pamoja na matumizi ya njia za uwekezaji wa mitaji, wamiliki wa biashara changa mpya nchini hazitalazimika kuwa na dhamana ili kupata fedha za kuwekeza kwenye biashara zao,” amesema.
Akifafanua kuhusu ufadhili wa mitaji, utakaowezeshwa kupitia ushirikiano Buyuksarac amesema hiyo njia ya kukusanya mtaji kwa kuuza sehemu ya umiliki wa kampuni kwa wawekezaji ili kupata fedha.
“Badala ya kukopa fedha kupitia benki, kampuni huuza itauza hisa hivyo wawekezaji wanakuwa sehemu ya kampuni,” amesema.
Kwa mujibu wa Buyuksarac, programu mbili ambazo zinalenga kuongeza mwamko na fursa kwa wajasiriamali vijana nchini zinatarajiwa kuzinduliwa katika kipindi cha miezi miwili ijayo katika Maadhimisho ya wiki ya Biashara Changa (Startup Week) yatakayofanyika kuanzia Oktoba 13 hadi 17 mwaka huu.
Chama cha Kampuni changa Tanzania (TSA) ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyosajiliwa na kufanya kazi kama jukwaa la wanachama na mwavuli wa mfumo mzima wa biashara changa nchini.
Kwa miaka kadhaa sasa, chama hiki kimekuwa kikijihusisha kikamilifu katika kutetea mabadiliko ya sera pamoja na kuhamasisha ukuaji wa mazingira ya biashara changa hapa nchini.