Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa Dola za Marekani 10 bilioni zaidi ya Sh25 trilioni na kampuni kutoka Qatar.
Kiasi hicho cha fedha kinalenga kutumika katika sekta miradi ya kimkakati na kipaumbele ukiwemo uchumi wa buluu, utalii, uhifadhi wa mafuta, bandari na nishati ya umeme.
Mkataba huo umesainiwa leo Agosti 29, 2025 Ikulu Zanzibar, kwa upande wa Qatar umewakilishwa na mmoja wa wanafamilia ya Kifalme wa Qatar, Sheikh Mansour Bin Jabor Bin Jassim Al Thani, ambaye pia ndiye mmiliki wa Kampuni ya Al Mansour Holding itakayotekeleza miradi hiyo.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema makubaliano hayo yatasaidia kufanya miradi ya pamoja na yatakuwa na maana kubwa kwa uchumi wa Zanzibar.
Amesema Zanzibar imeorodhesha miradi ya kimkakati ambayo wangependa kupata uwekezaji kutoka Qatar na wao wamekubali jambo hilo.
“Kwa kweli fedha hizi Dola za Marekani bilioni 10 ni nyingi sana zitafanya mambo mbalimbali ikiwemo kuhifadhi mafuta, ujenzi wa bandari, kumbi za mikutano na sekta nyingine,” amesema na kuongeza
“Kwa kweli sekta nyingi zimo kwenye mkataba huu, sekta zetu za kipaumbele kama vile sekta ya uchumi wa buluu na pia sekta ya nishati ya umeme,”
Dk Mwinyi amesema anajisikia fahari kubwa kwani wamepata watu wenye nia, dhamira na uwezo wa kifedha kwa kushirikiana na Serikali katika miradi hiyo mikubwa ya kimkakati.
Amesema hana shaka kwamba utekelezaji utakapoanza Zanzibar itakuwa imepata fedha nyingi za uwekezaji kutoka nje na za kutosha kuifanya miradi iende haraka kuliko walivyopanga kabla ya kuwapata wawekezaji hao.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, utiaji saini ni jambo la kwanza na hivi sasa ni mwanzo tu wa mambo ya utekelezaji kwani timu yao ya wataalamu ipo ili kufanya miradi hiyo kwa haraka.
Mkataba huo wa ushirikiano, kwa upande wa Zanzibar umesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Khamis Suleiman Mwalim.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff aliyehudhuria hafla hiyo, amesema ni hatua ya kupongezwa kwani miradi mingi itatekelezwa kupitia makubaliano hayo.