Bado Watatu – 13 | Mwanaspoti

LAKINI tulipomaliza kushuka ngazi na kuliona gari ambalo tulielekea kujipakia, kidogo alishituka. Pengine alilishitukia kuwa lilikuwa gari la usalama.

Hata hivyo, hakuniuliza kitu. Nilipojipakia katika siti ya dereva na yeye alijipakia katika siti ya upande wa pili akakaa.

Nikaliwasha gari tukaondoka. Sikumuuliza kitu mpaka tulipoikamata barabara ya Mikanjuni.

“Utanionyesha ni Mikanjjuni ipi anayoishi,” nikamwambia.

“Twende tu,” msichana akaniambia lakini alionyesha kuwa na mawazo.

Nilishuku ni lile gari ndilo lililomchanganya, lakini alishindwa kuniuliza kitu akaamua kubaki kimya.

“Hapo tairitatu, kata kulia,” akaniambia.

Nikakata kulia na kuendelea kwenda.

“Nyumba yake iko huo mtaa wa pili, utakata kulia tena,” akaniambia tena.

Nilipoufikia mtaa huo wa pili nikakata kulia.

“Nyumba ya pili kushoto.”

Sikuona nyumba. Niliona kiwanja tu.

“Hapa kwenye kiwanja?” nikamuuliza.

Nikasimamisha gari mbele ya kiwanja hicho lakini nilipotupa macho kwenye kile kiwanja nikaona kulikuwa na banda la uani la vyumba vitatu ambalo pia lilikuwa halijakamilika.

Ingawa lilikuwa limepauliwa kwa bati, lilikuwa halijapigwa lipu hali iliyoonyesha kwamba ujenzi wake ulikuwa unaendelea.

“Nyumba yake ndiyo ile?” Nikamuuliza Husna.

“Ndiyo anaishi pale,” Husna akanijibu huku akifungua mlango na kushuka.

Na mimi nikashuka na kumfuata. Tuliingia katika kile kiwanja na kusimama mbele ya mlango wa kwanza wa banda hilo.

“Sijui kama kuna watu humu,” msichana akasema huku akipiga hodi.

Licha ya kupiga hodi zaidi ya mara tatu hatukusikia jibu lolote. Kilichotupa moyo kwamba mwenyewe hakuwa mbali, redio ilikuwa ikisikika kwa ndani.

“Sijui wametoka kidogo?” Msichana akauliza kama aliyekuwa akijiuliza mwenyewe.

“Lakini redio inasikika ndani.”

Msichana aliugonga mlango, alipoona hakukuwa na majibu akajaribu kufungua mlango. Mlango ukafunguka.

“Mlango uko wazi.” akasema huku akiendelea kuufungua mlango huo lakini ghafla sote tulishituka.

Tuliona mwili wa mtu ukining’inia kwenye kitanzi ndani ya chumba hicho.

Niikamsikia Husna akipiga yowe.

“Oh! Lerry amejinyonga!”

“Huyo ndiye Lerry?” nikamuuliza.

“Lerry ndiye huyu. Sijui kaka yake yuko wapi?” Msichana akaniambia kwa taharuki.

Matukio yale yalinishangaza. Nilitarajia kama nitampata Lerry angetufumbulia hiki kitendawili, kumbe naye tunakuja kumkuta ameshanyongwa.

Kwa vile ule mchezo nilishaanza kuuzoea niliingia ndani ya kile chumba nikautazama vizuri mwili huo uliokuwa ukining’inia.

Ulikuwa mwili wa mtu mwenye umri wa kati ya miaka thelathini na thelathini na tano.

Ulikuwa umevaa tisheti ya rangi nyekundu na suruali aina ya jinzi ya rangi ya bluu. Miguuni alivaa viatu vya raba vya rangi nyekundu.

Jinsi mwili huo ulivyokakamaa ulionesha kuwa ulikuwa umekaa kwenye kitanzi hicho kwa muda mrefu.  Nilikisia kama hakuwa amenyongwa usiku uliopita, alinyongwa alfajiri sana.

Chumba hicho kilikuwa kama sebule. Kulikuwa na makochi matatu ya kizamani. Meza ndogo na kabati. Kulikuwa na mlango wa kuingilia chumba kingine. Nikaufungua na kuchungulia ndani.

Nilikuta kitanda, kabati na meza ndogo. Nikahisi kwamba kilikuwa chumba chake cha kulala.

Husna alipoona nimeingia katika chumba hicho, naye alinifuata. Macho yake yalikuwa mekundu.

“Sijui Frank yuko wapi jamani?” nikamsikia akisema peke yake.

Hakuwa akijua kuwa Frank ndiye aliyetangulia kunyongwa kabla hata ya Lerry.

“Hiki ndio chumba chake cha kulala?” nikamuuliza Husna nikimuonyesha mlango wa kile chumba.

“Unahisi nini, amejinyonga au amenyongwa?” Nikamuuliza.

Husna akabetua mabega yake.

“Sijui kama amenyongwa au amejinyonga mwenyewe. Wewe uliniambia Frank amekuja huku sasa yuko wapi?”

“Hatuwezi kujua, yeye aliniambia anakuja huku.”

“Sasa tutafanya nini?”

“La kufanya ni kupiga simu polisi.”

“Ndiyo, mimi ndiye nitakayepiga.”

Nikatoka nje ya chumba hicho. Nikatoa simu yangu na kukiarifu kituo cha polisi cha Chumbageni kuhusu lile tukio.

Dakika chache baadaye polisi na makachero wakawa wametinga katika eneo hilo. Ziliwasili gari mbili za polisi.

Wakati tunauondoa ule mwili wa Lerry kwenye kitanzi, niliona kipande cha karatasi kilichochomekwa kwenye shingo ya marehemu.  Kiliandikwa BADO MMOJA

Chini ya maandishi hayo kulikuwa na sahihi ile ile niliyoiona kwenye mwili wa Frank na kwenye mwili wa Lazaro. Chini ya sahihi kulikuwa na alama ya dole gumba.

Nikajiambia kimoyomoyo marehemu Thomas Christopher amefanikiwa kuwamaliza marehemu wenzake, sasa bado mmoja ambaye hakuwa akijulikana ni nani.

Nikatoka nje ya kile chumba na kumuuliza Husna aliyekuwa amekaa kwenye tofali akiwa amejiinamia.

“Huyu jamaa hakuwa na mke?”

“Alikuwa hajaoa bado.”

“Kuna ndugu yao mwingine unayemfahamu?”

“Frank aliwahi kunionyesha ndugu yake mwingine. Lakini nilimuona mara moja tu nyumbani kwa Frank na sijui anaishi wapi.”

“Atakuwa analo lakini silifahamu.”

“Umesema hujui anaishi wapi?”

“Sijui, sikuwahi kumuuliza na nilimuona siku moja tu.”

Nikahisi kwamba ilikuwa vyema niongee na ofisa upelelezi wa mkoa ambaye nilikuwa sijamfahamisha rasmi kuhusu lile tukio. Kwa vile sikutaka yule msichana asikie nilikuwa ninaongea nini, nikasogea kando kidogo na kumpigia ofisa upelelezi.

“Afande umeshapata taarifa ya huyu mtu mwingine aliyenyongwa huku Mikanjuni?” nikamuuliza.

“Bado sijapata taarifa. Ni nani aliyenyongwa?”

“Ni Lerry, yule jamaa ambaye ni ndugu yake Frank.”

“Hapa nipo Mikanjuni nyumbani kwake. Nililetwa hapa na mpenzi wake Frank ambaye nilikutana naye nyumbani kwa Frank leo akanileta hapa. Tulipofika ndio tukaukuta mwili huo unaning’inia kwenye kitanzi.”

“Eh! Hili sasa limekuwa balaa. Kila siku watu wananyongwa. Umepata fununu zozote kuhusu kunyongwa kwake?”

“Sijapata fununu. Katika hili banda lake yupo mwenyewe tu. Hakuna mtu yeyote.”

“Amenyongwa mahali gani?”

 “Mwili wake tumeukuta chumbani mwake uking’inia.”

 “Watu wa karibu karibu wanasemaje?”

 “Unajua hii si nyumba ni banda tu la uani. Hakuna watu wa karibu labda majirani ambao sidhani kama wana lolote wanalolifahamu.”

“Na huyo aliyengongwa leo ni mmoja wa wale watu ambao walihukumiwa kunyongwa?”

“Ndiyo. Na afisa magereza ameniambia wameshanyongwa.”

“Wale wa kwanza uliwakuta na kipande cha karatasi chenye maelezo na sahihi ya mtu ambaye tunadhani ndiye anayewanyonga, je huyo umemkuta na kikaratasi hicho?”

“Kimeandikwa BADO MMOJA. Yaani kuna mtu mmoja ambaye atanyongwa.”

“Umeshamgundua ni nani?”

“Unajua hawa watu ni ndugu. Sasa huyu msichana aliyenifikisha hapa ameniambia kuna ndugu yao wa mwisho ambaye hajui anaishi wapi. Nafikiri huyo ndiye aliyekusudiwa.”

“Huyo msichana tutahitaji kumhoji. Inaonekana anawajua vizuri hao watu. Njoo naye hapa ofisini kwangu atupe maelezo.”

“Sawa. Nitakuja naye.”

“Polisi wameshafika hapo?”

“Kama si lazima wewe kuwepo hapo, njoo na huyo msichana. Ninawasubiri.”

Nilikata simu nikamsogelea yule msichana ambaye alionekana wazi kuwa na sintofahamu kuhusu mimi na kuhusu tukio lililotokea.

“Mimi na wewe tunahitajika kituo cha polisi. Subiri niagane na hawa polisi,” nikamwambia msichana huyo kisha nikaingia katika kile chumba.

Mwili wa marehemu ulikuwa umelazwa chini. Nikampekua mifukoni na kuchukua simu yake kisha nikaacha maagizo muhimu kwa polisi hao kuhusu hatua za kuchukua.

Baada ya hapo nilitoka mle chumbani nikaondoka na yule msichana.

Wakati tumo ndani ya gari tukielekea ofisini kwa afisa upelelezi nilimwambia: “Ukweli ukidhihiri, uongo hujitenga. Sasa ukweli umeshadhihiri, uongo hauna budi kujitenga. Mimi sikuwa rafiki wa Frank kama nilivyokueleza hapo awali.”

Msichana alishituka akanitazama mara moja kisha akayarudisha macho yake kwenye kioo.

“Wewe ni nani?” Akaniuliza. Sauti yake ilionyesha alikuwa ameshaanza kupata hofu.

“Mimi ni kachero wa polisi. Nilikuwa nimemfuata Frank nyumbani kwake anipe maelezo kuhusu mtu ambaye inasemekana ni ndugu yake ambaye alikuwa amenyongwa huko Kisosora…”

Sikuwa nimemaliza sentensi yangu, nikanyamaza kidogo na kumtazama Husna kuona kama atashituka kumwambia hivyo.

Husna alishituka akaniuliza: “Ndugu yake yupi?”

“Anaitwa John Lazaro au jina jingine Ramadhani Unyeke”

“Frank hakupata kukueleza kuhusu ndugu yake aliyenyongwa?”

“Hakupata kunieleza hivyo.”

“Labda alikuficha lakini mtu niliyekutajia ni ndugu yake na mwili wake upo hospitali hadi sasa.”

“Kwani huyo Frank mwenyewe yuko wapi?’

“Natumaini ulikuwa hufahamu yaliyomkuta Frank. Frank siye aliyekutumia meseji wewe. Niliyekutumia meseji kukuita ni mimi. Niliona namba yako kwenye simu yake. Nilikuita ili utusaidie kutueleza kuhusu hawa watu.”

“Frank amepatwa na nini?” Husna akaniuliza.