Ligi Kuu yaipa jeuri Yanga, yatoa kauli ya kutisha

UMEIONA ratiba ya Ligi Kuu Bara? Basi bingwa mtetezi Yanga imeiona kisha bosi mmoja mzito wa klabu hiyo, ametoa tamko, wako tayari kwa msimu huku akiringia hesabu walizonazo kutokana na kikosi hicho kinachoendelea kujifua kwa sasa kambini Avic Town, Kigamboni Dar es Salaam.

Bosi aliyeyasema hayo ni Rodgers Gumbo, akiliambia Mwanaspoti wameipokea ratiba ya ligi kuelekea msimu mpya wa 2025/26 na kwamba timu yao ipo tayari kuendeleza rekodi zao.

Gumbo alisema kabla ya msimu kuanza, uongozi wa klabu hiyo ulishafanya hesabu kubwa kuanzia muundo wa kikosi chao kilichoongezewa nguvu kubwa pamoja na maboresho mengine ya kiutawala.

Bosi huyo anayeongoza Kamati ya Mashindano ya Yanga, alisema kuanzia usajili, walilazimika kungalia mbali kwa kutengeneza timu itakayokwenda kutafuta mafanikio makubwa Afrika badala ya kuangalia kipimo cha mashindano ya ndani.

“Tumeiona ratiba hatuna shida nayo sana, ninachosema, Yanga tupo tayari kwa msimu huu mpya ambao tutauanza kuanzia mchezo wa ngao ya jamii dhidi ya watani wetu Simba,” alisema Gumbo na kuongeza;

“Baada ya timu zilizopanda ligi, uongozi wetu ulishakaa chini na kufanya tathimini kubwa ya kikosi chetu, pia hata kuangalia wapinzani wetu lakini kikubwa tumetengeneza timu kubwa. Malengo yetu ni makubwa ilitulazimu usajili wetu uwe wa viwango vya mbali, ndiyo maana unaona tulisajili timu itakayocheza kwa nguvu mashindano ya Afrika.

“Unajua kama utakuwa na timu kubwa ya kushindana kibabe katika mashindano ya Afrika maana yake hata hapa ndani una nafasi kubwa ya kufanya makubwa.”

Aidha Gumbo alisema uongozi wa klabu hiyo baada ya kuiboresha kambi yao ya Avic Town, pia kutakuwa na maboresho makubwa ya masilahi kwenye kuongeza ushindani ndani ya kikosi chao na hata kwenye mashindano kijumla.

“Tuliwaleta wataalam wameiboresha kambi yetu na sasa imekuwa ya kisasa, pale ndipo ambapo panatupa jeuri ya kujiandaa tunapotaka kwenda kukutana na timu yoyote,” alisema Gumbo na kuongeza;

“Ukiacha hilo idara yetu ya mashindano, tumepitia yale tuliyoyafanikisha msimu uliopita, kutakuwa na maboresho makubwa ili kuhakikisha wachezaji wetu wanajituma kuitafutia ushindi klabu yetu.

Hata hivyo, Gumbo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji aliwaonya mashabiki na wanachama wao kuhakikisna wanasahau mafanikio yao ya msimu uliopita na kuanza hesabu mpya kupigania timu yao.

“Kila mmoja anafahamu Yanga ndio klabu iliyochukua mataji mengi msimu uliopita, mashabiki wetu tunatarajia wameiweka kando furaha hiyo, baada ya hapo wavae ujasiri na kuanza kujipanga kuipigania timu yao katika mchezo wowote, hatutakiwi kuidharau timu yoyote kwa kuwa kila timu inajipanga kupambana na sisi.”

Yanga itauanza msimu nyumbani Septemba 24, 2025 kwa kuvaana na Pamba Jiji kabla ya kuifuata ugenini Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu msimu huu kwenye Uwanja wa Sokoine, siku ya Septemba 30, siku chache baada ya kumalizana na Wiliete Banguela ya Angola katika mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mechi ya awali baina yao itapigwa Septemba 19-21.