Dar es Salaam. Kutambua mfumo mzima wa hisia wa mtoto akiwa amekwazika, amekasirika, ana furaha anacheza na nani au anaishi vipi, ni miongoni mwa vipengele vya maana katika kulea mtoto.
Lakini kutunza mtoto ni kutimiza haki za msingi za mtoto kama kumpa malazi mazuri, elimu bora, mavazi na vyakula bila ya kufuatilia kile anachokifanya ikiwemo mienendo yake.
Kulingana na tafsiri hizo ni wazi katika jamii wapo baadhi ya wazazi na walezi wasiowalea watoto wao. Na hilo linawezekana kwa sababu ya muda, majukumu, usasa au kutojali wajibu.
Akizungumza kwenye kipindi cha Power Breakfast cha kituo cha habari cha Clouds FM hivi karibuni, Ofisa wa Polisi, Eliezer Hokororo kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Dawati la Jinsia na watoto, alisema inawezekana mzazi ukakosa muda na ukashindwa kujua mfumo mzima wa hisia na tabia za mtoto katika kukua kwake kwakuwa kila utakaporudi unakuta amelala.
“Lazima tuwe na utaratibu wa kufuatilia ukuaji wa mtoto, ameona nini, anacheza na nani au ana tabia gani. Katika utaratibu wa sasa hivi, mtoto anaweza akafika nyumbani jioni kutoka shuleni akalala na mzazi akarudi akiwa amechelewa, lakini bado kuna wajibu wa kutenga muda wa kuhusiana na mtoto ili kutambua makuzi yake,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa saikolojia, Dk Neema Mwankina anafafanua juu ya kutunza mtoto akisema ni kuhakikisha anapata mahitaji yote ya msingi ambayo anapaswa kuyapata ikiwemo chakula, mavazi, malazi ma shule, kumlinda na kumpa matibabu sahihi ya kiafya.
“Mzazi ambaye anamtunza mtoto kuna uwezekano mtoto huyo atakuwa hana maadili yanayostaili huko mbele kwa sababu ametunzwa kwa kupewa kila kitu bila ya kulelewa. Hakuweza kuambiwa kitu gani asifanye kwenye maisha yake,” anasema.
Akielezea kuhusu kulea, anasema ni mchakato wa kukuza na kumtunza mtoto kimwili, kiimani, kiakili, kihisia na kimaadili ili akue akiwa mtu mzima mwenye maadili na uwezo wa kijitegemea.
Anasema lazima uangalie kwanza mtoto ana kasoro au dosari gani ya mwili katika ukuaji wake. Kiakili lazima mtoto aangaliwe je, ana uwezo wa kuelewa haraka au taratibu au yuko katikati ili ujue anaendaje katika ile njia anayopaswa.
“Kihisia lazima mzazi uangalie na kumfundisha kihisia mtoto akiona wazazi wake au ndugu zake anafurahia? Kimaadili mzazi lazima umkanye mtoto umweleze hili baya uwezi kuongea kwenye kinywa chako au tabia hii si nzuri hupaswi kuwa nayo katika maisha yako.
“Fimbo sio dhambi kwa maana inamfundisha na kumuonya mtoto kwa upendo katika kumtoa hatua moja kwenda nyingine,’’ anasema.
Anasema endapo mtoto akitunzwa bila ya kulelewa, matokeo yake anajiingiza kwenye tabia mbaya kama ulawiti uvutaji wa bangi ama dawa za kulevya na tabia nyingine zisizofaa.
Mtoto anatakiwa akue akitengenezewa mazingira ya kuja kuwa kijana bora anayejitambua, ili hatimaye aje kuwa mama na baba bora wa familia yake baadaye.
Anasema wazazi wanatakuwa kuwalea watoto katika njia ipasayo kwakuwa dunia haitawwacha hata watakapokuwa watu wazima. Wawafundishe tabia kwamba kutukana, wizi, kutaazama sinema za utupu, kulewa zote ni dhambi ili waelewe mapema.
“Mtoto ameenda kuzurura tangu asubuhi na hadi inafika jioni hujui yuko wapi hapo unakuwa unamtunza na humlei. Mtoto anapaswa kuelimishwa na kuonywa pale anapokosea ili ajue thamani yake inaanzia utotoni,” anasema na kuongeza:
“Ukimtunza mtoto kwanza hata wewe mwenyewe anaweza asikuthamini wala kujali. Mtoto akilelewa kwa njia zinazofaa atakuwa na hekima na kujali.’’
Kwa upande wa saikolojia, Dk Mwankina anasema kulea ni kumfundisha mtoto stadi za maisha kama kuosha vyombo, kudeki, kufua, kuchota maji, kupika na kazi nyinginezo za kivitendo.
Anasema mwezeshe mtoto ajue jinsi ya kushughulikia hasira zake, ajue madhara ya kutodhibiti hasira, ugomvi na chuki afundishwe kujitambua.
Anatoa wito kwa wazazi na walezi kuwalea watoto wao na si kuwatunza, kwakuwa kuwatunza watoto mara nyingi kunaleta matokeo yasiyotarajiwa.
Mwanasaikolojia kutoka nchini Marekani Dk Aliza Pressman ambaye pia ni mhadhiri katika Hospitali ya Mount Sinai, anasema ametafiti kwa miaka 20 juu ya jinsi ya kulea watoto ili wawe na mafanikio na ujuzi.
Katika andiko lake hilo lililochapishwa na shirika la CNBC mwaka 2024, mwanasaikolojia huyo anasema kwanza uwezo wa mtoto wa ndani ikiwemo kujiamini kujikubali na kujipenda, unaanzia na changamoto za umri wake anazopitia au kupitishwa.
Anasema kutokana na changamoto ya ugumu anaopitia, mtoto huyo anahitaji kuambiwa na mzazi au mlezi wake kwamba ataweza hivyo asikate tamaa na kupewa motisha.
Akieleza namna ya kuwajenga watoto anasema wanapaswa kutiwa moyo kwa kujaribu jambo wasilo na uwezo nalo, ikiwemo kuwambia kauli kama vile jitihada huleta maendeleo.
Mzazi, Elizabeth Yohana kutoka Dar es Salaam anasema mtindo wa maisha ya sasa akihusisha ubize wa majukumu kati ya mama na baba, unachangia kwa kiasi kikubwa watoto kutelekezwa kwenye malezi.
“Mimi nikiwa kama baba huwa najitahidi kuwahi kurudi nionane na mwanangu nimuulize amefanya nini siku nzima alienda wapi na kucheza na nani,” anasema mzazi mwingine, Ramadhan Hussein