TUONGEE KIUME: Mwanamume anatetea na kubadili maisha ya watu

Wiki kadhaa zilizopita nilikuwa barabarani naendesha gari. Mara nikafika sehemu yenye barabara nyembamba.

Mbele yangu upande wa kulia kuna gari inakuja, na upande wa kushoto kuna mkokoteni unakwenda ninapoelekea. Ikabidi nisimame kusubiri mwenye mkokoteni asogee mbele ili niweze kupita vizuri kwa usalama.

Lakini ghafla nikasikia, pipiiiiii!!! Honi kibao. Kuangalia nyuma naona ni bodaboda mwenye haraka kama ‘ambyulensi’.

Niwe mkweli, honi zake zilinikwaza sana, nikashusha kioo nikamtemea maneno machafu. Bodaboda naye hakukubali, akanirudishia maneno makali.

Hasira zikanipanda mara mia moja hamsini, nikaongeza spidi na kumfikia kisha nikatishia kama nataka kumgonga. Akayumba, almanusura atumbukie mtaroni na abiria wake.

Lakini bado alikuwa na jeuri, unajua alinambia nini; “Watu hawagongwi hivyo, huo mkwara tu.” Sikumzingatia tena, nikaongeza spidi nikaondoka zangu.

Huwezi kuamini, njia nzima nilikuwa bado nimekasirika. Nilikuwa namuwaza yule bodaboda. Na nadhani kilichonitesa zaidi ilikuwa ni yale maneno yake ya mwisho, ya kwamba sikuwa na uwezo wa kumgonga, nilikuwa nimejaa mkwara.

Iliniuma sana. Niliona ni kama mtu kaniambia kama wewe mwanaume kweli basi nigonge.

Siku yangu iliharibika kisa maneno ya bodaboda na kwa kiasi fulani ilinifanya nijione mjinga. Nikaamua kutafuta dawa.

Nikaingia zangu mtandaoni na mwishowe nikakutana na video ya mtu anayefundisha kwamba, kama unataka kuwa na maisha ya amani, mbinu ni moja tu; ni kuacha kuchukulia vitu kwa ubinafsi, kwa ‘kizungu’ wanasema: ‘Don’t take things personal’.

Mwalimu wa kwenye video hiyo alikuwa anafundisha kwamba, asilimia kubwa ya matatizo tunayopitia sio kwa sababu ya matatizo yenyewe, bali ni kwa sababu ya namna tunavyoyapokea.

Alikuwa anasema, kama kila unachofanyiwa utachukulia kama vile kina lengo la kukushambulia wewe basi jua utaishi maisha magumu sana.

Watu wakicheka utaona wanakucheka wewe. Na hata kama ni kweli wanakucheka wewe, utaona wewe ndiyo tatizo na sio wao.

Mwalimu kwenye video hiyo akafundisha kwamba, kama unataka kuishi kwa amani, jifunze kutochukulia vitu kwa ubinafsi na njia mojawapo ya kufanikisha hilo ni kuwatetea watu.

Kwa mfano, kama unaendesha, halafu bodaboda anakupigia honi nyingi za kukera, usiwaze kwamba bodaboda anakuona hujui kuendesha gari au huna akili, bali mtetee kwamba, huenda anapiga honi nyingi za kukera, kwa sababu labda anamwahisha mteja aliyechelewa uwanja wa ndege, au katumwa dawa za dharura akichelewa tu, mgonjwa anapoteza maisha.

Wakati namsikiliza mwalimu kwenye video hiyo niliona kama anatania, lakini nikasema ngoja nitajaribu njia hiyo… huwezi kuamini, matokeo yake nimekuwa mtu mwenye amani sana.

Bodaboda akinipigia honi za kukera, nakasirika, kwa sababu kukasirika ni hisia muhimu na muda mwingine inakuja bila kupanga, lakini sekunde hiyo hiyo namtetea, nasema anafanya hivi kwa sababu fulani zinamuhusu yeye mwenyewe, sio mimi.

Nikiwa ofisini, mtu akaniongelesha vibaya, nakasirika, lakini badala ya kuona kama haniheshimu, namtetea kwamba huenda ana msongo wa mawazo unaomsumbua, au huenda hajapumzika vizuri wiki hii, kisha tunaendelea na maongezi kama kawaida.

Ni njia ngumu hasa kwetu wanaume tunaopenda kujimwambafai, lakini ni njia ambayo ukiweza kuifanyia kazi utaona mabadiliko yake nje- nje.