Waganda waja kivingine mbio za magari Afrika

UJUMBE mzito wa madereva na mashabiki wa mbio za magari kutoka Uganda unatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kwa ajili ya kusherehesha mashindano ya magari ubingwa wa Afrika yatakayochezwa nchini  Septemba 19, 20 na 21 mkoani Morogoro.

Waganda wanakuja Morogoro wakiwa na mabingwa watarajiwa, Mtanzania Yassin Nasser ambaye ni dereva na Mganda Ally Katumba, ambaye ni msoma ramani, wakati washabiki, licha ya kuwa mashuhuda wa namna ambavyo Nasser na Katumba watautwaa ubingwa wa bara la Afrika endapo watamaliza katika nafasi ya pili na kupata  pointi 28 na kumshinda mpinzani wake wa karibu, Samman Vohra kutoka Kenya, pia wanakuja kutalii na kufurahia mazingira mazuri ya Tanzania

Msafara huu unakuja na bango la Safiri na Bombadier Yetu kwenda Mbio za Magari Tanzania (Travel with our Bombadier to Rally Tanzania).

Mwezi Septemba ambao kwa nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni msimu wa sherehe na mavuno, mara hii utaboreshwa mbio hizo.

Wakiongea kutoka Kampala, washabiki kutoka Uganda wameuambia mtandao maalum wa wadau wa mbio za magari, Rally TZ, kwamba watatokea Kampala na kuingia Tanzania kwa basi kupitia Masaka na Mtukula Septemba 15 na watapumzika siku moja mjini Tabora.

Baada ya Tabora, tarehe Septemba 17, watasafiri kwa basi hadi Dodoma ambako watakwea treni ya Mwendokasi (SGR) hadi Dar es Salaam na siku inayofuata watarudi na treni hiyo kwa ajili ya kushuhudia ufunguzi na mbio za mchujo(shakedown) siku ya Ijumaa, tarehe 19 Septemba.

“Mbio za magari ni utalii mzuri sana kwani unapata vyote, burudani ya magari yakishindana na mazingira mazuri ya nchi na kujenga urafiki na watu mbalimbali,” alisema mmoja wa wanaotarajia kuja, Sebagala Ronald.

Hata kama atashinda raundi ya ARC (Africa Rally Championship) ya Morogoro, Vohra ataongeza pointi 30 ambazo hazitampa ubingwa wa Afrika endapo Nassar atamaliza katika nafasi ya pili na kutwaa pointi 28.

Mkoa wa Morogoro ndio mwenyeji wa raundi ya tano na ya mwisho ya ubingwa wa mbio za magari kwa Afrika baada ya raundi nne kufanyika nchini Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Hadi mwisho wa raundi ya nne nchini Burundi, Mtanzania Yassin Nasser walikuwa wakiongoza kwa pointi 8 mbele ya Mkenya Vohra.

Mtanzania mwingine, Prince Charles Nyerere, ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu nchini Burundi, ana uhakika wa kutwaa taji la ARC 2, na hatakuwa na mpinzani kuelekea kwenye raundi ya hitimisho.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Mbio za Magari nchini, Satinder Birdi amezishukuru kampuni za Mkewawa kwa kudhamini raaundi ya tano ya ubingwa wa Afrika kwa mwaka huu.