Vyama vitatu tayari kwa kampeni, kimoja chaahirisha uzinduzi kitaifa

Dar es Salaam. Vyama vitatu, kikiwamo cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Wananchi (CUF) na Chama cha Wakulima (AAFP), leo vinazindua rasmi kampeni zao za uchaguzi mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, huku chama kimoja kikiahirisha.

Chama ambacho kilipaswa kuzindua kampeni zake leo Agosti 31, 2025, kulingana na ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), cha NRA, kimesogeza mbele uzinduzi wake, huku kikisema kitafanya hivyo kati ya Septemba 6 na 7, mkoani Kigoma.

Kwa vyama vinavyozindua kampeni, uzinduzi huo unafanyika katika mikoa mitatu tofauti. Chaumma kitakuwa viwanja vya Biafra, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, AAFP wako mkoani Morogoro katika Kata ya Kisaki, na CUF kinazindulia kampeni zake viwanja vya Furahisha, jijini Mwanza.

Wakizungumza na Mwananchi leo kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama hivyo wamesema mbali ya kuwatambulisha wagombea wa kiti cha urais, watawatambulisha wagombea ubunge na udiwani.

Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chaumma, John Mrema, amesema shughuli ya uzinduzi itaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Hashimu Rungwe, katika viwanja vya Biafra.

“Ni tukio muhimu na tunawasihi wananchi wajitokeze kusikiliza kwa makini sera zetu na tutafanya nini ikiwa watatupa kura za kutosha kutuweka madarakani kwa miaka mitano ijayo,” amesema Mrema.

Mrema amesema katika uzinduzi huo, Chaumma kitamtambulisha rasmi kwa wananchi mgombea wake wa kiti cha urais, Salum Mwalimu, sambamba na mgombea mwenza Devotha Minja.

“Lakini pia tutawatambulisha wagombea ubunge na udiwani wa majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Chama cha AAFP, Rashid Rai, amesema chama kitamtambulisha rasmi Kunje Ngombale-Mwiru kuwa ndiye mgombea wao wa kiti cha urais.

Rai amesema kama ilivyo ada ya uzinduzi wa kampeni, watawanadi pia wagombea wao wa nafasi za ubunge na udiwani.

Chama cha CUF kimemteua Samandito Gombo ambaye pia amepitishwa na INEC kupeperusha bendera ya urais, akishirikiana na mgombea mwenza wake, Husna Abdallah Mohamed.

Mbali na urais, vyama hivyo pia vitawanadi wagombea wao wa nafasi za ubunge na udiwani, huku vikitarajia kutumia kampeni hizi kama jukwaa kuu la kuwasilisha ilani zao kwa wananchi, kuelezea sera, mikakati ya maendeleo na vipaumbele vyao kwa miaka mitano ijayo endapo watapewa ridhaa ya kuongoza.

Uzinduzi huoo wa kampeni unafanyika katika kipindi ambacho maandalizi ya uchaguzi yameingia katika hatua muhimu, huku INEC ikiendelea kusimamia mchakato wa kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa amani.

Tayari chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeshazindua kampeni zake Agosti 28, 2025, katika viwanja vya Tanganyika Packers, jijini Dar es Salaam, huku vyama vingine vya siasa vikitarajiwa kuzindua kampeni zao kuanzia wiki ijayo.

Ushindani unatarajiwa katika uchaguzi wa mwaka huu, huku vyama vya upinzani vikionesha dhamira ya kuleta ushindani wa kweli kwa chama tawala kwa kuwasilisha sera mbadala na mikakati bunifu ya maendeleo kwa Taifa.

Akizungumzia hatua hiyo, Katibu Mkuu wa Chama cha AAFP, Rashid Rai, amesema kampeni zao wanazizindua leo mkoani Morogoro, katika Kata ya Kisaki, kwa kuwa ni miongoni mwa maeneo yao ya kimkakati.

“Tutakuwa hapa Morogoro kwa siku saba. Hapa ndipo chama chetu kiliasisiwa. Tutakuwa Kilombero, Mvomero na Mlimba na maeneo mengine ya mkoa huu kwa siku saba,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa NRA, Hassan Almas, amesema uzinduzi wa kampeni kitaifa bado, bali leo chama hicho kitafanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Dar es Salaam.

“Hatutazindua rasmi, lakini leo tunafanya mikutano ya kampeni kwenye majimbo yote ya Wilaya ya Temeke, Buza, Chamazi, Mbagala Rangi Tatu, Majimatitu, na tutaelekea mkoani Kigoma kuzindua kampeni yetu Septemba 6 na 7,” amesema.