Dar es Salaam. Huduma ya mabasi yaendayo haraka (mwendokasi) katika barabara ya Mbagala, ambayo awali ilitarajiwa kuanza leo Jumatatu Septemba mosi, 2025, imesogezwa mbele kutokana na kutokamilika kwa miundombinu muhimu yakiwamo mageti janja na kituo cha kujazia gesi.
Akizungumza leo Jumatatu, Septemba mosi 2025 na Mwananchi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Athuman Kihamia, amesema kuchelewa kuanza kwa huduma hiyo kunatokana na changamoto hizo, licha ya mabasi kuwa tayari yamewasili.
“Mabasi yamewasili, lakini hatutaweza kuanza kutoa huduma leo kama tulivyoahidi kwa kuwa baadhi ya miundombinu haijakamilika. Mageti janja kwa ajili ya ukataji wa tiketi bado hayajafungwa na kituo cha kujazia gesi kilichopo kwenye karakana ya Mbagala nacho hakijakamilika.
“Hata hivyo, taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya ujenzi huo tutaitoa baada ya wiki moja,” amesema Dk Kihamia.
Mabasi hayo 151 yaliwasili katika karakana ya Mbagala Rangi Tatu usiku wa Agosti 29, 2025, baada ya kutoka bandarani, shughuli iliyochukua takribani siku mbili.
Kampuni ya wazawa ya Mofat ndiyo iliyopewa jukumu la kuendesha awamu ya kwanza ya mradi huo na imekabidhiwa kuleta mabasi 255 kati ya 755 yanayohitajika kwa mradi mzima.
Awali, wiki iliyopita, Dk Kihamia aliliambia gazeti The Citizen kwamba huduma ingeanza rasmi Septemba mosi, 2025.
Pia, Agosti 13, 2025, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokagua miundombinu hiyo aliagiza sehemu zilizobaki zikamilishwe ili huduma ianze ndani ya mwezi huo.
Hata hivyo, wakati Majaliwa akiagiza hayo, moja ya changamoto iliyokuwa imebakia ni ujenzi wa kipande cha barabara katika eneo la Kamata, ambacho bado hakijakamilika.
Mbali na changamoto za barabara, vituo vya mwendokasi navyo havikuwa na mageti janja kwa ajili ya mfumo wa kulipia kwa kadi.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mofat, Muhammad Abdallah Kassim, akizungumza na Mwananchi wakati wakipokea mabasi hayo, alisema hawatapokea fedha taslimu kwa malipo ya nauli na badala yake abiria wanapaswa kutumia kadi za Dart au za benki ambazo tayari zitafanya kazi na mfumo huo.
“Sisi hatupokei fedha taslimu. Abiria ataweka fedha kwenye kadi na kisha atatumia kusafiri. Mageti tayari yamewasili na kazi ya kuyafunga katika vituo mbalimbali inaendelea,” alisema Kassim.
Hata hivyo, ucheleweshaji huo umewavunja moyo baadhi ya wakazi wa Mbagala, akiwamo Deogratius Kisinde, aliyesema, “Tumemsikia mara kadhaa Mkurugenzi wa Dart akiahidi huduma ingeanza leo, lakini hakuna kinachoendelea. Mabasi tumeona yakiingizwa kwenye karakana tangu juzi. Ni vema mamlaka ziwe zinatoa ahadi za kitaalamu na si za kisiasa.”
Mabasi hayo yenye urefu wa mita 18, yatakayobeba abiria 160 kila moja, yanatarajiwa kusafirisha kati ya abiria 325,000 hadi 400,000 kwa siku mara huduma itakapoanza.
Safari zitakuwa zikifanyika kutoka Mbagala hadi Gerezani, Kivukoni na Morocco, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.