Kahama. Mwanamume ambaye hajafahamika jina wala makazi yake amekutwa amefariki dunia kwenye bwawa la maji lililopo Kata ya Nyihogo, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, Stanley Luhwago akizungumza leo Septemba mosi, 2025, amesema tukio hilo limetokea Agosti 31, 2025.
Amesema walipokea taarifa kutoka kwa wananchi waliouona mwili huo ukielea juu ya maji.
Amesema kwa kushirikiana na wananchi walifika eneo la tukio na kufanikiwa kuupoa mwili huo kisha kuukabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Luhwago amewataka wananchi kutoingia katika maeneo hatarishi bila tahadhari, sambamba na kuwalinda watoto wasiogelee kwenye bwawa hilo kutokana na kuwa na tope jingi pamoja na magugu maji hatari.
“Kumekuwa na tabia za watu kuogelea au kufanya shughuli za uvuvi katika bwawa hili hatarishi ambalo limejaa magugu mengi, na matope, hali ambayo imekuwa ikisababisha madhara kama vile vifo.”
Luhwago amesema changamoto iliyosababisha shughuli ya maokozi kufanyika kwa muda mrefu ni kutokana na eneo la bwawa ulipokuwa mwili huo kuzungukwa na magugu mengi hali iliyowakwamisha kuufikia mwili kwa wakati.
Mkazi wa Mhungula Edward James, ameiomba Serikali kuweka uzio ili kudhibiti uingiaji holela wa watu kwenye bwawa hilo, ambao mara nyingi wamekuwa wakipoteza maisha baada ya kuanza shughuli za kuongelea au kuvua samaki.
“Bwawa hili ni hatarishi, kila anayeingia hapa mara nyingi hatoki salama, kwa mwaka huu hili ni tukio la tatu, miili ya watu kubainika ikiwa inaelea jambo ambalo linatupa wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa matukio haya,”amesema James.
Brayton Steward, mkazi wa Mtaa wa Nyihogo ameiomba Serikali kulifukia bwawa hilo kama halitumiki na kutunzwa ipasavyo.
Amesema upo uwezekano wa watu kuuawa katika maeneo mengine na kutupwa bwawani humo.
“Hiki kilikuwa chanzo cha maji kwa wakazi wa Kahama zamani ila kwa sasa limekuwa hatarishi kutokana na kuzungukwa na msitu mkubwa, kama lisipofukiwa au kuwekewa uzio, watu watakuwa wakipoteza maisha kwa kile kinachodaiwa ni kuogelea katika bwawa hili,” amesema Steward.