YANGA inaendelea kujifua kwenye kambi yao iliyopo Avic Town, Kigamboni chini ya kocha Romain Folz, lakini kuna winga mmoja mpya aliyetua klabuni hapo hivi karibuni amejishtukia baada ya kukiangalia kikosi hicho na fasta akaamua kujiongeza mwenyewe ili mambo yawe mepesi.
Nyota huyo ni kiungo mshambuliaji aliyetua Jangwani kutoka Tabora United, Offen Chikola amesema kwa namna ushindani ulivyo mkali katika nafasi anayocheza, analazimika kufanya mazoezi binafsi kwa bidii kuhakikisha anakuwa fiti, ili atakapopewa nafasi aonyeshe kiwango.
Chikola aliyemaliza msimu uliopita na mabao saba na asisti mbili, ameliambia Mwanaspoti, baada ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya chama lake la zamani, Tabora United iliyopigwa Ijumaa iliyopita, walipewa mapumziko ya siku mbili wikiendi yaani Jumamosi na Jumapili.
Nyota huyo anasema naye alizoziona siku hizo mbili ni fursa kwake ya kwenda kupiga tizi binafsi na mtaalum mazoezi ya viungo, Godfrey Mkinga ‘Denzel Trainer’ ili kuzidi kujiweka fiti.
“Nilikuwa nimemwambia mapema kuhitaji huduma yake, akawa amezitazama video za mechi nilizocheza nikiwa Tabora, baada ya kukutana naye aliniambia nina nguvu, ila natakiwa niongeze kasi, pumzi na wepesi vitakavyonisaidia kufunga zaidi,” alisema Chikola na kuongeza;
“Zoezi lililofuata nikapima kilo zilikuwa 69 akasema natakiwa kucheza humo zikizidi iwe 70, hivyo lazima nipambane kutunza ufiti, baada ya mechi na Tabora kocha aliniambia kitu cha kukifanyia kazi na alisema kila mtu akijituma kwa bidii atapata nafasi ya kucheza.”
Mbali na kumtafuta treina binafsi, Chikola alisema alimwambia mkufunzi wa timu ili kumjenga na mazoezi ya utimamu mkubwa na alimwambia atalifanyia kazi jambo hilo, hivyo anaamini hilo likifanikiwa hawezi kukosa kucheza mashindano mbalimbali yaliyopo mbele yao.
“Natakiwa ninapopewa nafasi ya kucheza kocha ashawishike zaidi kunipanga, yote hayo hayaji kwa bahati mbaya isipokuwa kwa bidii ya mazoezi na kuzingatia maelekezo ninayokuwa napewa na kocha na kujifunza kwa wengine,” alisema Chikola.
Katika nafasi anayocheza Chikola anashindana namba na Maxi Nzengeli aliyemaliza msimu uliopita na mabao sita na asisti 10, Clement Mzize aliyefunga mabao 14 naasisti nne na Farid Mussa, huku pia akisajiliwa Edmund John aliyetoka Singida Black Stars.