Straika Singida BS kubaki Pamba Jiji

BAADA ya mshambuliaji wa Singida Black Stars, Abdoulaye Yonta Camara, raia wa Guinea kukitumikia kikosi cha Pamba Jiji kwa mkopo wa miezi sita kwa msimu wa 2024-2025, mabosi wa timu hiyo wanafanya mazungumzo ya kuendelea kubaki naye.

Camara alijiunga na Singida Agosti 14, 2024, ingawa sababu za kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara ziliwafanya mabosi wa kikosi hicho kumtoa kwa mkopo dirisha dogo la Januari 2025 na kuonyesha kiwango bora kilichowavutia viongozi wa Pamba Jiji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha alisema hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa juu ya suala hilo, ingawa uamuzi wa mwisho umebaki kwa benchi la ufundi endapo litahitaji kuendelea na mchezaji huyo.

“Ni mchezaji mzuri ambaye ametusaidia sana kwa msimu uliopita, tunasubiria uamuzi wa mwisho wa benchi la ufundi kuona ni kama atampendekeza tuendelea naye pia msimu ujao, mazungumzo yaliyopo ni ya mkopo tu na sio kumnunua,” alisema Ezekiel.

Nyota huyo alitua nchini kwa mara ya kwanza akitokea Milo, huku akikumbukwa zaidi katika msimu wa 2023-2024 alipoibuka pia mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21. Aliwahi kuzichezea AS Ashanti Golden Boys na Wakriya AC zote za kwao Guinea.

Kwa msimu wa 2024-2025, Camara alifunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara akiwa na timu ya Pamba Jiji, nyuma ya mshambuliaji mwenzake, Mkenya Mathew Momanyi Tegisi aliyefunga mabao saba, hivyo kutengeneza pamoja pacha kali eneo la ushambuliaji.