Bado Watatu – 16 | Mwanaspoti

“Sijambo. Karibu” Msichana akanijibu huku akinitazama kwa macho ya udadisi.

“Sijui kama unanikumbuka?”

“Nakukumbuka, ulikuja juzi kumuulizia mtu fulani , nikakwambia hatumfahamu”

“Sasa nimekuja tena kwa tatizo hilo hilo. Nakumbuka uliniambia kwamba nyinyi ni wapangaji, sasa nilikuwa namhitaji mwenye nyumba hii”

“Nakumbuka nilikwambia mwenye nyumba haishi hapa, anaishi Iringa”

“Nipatie hata namba yake”

“Anayo mume wangu na hayupo hivi sasa?”

“Amekwenda Pangani lakini atarudi,”

“Nije muda gani ili nipate hiyo namba”

“Jioni kuanzia saa kumi na moja atakuwepo”

“Sawa. Nitakuja ,muda huo. Kwaheri”

Msichana alisubiri hadi ninaondoka akafunga geti. Nilijipakia kwenye gari na kuondoka. Nilikwenda tena katika gereza la Mawani. Akili yangu ilikuwa ikiniambia tatizo linaweza kuwa upande wa gerezani hapo. Kwa nini waliothibitishwa kuwa wamenyongwa wawepo tena uraini?

Nilipofika nikakutana tena na mkuu wa gereza hilo.

“Samahani mkuu kwa usumbufu lakini ndiyo kazi zetu zilivyo, uliniambia kwamba wale jamaa niliokuulizia walishanyongwa?”

“Ndiyo wale walishanyongwa. Si tulitazama kumbukumbu zao?’ Mkuu wa gereza hilo akaniambia.

“Ndiyo. Lakini upande wa magereza mnasema wameshanyongwa lakini watu hao wapo uraiani na maiti zao ziko mochwari, unadhani tatizo liko wapi?”

“Nyinyi sasa ndio mchunguze kujua tatizo liko wapi. Sisi tunasema hao watu wameshanyongwa. Sasa sijui nyinyi mnasemaje?”

“Kama makaburi yao yatafukuliwa na tukakuta miili yao na wakati huo huo miili hiyo ipo mochwari, unadhani hao watu watakuwa ni wa aina gani?”

Mkuu wa gereza kabla ya kunijibu alicheka kidogo.

“Mimi siamini kwamba hao watu walikuwa hai na walikuwa uraiani”

“Nakumbuka uliwahi kuniambia kwamba alama za vidole hazifanani na mimi ninakubaliana na hilo, hakuna binadamu ambao alama za vidole vyao zinafanana hata wakiwa mapacha. Sasa ni kwanini alama za vidole wa watu hao walionyongwa huku jela zifanane na za wale watu walionyongwa uraiani?”

“Hilo jambo linahitaji uchunguzi.”

“Nakubaliana na wewe. Nimekuja kukufahamisha kwamba kesho tutaomba kibali cha mahakama ili makaburi ya watu hao yafukuliwe.”

“Ni jambo zuri kama mtafanya hivyo.”

“Hatua hiyo itatusaidia kujua wale walionyongwa kwa hukumu ya mahakama ni kina nani na wale walionyongwa uraiani ni kina nani. Tutazilinganisha tena alama zao za vidole. Kama hatuamini kuwa alama za vidole zinafanafana, sidhani kama alama zao zitafanana!”

“Sikiliza Inspekta Fadhil, hatua ya kuyafukua makaburi yao itatusaidia sana. Tutakuwa tumepanua wigo wa huu uchunguzi na kama wasemavyo watu wa vijiweni kitaeleweka.”

Nikampa mkono mkuu huyo wa gereza.

“Asante mkuu. Kama tutakipata kibali hicho kesho, tutakuja kuyafukua makaburi yao.”

Baada ya kuagana na mkuu huyo wa gereza nilitoka ofisini mwake nikaenda kupanda gari na kuondoka.

Niliporudi ofisini kwangu nikapata ripoti ya uchunguzi wa alama za vidole za mtu aliyenyongwa siku ile. Alikuwa ni Datsan Unyeke ambaye pia alihukumiwa kunyongwa pamoja na wenzake wengine kwa kosa la kumuua Thomas Christopher’

Ilikuwa ni kama vichekesho au mchezo wa kuigiza. Mtu ambaye tunamtuhumu kufanya mauaji haya ndiye yeye aliyefanyiwa mauaji. Yaani muda ule tunapomtafuta ni kama hakuwepo duniani! Tunamtafuta mtu hewa!

Huyu Dastan alikuwa na faili lake peke yake. Na sababu ya kuwepo kwa mafaili tofauti lakini yote yakihusika na kesi moja ya mauaji ya mtu huyo huyo na kwa kosa hilo hilo, ni kwamba hao watuhumiwa hawakukamatwa na kushitakiwa pamoja.

Niligundua kwamba watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati fofauti na hivyo kushitakiwa kwa nyakati tofauti lakini kwa kosa hilo hilo na wote wakapatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia na kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Hiyo ndiyo sababu Dastan ambaye alikamatwa mwisho akawa na faili la peke yake kwani wakati anakamatwa wenzake walikuwa wakisubiri hukumu.

Mafaili ya kesi yao yalionesha kwamba watu hao walikuwa ndugu na walishirikiana kumuua Thomas Christopher na walipogundua kuwa wamejulikana na kuanza kutafutwa wakakimbia.

Katika msako huo wa polisi uliochukua miezi kadhaa watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati fofauti hali iliyosababisha iwe vigumu kushitakiwa wote kwa pamoja.

Lakini ilionekana wazi walikuwa wamebadili majina. Kila aliyebainika alikuwa na jina tofauti na lile ambalo alilitaja wakati anakamatwa na kushitakiwa.

Hilo nalo lilinipa swali. Nikajiuliza ni kwa nini wamebadili, majina. Majibu ya haraka haraka niliyoyapata ni kuwa walibadili majina ili wasionekane kuwa ni ndugu na pili walibadili majina ili wasitambulike wao ndio waliohukumiwa kunyongwa.

Lakini nikajiambia kama miili yao itakutwa makaburini walimozikwa, hawa watu walionyongwa kipindi hiki ambao tunawahisi ni wao, watakuwa ni kina nani na kwanini alama za vidole vyao zinafanana?

Ile dhana ya mizuka ambayo nilikuwa siiamini, sasa ilikuwa ikinijia akilini mwangu. Niliona kama miili yao itakuwemo makaburini, hawa walionyongwa kipindi hiki walikuwa mizuka yao ambayo iliibuka baada ya wao kunyongwa.

Bado, nilijiambia, kuna yule mtu anayetuhumiwa kwa mauaji ambaye naye uchunguzi umeonesha kuwa aliuawa kwa kunyongwa na watu hao ambao nao walikamatwa na kuhukumiwa.

Sasa, nikajiuliza, vipi mtu ambaye aliuawa na kuthibitika kuwa alikufa kuwa hai na kuwaua kwa kuwanyonga watu waliomuua?

Kama tutaamini wauaji hao ni mizuka, je yeye aliyewanyonga ambaye tayari alishakufa atakuwa nani? Si atakuwa mzuka pia?

Nikajimbia kila kitu kinaonesha uchunguzi huu unahusika na mizuka na si binaadamu kamili.

Na kama kweli ni mizuka, niliendelea kujiambia, nitasumbuka sana.

“Acha nimpigie bosi wangu nimweleze,” nikajiambia kimoyomoyo kisha nikainua mkono wa simu ya mezani na kumpigia afisa upelelezi.

Afisa huyo alipopokea simu yangu nilimsalimia.

“Afande habari ya muda huu?”

“Nzuri, je una habari gani?”

“Habari ni ile ile inayohusu hawa watu walionyongwa, yaani jinsi upelelezi unavyokwenda ninafikia kuamini tunashughulika na mizuka.”

“Hawa watu wote walionyongwa ambao uchunguzi umeonesha kuwa ni ndugu moja, inaonekana walishanyongwa na kama wamenyongwa hawapo tena duniani. Sasa kama hawapo tena duniani, hawa walionyongwa sasa ni kina nani, kama si mizuka? Isitoshe afande hata huyo muuaji ndiye aliyeuawa na watu hao. Na yeye kama anaishi atakuwa ni mzuka!”

“Sikiliza Fadhil ukiingiza hisia zako katika Imani utakwenda kinyume. Wewe ulisikia mzuka unakufa? Mzuka haufi. Mzuka ukifa maana yake ni kwamba binaadamu amekufa mara mbili na hakuna kitu kama hicho. Hao watu unaotaka kuamini kuwa ni mizuka wako mochwari! Kumbuka mochwari hakukai mizuka!”

“Unajua ninatatizika kwa kuona watu wote ninaowachunguza wameshakufa lakini hilo tuliache. Muhimu ninalotaka kukueleza ni kwamba ninataka kwenda kuyafukua makaburi yao ili tuone kama miili ya matu hao imo ndani.”

“Ni wazo zuri. Hilo litakuthibitishia wewe kama watu hao ni mizuka au si mizuka.”

“Nimeshamfahamisha mkuu wa gereza kesho tunatarajia kuomba kiballi cha mahakama ili turuhuisiwe kuyafukua makaburi yao kwa ajili ya uchunguzi.”

“Sasa hiyo kazi ya kuomba kibali niachie mimi. Kibali utakuja kukichukua kwangu. Wewe usisumbuke kwenda mahakamani. Nitakapokuwa ninacho mkononi nitakupigia simu. Sawa?”

“Nadhani tumemaliza.”

Nikakata simu. Sikutaka kuendelea kukaa ofisini nikatoka. Niliona niende nyumbani kwangu nikatulize akili yangu.

Wakati nimekaa kwenye kochi nyumbani kwangu niliona niyawache kwanza mawazo ya kina Unyeke. Ghafla nikamkumbuka Hamisa. Nilihisi kwamba huenda hasira yake kwa wakati ule ikawa imepungua.

Nikajishauri nimpigie simu. Wazo la kumpigia simu halikupata upinzani akilini mwangu, nikampigia. Sikuwa na uhakika kwamba angepokea simu yangu lakini ghafla simu ilipokelewa.

“Hello…! Sauti tulivu ya Hamisa ikasikika kwenye simu. Ile sauti kidogo iliutuliza moyo wangu.

“Ni njema. Fadhil nina mgonjwa ninamhudumia, nitafute muda mwingine.”

“Sawa. Nitakutafuta.”

Hamisa akakata simu yangu. Angalau nilifarijika, ameikata baada ya kunipa dharura. Kitendo cha kuongea na mimi kilikuwa kimenipa moyo kwamba ulikuwepo uwezekano wa kuzungumza tena na Hamisa na kuyamaliza matatizo yetu.

“Fadhil nina mgonjwa ninamhudumia. Nitafute muda mwingine” Maneno ya Hamisa yakajirudia akilini mwangu.

Kwa nini yalijirudia? Sikupata jibu lakini nilikuwa naujua upumbavu wa kupenda. Bila shaka Hamisa alinikosha alipolitaja jina langu na kunipa jibu lile. Kinyume chake ni kwamba sikutarajia kama angenipa jibu hilo.

Mawazo yangu yalikwenda mbali zaidi nikakumbuka siku ya kwanza niliyomjua Hamisa.

Siku hiyo Hamisa alikuja kituoni na kuripoti kwamba nyumba yake ilivunjwwa usiku na kuibiwa wakati mwenyewe akiwa kazini.

Haikuwa kazi yangu kuandikisha maelezo ya raia wanaokuja kuripoti matatizo yao, siku hiyo nilijipa kazi hiyo baada ya kushitushwa na uzuri wake.

“Una tatizo gani?” nikamuuliza.

“Nyumbani kwangu Mikanjuni”

Ilinipasa nimueleze Hamisa kwamba kulikuwa na kituo kingine cha Mabawa ambacho kinahudumia eneo lao lakini sikufanya hivyo, nikaendelea kumuuliza.