Viboko shuleni bado pasua kichwa, WHO yaonya

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imebaini kuwa adhabu ya viboko imesambaa kwa kiwango cha kutisha, ikiwakosesha usalama na haki takribani watoto 1.2 bilioni duniani kote.

 Ripoti hiyo inaonesha kuwa watoto wanakumbana na adhabu ya viboko nyumbani,  huku hali ikiwa mbaya zaidi shuleni ambapo kwa nchi za Afrika takribani asilimia 70 wanafunzi wanapewa adhabu hiyo.

 Utafiti wa shirika hilo uliohusisha takwimu kutoka nchi 58 umeonesha kuwa asilimia 17 ya watoto waliopigwa viboko Julai mwaka huu, walikumbwa na aina kali zaidi za adhabu hiyo ikiwa ni pamoja na kupigwa kichwani, usoni au masikioni, au kutandikwa mara nyingi kwa nguvu.

Wakati ripoti hiyo ikionesha hivyo, nchini Tanzania suala la adhabu ya viboko limekuwa likipigiwa kelele na wadau wa elimu na watetezi wa haki za binadamu,  jambo lililoifanya Serikali kutoa mwongozo maalumu wa utoaji wa adhabu hiyo shuleni.

Mwongozo huo unaelekeza adhabu ya viboko inapaswa kutolewa kwa mwanafunzi aliyefanya utovu wa nidhamu uliokithiri na viboko hivyo havitazidi vinne.

Aidha, anayeruhusiwa kumchapa mwanafunzi viboko ni mwalimu mkuu au mwalimu aliyeteuliwa na mwalimu mkuu.

Hata hivyo,  mwongozo huo hauzingatiwi hali inayosababisha kutokea kwa madhara makubwa, ikiwemo matukio ya watoto kupoteza maisha baada ya kukumbana na adhabu hiyo.

Februari 26, 2025 katika Shule ya Sekondari Mwasamba iliyopo Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, mwanafunzi aliyejulikana kwa jina la Mhoja Maduhu, alidaiwa kupoteza maisha baada ya kuchapwa viboko 10 na kukanyagwa kichwani na mwalimu wake.

 Mwanafunzi huyo alikumbana na adhabu hiyo baada ya kushindwa kufanya kazi za vikundi iliyotolewa na mwalimu huyo ambapo kwa mujibu wa mmoja wa wanafunzi waliokuwepo eneo la tukio, Mduhu alipigwa fimbo za kichwani na mgongoni kisha kukanyagwa.

Machi 4, 2025, Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten/Met) ulipokea taarifa kutoka kwa mwananchi juu ya kuvunjwa mkono kwa mwanafunzi Khudhaifa Salim Hamisi anayesoma darasa la pili shule ya Msingi Msufini iliyopo kata ya Chamazi Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

 Mwanafunzi huyu alivunjika mkono kufuatia kipigo kikali kutoka kwa mwalimu wake. Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi Mbande kilichopo Mbagala Wilaya ya Temeke.

 Utafiti uliofanywa na  Shirika la Hakielimu katika shule  nane  umeonyesha kuwa asilimia 98 ya wanafunzi wanajihisi kuwa salama kwa sababu walimu hawatumii adhabu za viboko.

 Ni kwa sababu hiyo shirika hilo liliungana na mashirika mengine 15 kuanzisha mtandao wa asasi za kiraia unaopambania shule salama,  lengo likiwa kuunganisha nguvu kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa watoto unapewa kipaumbele wanapokuwa shuleni.

Mkurugenzi wa shirika la haki za watoto la C-Sema Tanzania Michael Mwarwa,  anasema kutojiamini kwa wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari,  ni matokeo ya woga unaosababisha na adhabu ya viboko ana adhabu nyingine zinazotweza utu wao hivyo kuathirika kisaikolojia.

 “Hakuna utafiti wowote wa kisayansi ambao unaonesha mtoto akipigwa au akipewa adhabu ya viboko anakuwa na akili, msikivu na mwenye nidhamu, lakini kuna kazi za kitafiti za kisayansi zinaonesha mtoto akipewa malezi mazuri, akiadabishwa anakuwa mwenye akili, kujitambua na kujiamini,”anasema.

 Mkurugenzi huyo ambaye shirika lake linahusika kupokea kesi za ukatili anasema katika kipindi cha Januari na Februari, mwaka 2025 wamepokea malalamiko 52 yanayohusu ukatili kwa watoto.

 “Kupitia namba ya bure ya 116 kazi yetu ni kupokea kesi zinazohusu matukio ya ukatili, kwa upande huu wa watoto katika kipindi cha miezi miwili tumepokea malalamiko 52 yanayohusu ukatili dhidi ya watoto. Aina za ukatili zilizoripotiwa ni kupigwa, kung’atwa na kuchomwa moto sehemu mbalimbali,’’ anafafanua na kuongeza:

‘’Ukweli ni kwamba adhabu hailengi kumfundisha mtoto zaidi ya kumuumiza, sasa usitegemee kupata matokeo ya kudumu kama utampa maumivu ya kimwili na kihisia,  lakini ukimuadabisha kwa kumpa kazi za mikono,  itamsaidia na siku zote itabaki kichwani mwake.’’

Mkurugenzi wa WHO anayeshughulika na sababu za kijamii za afya Dk Etienne Krug,  anakemea hali hiyo akieleza kuwa kinachofanyika ni unyanyasaji kwa watoto.

 “Hii si nidhamu, ni unyanyasaji.Ushahidi uko wazi, viboko vinaharibu maendeleo ya kimwili, kihisia na kiakili ya watoto. Hakuna mtoto anayepaswa kupigwa kwa jina la kurekebishwa.”

“Tunapowalinda watoto dhidi ya adhabu ya viboko, tunawekeza katika familia zenye afya bora, jamii imara, na dunia yenye amani zaidi.” 

Kufuatia hali hiyo,  Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia ukatili dhidi ya watoto Najat Maalla M’jid,  amezitaka    serikali kuimarisha ulinzi wa kisheria, kupanua kampeni za uhamasishaji, na kukuza mbinu mbadala za malezi zinazoheshimu haki za watoto.

“Watoto hutumia muda mwingi nyumbani na shuleni. Wakati maeneo haya mawili yanahalalisha vurugu, yanaharibu usalama wao, utu wao, na imani yao kwa watu wazima,”anasisitiza M’jid.

Machi 6, 2025 Mwananchi lilizungumza na Kamishna wa Elimu,  Dk Lyabwene Mtahabwa aliyeeleza kuwa kinachofanywa na Serikali,  ni kufuatilia kwa ukaribu kuhakikisha mwongozo  wa utoaji adhabu shuleni unatekelezwa kama ulivyotolewa.

 Kulingana na mwongozo huo,  adhabu ya viboko vitatu  kwa mwanafunzi inapaswa kutolewa na mwalimu mkuu au mkuu wa shule au mwalimu aliyekasimiwa jukumu hilo na mkuu wa shule na inapaswa kutolewa kwa utaratibu.

 “Kusema kwamba adhabu ya viboko itaondoka kabisa sio kweli, hilo linaweza kutokea huko siku za usoni, lakini tunachofanya ni kuimarisha ufuatiliaji kuhakikisha adhabu hii inatolewa kulingana na mwongozo.

“Ufuatiliaji wetu utaongezeka maradufu, watakaokiuka watachukuliwa hatua. Hakuna kitu muhimu kwetu kama usalama wa mtoto,  hivyo wanajamii tunapaswa kushirikiana kwa kutoa taarifa pale unapofanyika ukatili ili hatua zichukuliwe,” anasema Dk Mtahabwa.

Kamishna huyo anasema ufuatiliaji huo utaenda kuongezeka maradufu kwa wathibiti ubora wa elimu,  akifafanua kwamba wao ndiyo watakuwa wa kwanza kuhojiwa yanapotokea matukio ya ukatili kwa wanafunzi shuleni. 

“Kama mthibiti ubora upo na shule yako ina kawaida ya kutoa adhabu kali basi wewe hufai, ni lazima kuwe na ufuatiliaji wa karibu kujua kinachoendelea shuleni,” alisema.

Mwelimishaji wa afua zinazoleta tija kwenye elimu,  Neema Kitundu anasema mtoto anapokosea anaweza kuadabishwa kwa kupewa kazi itakayomfanya asirudie kosa alilofanya.

 “Kazi utakayompa kulingana na umri wake itamfanya asifikirie kurudia tena kosa alilofanya, mfano kazi ya bustani, usafi na shughuli nyingine zitakazomtofautisha na wenzake na kumfanya ajutie kosa alilolofanya bila kumdhuru mwili,” anasema.

 Kwa upande wake, Mshauri kutoka shirika la Hakielimu Dk Wilberforce Meena anasema badala ya kumchapa mwanafunzi viboko kwa sababu hakufanya kazi za darasani,  mwalimu anaweza kumuongezea kazi zaidi na kuuchukua muda wake wa mapumziko.

 “Mfano mtoto hakufanya kazi ya darasani, unaweza ukamzuia asiende mapumziko ule muda wake wanacheza yeye unampa kazi nyingine ya kufanya au muda wenzake wanatoka yeye anabaki darasani kufanya zoezi ulilompa. Hii itamfunza, wakati mwingine akitaka kuacha kufanya kazi aliyopewa atakumbuka kilichomkuta,” anasema.

Naye Meneja program wa shirika la Children in Crossfire, Saraphina Lelo anasema licha ya aina hiyo ya ukatili kufanyika zaidi shuleni, ipo hatari ya kuendelea kutengeneza jamii yenye vitendo vya ukatili.

 “Inawezekana haya yanafanyika shuleni lakini huyu mtoto anakuwa na kiwewe muda wote na anaamini huo ndiyo mfumo wa maisha. Ikumbukwe huyu mtoto ndiye atakuja kuwa baba au mama hivyo anaweza kuendeleza adhabu hiyo kwa watoto wake. Jamii itaendelea ikijua viboko ndiyo adhabu sahihi kwa mtoto wakati inamuumiza,” anasema Saraphina.