Dar es Salaam. Kuna uhusiano wa karibu baina ya elimu na kipaji. Elimu inakuwezesha kukidhi matarajio yako na ya wengine ila kipaji kinakidhi matarajio yako.
Ukiwa na elimu na kipaji, unafika mbali zaidi kuliko ukiwa na kimoja peke yake.Kila mtu ameumbwa na kipaji.
Mwanasaikolojia, Howard Gardner katika nadharia yake amechambua aina mbalimbali za uwezo wa watu na vipawa walivyojaaliwa na Mungu.
Gardner anabainisha kuwa kuna vipaji vya aina mbalimbali ambavyo kila mtu, Mungu amempa
Kwa mfano, kuna kipaji cha kutumia mwili (Bodily-kinesthetic intelligence) hapa ndiyo wanapatikana waruka sarakasi,wacheza dansi)
Kipaji cha kuzungumzaji(Linguistic intelligence), wachekeshaji,na wazungumzaji wazuri wa kisiasa wanatoka katika kundi hili.
Uwezo na kipaji cha kuwajua watu haraka(interpersonal intelligence). Kuna watu wanasomeshwa ili wawajue watu kiundani ndani ya muda mfupi na kuna watu hawakusoma lakini wanawajua watu vizuri sana.
Hicho ndicho huitwa kipaji.Kipaji ni uwezo wa asili wa kufanya jambo bila kufundishwa au kutumia nguvu sana. Kuna njia tano ambazo unaweza kuzitumia kugundua kipaji chako.
Angalia unaweza kufanya jambo gani bila kutumia nguvu nyingi na ukalifanikisha jambo hilo vizuri na kwa urahisi.
Shiriki katika mambo ambayo unadhani unayaweza ili uweze kujua kipaji chako, kama vile;kucheza mpira,mashindano ya uandishi wa riwaya,mashairi na tamthilia.
Kitafute kipaji chako kwenye ‘hobby’ yako, kama una hobby ya kutazama tamthilia, unaweza kuwa na kipaji cha utunzi wa tamthilia au riwaya bila ya wewe kujijua,jaribu kuandika ili ugundue kipaji chako.
Waulize watu waliokuzunguka juu ya kile wanachokiona kwako.Watu wa karibu wanaweza kukusaidia kukwambia uwezo na kipaji chako.Waulize leo ikiwa bado hujajua kipaji chako.
Waulize wazazi wako,wao wameshuhudia kila hatua uliyopitia katika maisha yako ya utotoni na ujanani hivyo wanajua ulikuwa unapenda nini na unaweza nini zaidi.
Kupitia ulivyokuwa unavipenda na kuvifanya,kuna kipaji kimejificha hapo.Wazazi wana nafasi kubwa na muhimu katika hatua ya utambuzi wa kipaji.Jitahidi kujua kipaji chako ili ujue uwezo wako wa asili.