NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji, wasambazaji, wafanyabiashara na waingizaji wa bidhaa nchini kuhakikisha bidhaa wanazozalisha au kuuza zinakidhi matakwa ya viwango na ubora ili kulinda afya za wananchi na kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora sokoni.
Akizungumza leo Septemba 1, 2025 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Meneja Ukaguzi na Utekelezaji wa Sheria wa TBS, Bi. Nuru Mwasulama, amesema kuwa bidhaa yoyote kabla ya kutumika inapaswa kukidhi matakwa ya usalama na ubora na kupata ruhusa rasmi ya kutumika.
Aidha Bi. Nuru amebainisha kuwa TBS imeendelea kufanya ukaguzi sokoni ili kubaini bidhaa hafifu zisizokidhi viwango na kuondoa sokoni zile ambazo hazifai kwa matumizi ya wananchi.
“Katika kusimamia udhibiti wa ubora, bidhaa zinazozalishwa viwandani ndani ya nchi hupatiwa ithibati ya ubora kwa kuzingatia matakwa ya viwango. Kwa bidhaa kutoka nje ya nchi, hususan vyakula na vipodozi, hufanyiwa usajili kulingana na viwango husika,” amesema.
Pamoja na hayo ametaja baadhi ya bidhaa hafifu zisizofaa kuwepo sokoni kuwa ni pamoja na vipodozi vilivyopigwa marufuku, nguo za ndani za mitumba, vifaa vya ujenzi visivyokidhi vipimo na bidhaa zilizochezewa vifungashio.
Vilevile Bi. Nuru amewataka wananchi kujenga tabia ya kukagua vifungashio vya bidhaa kabla ya kununua ili kubaini kama havijabadilishwa au kuchezewa.
Hata hivyo pia amewakumbusha wazalishaji, waingizaji na wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa zao zinazingatia viwango vya ubora kwa kuwa suala la usalama wa wananchi ni la kila mdau.