Tuwajenge watoto kupenda elimu tangu utotoni

Dar es Salaam. Katika jamii yoyote ile elimu ni silaha muhimu ya kuleta mabadiliko ya kweli.

Kupitia elimu, mtu anaweza kufikia ndoto zake, kuibadilisha familia yake, na hata kulibadili taifa zima. Hali hii inaleta umuhimu wa kumjenga mtoto kupenda elimu tangu akiwa mdogo.

Ni jambo lisilopingika kwamba mapenzi ya elimu hayaanzi tu ghafla mtoto anapofikia umri wa shule ya sekondari au chuo kikuu, bali hujengwa hatua kwa hatua, tangu akiwa katika umri wa awali kabisa. Kujenga msingi huu imara wa mapenzi kwa elimu kunamhakikishia mtoto mwelekeo bora wa maisha yake ya baadaye.

Ndio maana hata Dira ya maendeleo ya Taifa letu ya 2050, imeweka msisitizo mkubwa katika uwekezaji unaopaswa kufanywa katika ngazi ya elimu ya awali kama mahala unapojengwa msingi wa kuja kuwa na wananchi walioelimika.

Katika familia nyingi, bado kuna changamoto kubwa ya watoto kutopenda kusoma. Watoto wengi hukua bila kufundwa au kuhamasishwa kuhusu thamani ya elimu. Wanapopewa vitabu hawaoni umuhimu wake, na baadhi yao huona kama ni adhabu.

Tatizo hili lina madhara makubwa kwa maendeleo yao ya baadaye. Mtoto ambaye hapendi kusoma anakosa msingi wa maarifa, fikra bunifu, na uwezo wa kujitegemea kiakili.

Matokeo yake, hata watoto wenye uwezo mkubwa wa kiakili hujikuta wakiyumba katika masomo, kupoteza mwelekeo na hatimaye kuacha shule. Hii ni hasara si tu kwa familia zao bali kwa jamii nzima.

Kuna watoto wengi  walioonyesha viwango vya juu vya uwezo wakiwa wadogo, lakini kutokana na ukosefu wa msukumo sahihi kutoka kwa wazazi au walimu, waliishia kuwa watu wa kawaida  au hata kuacha shule. Miongoni mwao walikuwepo ambao wangeweza kuwa madaktari, wahandisi, marubani, wanasayansi au hata mawaziri.

Lakini kwa sababu mapenzi ya elimu hayakujengwa ndani yao tangu utotoni, walikosa msukumo wa ndani wa kuendelea na masomo. Kosa hili mara nyingi huwa si la mtoto bali ni la wale waliomzunguka, hususan wazazi na walimu.

Wazazi wana nafasi kubwa sana katika kujenga mapenzi ya mtoto kwa elimu. Malezi ya awali ndiyo msingi wa maisha ya mtoto. Mzazi anayemfundisha mtoto kusoma vitabu, kusikiliza simulizi zenye mafunzo, kumpongeza anapofaulu, na kumsaidia anapokwama, anamjengea mtoto hali ya kuamini kuwa elimu ni jambo la thamani.

Mzazi anayejali maendeleo ya mtoto wake kielimu anakuwa ameshachukua jukumu lake la msingi kama mlezi.

Pale  mzazi anapopuuza masuala ya elimu na kumwachia mtoto aamue mwenyewe, ni rahisi kwa mtoto huyo kupotea njia. Elimu ni mbegu inayohitaji kupandwa kwa uangalifu na kumwagiliwa kwa upendo na mwongozo wa kila siku.

Lakini mzazi peke yake si wa kulaumiwa wala si wa kupongezwa peke yake. Walimu nao wana mchango mkubwa sana katika maisha ya mtoto. Walimu ni walezi wa pili, na mara nyingi watoto hutumia muda mrefu shuleni kuliko nyumbani.

Mwalimu bora ni yule anayejua namna ya kumvutia mtoto kwenye elimu, kumfanya aione shule kuwa sehemu salama na ya kufurahisha, na kumtia hamasa ya kuwa bora zaidi kila siku.

Kwa bahati mbaya, baadhi ya walimu wamekuwa chanzo cha watoto kuchukia shule na elimu kwa ujumla. Wapo walimu wanaowatisha watoto, kuwabeza, au kuwafanya wajisikie hawana thamani kwa sababu ya makosa madogo au udhaifu wa kiakili. Mtoto anapopoteza ujasiri mbele ya mwalimu wake, hawezi tena kupenda kusoma.

Katika karne ya ishirini na moja, ambapo dunia imejaa ushindani mkubwa wa maarifa, teknolojia na ubunifu, elimu si chaguo bali ni hitaji. Mtoto asiyeandaliwa vyema leo atakuwa mzigo kwa Tanzania ya kesho.

Dunia ya leo haitambui tena hadhi ya familia, kabila au nafasi ya kijamii kama vigezo vya mafanikio, bali inathamini uwezo, maarifa na ujuzi.

Ndiyo maana kila mzazi na kila mwalimu anapaswa kuona wajibu wake katika kumjengea mtoto msingi wa kupenda elimu kama jambo la dharura na la lazima.

Wazazi hawapaswi kusema mtoto atajifunza mwenyewe kadri anavyokua. Hawapaswi pia kuchukulia elimu kama jukumu la walimu pekee. Badala yake, wanapaswa kuwa wa kwanza kumtia moyo mtoto wao, kumweleza faida za elimu, na kumwekea mazingira ya kusoma nyumbani.

Wawapeleke watoto maktaba, wawanunulie vitabu, na wawahimize kuuliza maswali. Kwa upande mwingine, walimu wazingatie kuwa wao ni mfano wa kuigwa. Kwa maneno yao na matendo yao, watoto hujifunza kupenda au kuchukia elimu.

Katika dunia ya sasa, elimu ni njia kuu ya kufungua milango ya mafanikio. Kupitia elimu, mtoto wa maskini anaweza kuwa kiongozi, mtoto wa kijijini anaweza kuwa mtaalamu wa kimataifa, na mtoto wa familia ya kawaida anaweza kuvumbua suluhisho la matatizo ya dunia.

Haya yote yanawezekana ikiwa tutaanza kuwaandaa watoto wetu mapema, tukiwajengea mazingira ya kupenda elimu tangu utotoni. Kupuuza jambo hili ni sawa na kuandaa kizazi cha watu watakaokuwa na maisha ya utegemezi, lawama na majuto.

Kujenga mapenzi ya elimu ni kazi ya pamoja inayohitaji ushirikiano kati ya wazazi, walimu, na jamii nzima. Mtoto anapopewa upendo, mwongozo na msukumo sahihi, huwa na nafasi kubwa ya kupenda elimu na kuitumia kubadili maisha yake.

Tukumbuke, msingi bora wa maisha bora ya baadaye huwekwa leo  katika miaka ya mwanzo ya maisha ya mtoto. Na hakuna msingi bora kuliko kumpa mtoto elimu na hamasa ya kuipenda elimu hiyo kwa hiari yake mwenyewe.