Buzungu mbioni kurejea Mtibwa Sugar

KIUNGO wa Kagera Sugar, Omary Buzungu ameuomba uongozi wa timu hiyo umruhusu arejee Mtibwa Sugar baada ya kikosi cha ‘Wanankurukumbi’ kushuka daraja ikiwa ni miezi sita  tangu nyota huyo alipojiunga nacho wakati wa dirisha dogo la Januari, mwaka huu.

Nyota huyo alijiunga na Kagera Sugar katika dirisha dogo la Januari 2025 akiwa ni pendekezo la aliyekuwa Kocha wa Mtibwa Sugar ambaye raia wa Marekani, Melis Medo aliyempendekeza akafanye naye tena kazi kutokana na uhusiano mzuri waliokuwa nao.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinaeleza Buzungu ameomba kusitisha mkataba wake na Kagera Sugar wa mwaka mmoja na miezi sita uliobaki, huku uongozi ukiwa tayari kumruhusu kurudi Mtibwa kutokana na uhusiano wa kibiashara baina ya pande hizo. “Mazungumzo ya kurudi yanaweza kukamilika siku hizi zijazo kwa sababu ya uhusiano mzuri baina ya pande zote mbili, hata sisi tulivyomruhusu kuondoka haikuwa na maana tulikuwa hatumuhitaji, ila tulitumia busara zetu,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya msimu ujao na tayari wapo wachezaji wanaofanya pia mazungumzo nao, hivyo muda utakapofika watawaweka wazi.

Ikiwa dili hilo litakamilika, Buzungu atakuwa mchezaji wa pili wa Kagera Sugar kujiunga na Mtibwa Sugar katika dirisha hili kubwa la usajili, baada ya kikosi hicho kufikia pia makubaliano ya kumsajili aliyekuwa beki wa kulia, Datius Peter.

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu uliopita, imerejea tena Ligi Kuu ikiwa ndio mabingwa wa Ligi ya Championship baada ya kumaliza kinara na pointi zake 71, ikiungana na Mbeya City iliyorejea pia kufuatia kushuka daraja msimu wa 2022-2023.