Upatu wa kinamama wasaidia kupata majiko ya nishati safi

Mwanza. Baadhi ya kinamama mkoani Mwanza wameamua kushirikiana kupitia michezo ya upatu ili kumudu gharama za majiko ya nishati safi, baada ya kutambua madhara ya kutumia kuni na mkaa.

Kwa muda mrefu, maisha ya kinamama wa Mwanza, hasa wajasiriamali wanaokaanga na kuuza samaki, yamekuwa yakitegemea kuni na mkaa.

Hali hiyo si tu imekuwa ikiathiri macho na mapafu, bali pia imewalazimisha kutumia fedha nyingi kila siku.

 Hata hivyo, mabadiliko yanaanza kujitokeza baada ya elimu ya nishati safi kuwafungua macho.

Wanawake hao sasa wanaamini mshikamano wao kupitia michezo ya upatu ndio suluhisho la kumiliki majiko ya gesi na umeme.

Upatu unavyowaokoa
Mkazi wa Ibanda ambaye ni  mama lishe, Salome Bahati anasema kwa siku hutumia mkaa wa zaidi ya Sh15,000 kupikia vyakula anavyouza kwenye mgahawa wake.

“Nimepewa elimu ya kutumia nishati safi na nimetambua faida zake. Ukiwa na jiko la umeme unapika chakula chote ndani ya saa moja, tofauti na mkaa unaochukua muda mrefu na gharama kubwa ,” anasema.

Changamoto ni bei ya majiko haya, ndiyo maana tunaona bora tushirikiane kwa upatu. Tukicheza upatu, kila mwezi mama mmoja tunamnunulia jiko la umeme au vifaa vya kupikia vya umeme hadi kila mmoja apate jiko lake

Salome anaeleza kuwa, tayari ameanza kuzungumza na wenzake eneo analofanyia biashara ili waanze kuchangia kila wiki kuondokana na matumizi makubwa ya mkaa yanayochangia uharibifu wa mazingira.

“Hata tukichanga Sh5,000 kila mmoja, baada ya miezi michache tunapata jiko. Hii itatusaidia kuacha moshi na kuokoa maisha yetu,” anasema.

Mkazi wa Bwiru Bima, Amina Jumanne anasisitiza mshikamano wa kina mama kupitia vikoba na michezo ya upatu, akishauri wengine kuchangiana kwa ajili ya vifaa vya nishati safi badala ya kugawana pesa ambazo wakati mwingine huishia bila kutimiza malengo.

“Majiko yapo lakini bei ni kubwa. Hatuwezi kununua gesi ya Sh25,000 mara moja. Tunaomba Serikali itusaidie, lakini kwa upande wetu tumeamua kujipanga wenyewe. Tutashirikiana kupitia vikoba, kila mwezi kinamama wawili au watatu wanapata jiko. Hii ni njia pekee ya kuhakikisha hakuna mama anayebaki nyuma,” anasema.

Maria Chacha, mkaanga samaki katika Mwalo wa Kishimba na mkazi wa Ibungilo, ambaye anatumia jiko la umeme kwa mkopo, anasema tofauti ya gharama ni kubwa sana.

“Gunia la mkaa natumia zaidi ya Sh62,000 kwa mwezi, lakini kwa jiko la umeme natumia Sh1,000 kwa siku na bado nabakiza. Changamoto ni malipo ya mkopo kupitia kampuni mbalimbali, wakati mwingine wananichanganya. Ndiyo maana upatu ni bora… mtu anapata jiko moja kwa moja na analimiliki,” anasema.

Madhara ya kuni na mkaa
Rozy Nyembo, muuzaji wa samaki katika mwalo wa Kishimba, anasema kutokana na moshi na joto la kuni, hulazimika kunywa lita tano za maji baridi kwa siku na wakati mwingine hadi lita 10.

“Kutokana na joto na moshi wa kazi zetu, kila siku natumia angalau kidumu cha lita tano cha maji ya baridi. Kikiwa si baridi, basi natakiwa kuongeza zaidi kwa sababu ya joto kali,” anasema.

Maria Chacha anasema moshi umekuwa adui mkubwa wa kinamama, licha ya macho kutoa machozi wakati wa kukaanga dagaa, usiku hulala kwa tabu kutokana na kuwashwa na macho.

“Madhara tunayoyapata ni makubwa ikiwamo macho kuuma masaa yote. Unapofika muda wa kulala, ukifumba macho yanaanza kuuma. Yakishatoa machozi unapata unafuu, lakini bado ni shida kubwa,” anasema.

Mwenyekiti wa Mwalo wa Kishimba, Khalid Masesa anasema matumizi ya kuni yamesababisha soko hilo kuungua zaidi ya mara nne.

“Soko hili linahudumia wauzaji wengi wa samaki wa kukaanga, lakini kuni tunazotumia ni hatari kiafya na kibiashara. Wakaangaji wanaumia macho na vifua, wateja wanalalamika. Pia, moto umetokea mara nne kwa sababu kuni zinaachwa zikiwaka. Tukipata majiko ya gesi au umeme, tutapunguza hatari zote,” anasema.

Khalid anaeleza kuwa gharama za kuni ni kubwa, kwani mfanyabiashara anaweza kutumia zaidi ya Sh200,000 kwa siku, wakati umeme au gesi haviwezi kufikia kiwango hicho.

“Tatizo ni elimu. Wengi wanadhani umeme ni ghali, kumbe ni nafuu. Elimu ikitolewa na bei ikipunguzwa, kila mtu atakimbilia nishati safi,” anasema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Medical Research, Kata ya Kitangiri wilayani Ilemela, Yudas Hume anasema ujio wa elimu ya nishati safi umekuja kwa wakati muafaka.

“Kwenye mtaa wangu kuna kaya zaidi ya 800 na watu zaidi ya 22,000. Wengi wao ni kinamama wajasiriamali. Mwamko wa kutumia majiko haya upo,” anasema.

 “Napenda kuishukuru Serikali ya Mama Samia kwa hatua hii. Imepunguza gharama za maisha hasa tulipotegemea kuni na mkaa. Ujio huu unatupunguzia mzigo.”

Anashauri elimu iendelee kutolewa na Serikali iangalie namna ya kupunguza gharama za vifaa vya nishati safi ili kila mwananchi aweze kumudu.

Kampeni ya matumizi ya nishati safi
Mhamasishaji wa Kampeni ya Pika Smart, Dolla Urio anasema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wote wanatumia nishati safi.

“Tupo Mwanza kwa ajili ya Kampeni ya Pika Smart kuhakikisha wananchi wote wanatumia vifaa vya kisasa vinavyotumia nishati safi. Serikali imeweka lengo kwamba, ifikapo 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi. Kwa sasa ni asilimia 20 pekee. Kwa elimu tunayotoa tunaamini tutaunga mkono kaulimbiu ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Nishati Safi kwa Wote,” anasema.

Dolla anasema mwitikio wa watu wa Mwanza umekuwa mkubwa kwani kwa siku wanaweza kuelimisha zaidi ya watu 100. Wengi huomba Serikali iwasaidie kupata majiko kwa mkopo.

“Hiyo ni changamoto tunayoipeleka serikalini. Pia, utafiti unaonesha kwamba kwa kutumia jiko sanifu, unaweza kutumia kati ya Sh200 na 700 kwa siku, wakati mkaa mtu hutumia Sh10,000 hadi Sh15,000. Ni tofauti kubwa,” anasema.