Yanga itazindua tamasha la Wiki ya Mwananchi kesho katika Viwanja vya Zakhem vilivyopo Mbagala jijini Dar es Salaam huku ikithibitisha kuwa baadhi ya tiketi zimeisha.
Meneja wa Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesema katika uzinduzi huo watataja majina ya wasanii watakaonogesha kilele Cha tamasha hilo litakalofanyika Septemba 12.
Kamwe amesema wamefanya maboresho makubwa kuelekea kilele cha Wiki ya Mwananchi kitakachofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Amesema kutakuwa na burudani nzuri na kubwa kutoka kwa wasanii wakubwa zitakazofuatiwa na michezo mbalimbali ya soka.
“Tumefanya kazi kubwa ya kupanga hizo burudani. Tamasha siku hiyo litaanza asubuhi saa tano, kwa hiyo tunataka kuwe na burudani kubwa kwa Wananchi,” amesema Kamwe.
“Ukiacha suala la burudani kutakuwa na mechi mbalimbali, lakini kubwa tutaanzia na mchezo wa timu yetu ya wasichana – Yanga Princess ambayo imefanyiwa maboresho makubwa.
“Kutakuwa na mchezo wa viongozi wa klabu yetu watakaocheza na watu maarufu wa Yanga. Hapa niwape siri makocha wetu Romain Folz na wasaidizi wake Manu Rodriguez watakuwa uwanjani.”
Kamwe ametambulisha kaulimbiu itakayobeba tamasha hilo akisema itakuwa ‘Tunapiga kichwani’ ikilenga kuendeleza vipigo kwa wapinzani wao.
“Kaulimbiu hii tumesema tuje nayo ili kuwafikishia salamu tutakaokutana nao kwamba kwa kuwa washazoea vipigo sasa Yanga inakuja kupiga kichwani. Ndio maana mnaona ile nyundo pale (anaonyesha mchoro wa nyundo uliopo katika bango).”
Amewataka mashabiki kuendelea kununua tiketi za tamasha hilo akithibitisha tayari zile za VIP A zimeshakwisha.