Kocha Fountain Gate Princess azitaka Simba, Yanga

KOCHA wa Fountain Gate Princess, Noah Kanyanga amesema mikakati ya timu hiyo ni kuhakikisha inarudi kwenye makali yake na kupambania ubingwa mbele ya vigogo Simba Queens na Yanga Princess.

Kanyanga aliwahi kuzifundisha Ceasiaa Queens, Mburahati Queens, Gets Program na sasa Fountain Gate aliyoanza nayo mwishoni mwa msimu uliopita.

Akizungumza na Mwanaspoti, alisema msimu uliopita haukuwa mzuri kwao na sasa wameingia mapema kambini miezi miwili kabla ya Ligi Kuu ya Wanawake kuanza mwezi Oktoba ili kujiandaa ambapo watakuwa na kambi ya mwezi mmoja Dodoma kisha watasafiri hadi Dar es Salaam kuweka kambi ya mwezi mmoja ambayo itaambatana na mechi za kirafiki.

“Mwishoni mwa msimu nilipambana kama kocha kuinusuru timu isishuke daraja. Tuliteleza msimu uliopita na hatutaki kurudia makosa, lengo ni kufanya vizuri na tunautaka kuirudisha Fountain ile yenye makali yake,” alisema.

“Tumekuja Dodoma sababu ndio makao makuu ya Fountain, pia ni sehemu iliyotulia, hivyo tulikuja huku ili wachezaji wazoeane kwanza kisha tutapata mechi za kirafiki za kujipima sababu Dar kuna timu nyingi.”

Kanyanga alieleza kwamba kwa usajili walioufanya msimu huu hakuna shaka watafanya vizuri kama changamoto ya vibali vya wachezaji itatatuliwa mapema mashabiki wasubiri kuona ushindani watakaouonyesha.

“Tumeongeza wachezaji wadogo na wale wenye uzoefu wameongeza morali kwenye timu. Tumekuwa na mazoezi mara mbili – asubuhi na jioni lengo ni kuweka miili vizuri na kurudi kwenye hali yake.”

Kocha huyo anayejivunia mafanikio ya kuwatoa nyota kama Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, Asha Mwalala, Janet Pangamwene na wengineo aliongeza kuwa atajiunga na JKU Queens kwa muda ili kuisaidia kwenye michuano ya Cecafa kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake.

“Nina leseni B ya ukocha ambayo inaruhusiwa na CAF kusimamia mashindano hayo. JKU ya Zanzibar wameniazima mara moja niongeze nguvu kisha nitarejea kwenye majukumu yangu, pia nitachukua na wachezaji,” alisema