Mbulu. Mgombea ubunge wa Mbulu Vijijini mkoani Manyara kwa tiketi ya ACT – Wazalendo Flatei Massay amekiacha solemba chama hicho na kurudi CCM.
Massay ambaye amekuwa mbunge wa Mbulu Vijijini kwa miaka 10 mfululizo, alihama CCM baada ya jina lake kukatwa na kutoshiriki kura ya maoni kuwani kipindi cha tatu.
Baada ya kujitoa CCM Massay alichukua fomu ya kugombea ubunge kwa tiketi ya ACT – Wazalendo Agosti 24 mwaka 2025 na kupitishwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Agosti 27, 2025.
Chama hicho kikiwa tayari kimejihakikishia mgombea, kwenye ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara Stephen Wasira Septemba mosi 2025, Massay alitangaza uamuzi huo mpya wa kurudi CCM.
Akizungumzia uamuzi huo, Massay amesema amechukua uamuzi huo baadhi ya wazee kumuomba arudi kwenye chama hicho tawala.
“Wazee wa jadi wakikuomba jambo unapaswa kukubali, walikuja kwangu wakiwa wamebeba majani na kuniomba nirudi CCM,” amesema Massay ambaye amekuwa maarufu kwa kuruka sarakasi bungeni.
Amesema atashirikiana na viongozi na wanachama wa CCM kuhakikisha zinapatikana kura za kutosha kwa nafasi ya urais, wabunge na madiwani wa CCM.
Akizungumza baada ya mapokezi ya mgombea huyo, Wasira amempongeza kwa uamuzi huo aliouchukua.
Wasira amesema uamuzi huo ni wa busara kwani Massay ni kijana ambaye amelelewa CCM na amekomaa kisiasa.
Katibu wa CCM mkoa wa Manyara, Shaban Mrisho amesema kati ya majimbo saba, wagombea ubunge wa CCM wa Hanang’ na Babati Vijijini hawana wapinzani baada ya Massay kujitoa.
Mrisho amesema kwa upande wa madiwani, kati ya kata 142 za mkoa wa Manyara, kwenye kata 96 CCM haina wapinzani.