Dk Nchimbi: Mpina nipigie kura na rejea CCM, yeye amjibu akisema…

Kisesa. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amemtumia ujumbe Luhaga Mpina wenye mambo mawili akimtaka ayatekeleze kwa sababu:”Mimi ni kaka yake kwa hiyo hana sababu ya kukataa.”

Dk Nchimbi ameutoa ujumbe huo leo Jumanne, Septemba 2, 2025, nyumbani kwao Mpina, eneo la Mwandoya, Jimbo la Kisesa, mkoani Simiyu aliposimama kuwasalimia wananchi na kuwaomba kura katika uchaguzi mkuu.

Mpina ameongoza jimbo hilo kwa miaka 20 mfululizo kuanzia 2005-2025. Katika mbio za mwaka huu alijitosa tena lakini jina lake halikurejeshwa na Kamati Kuu ili kuingia ungwe ya kura za maoni Agosti 4, 2025.

Kutokurejeshwa kwa jina hilo, kulimfanya waziri huyo wa zamani wa mifugo na uvuvi kutafuta jukwaa jingine la siasa na Agosti 5, 2025 alijiunga na ACT Wazalendo.

Agosti 6, 2025, mkutano mkuu maalumu uliofanyikia Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam ukamchagua kuwa mgombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Hata hivyo, wakati akiendelea kutafuta wadhamini kwenye mikoa 10 ikiwemo miwili ya Zanzibar ili kukidhi masharti ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Monalisa Ndala akaibua malalamiko dhidi ya Mpina.

Monalisa ambaye alikuwa Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam alidai kukiukwa kwa kanuni za uendeshaji wa chama hicho. Malalamiko aliyafikisha Ofisi Katibu Mkuu wa chama hicho na nakala kwenda kwa msajili wa vyama vya siasa.

Baadaye Monalisa alifikisha suala hilo ofisi ya Msajili. Msajili alilishughulikia kwa kuziita pande zote zinazosigana na mwisho akaamua malalamiko dhidi ya Monalisa yako sahihi na kuiandikia INEC barua kwamba Mpina hana vigezo vya kuteuliwa.

Mpina hakukubali amefungua kesi Mahakama Kuu na kesi inaendelea.

Leo Jumanne, Dk Nchimbi na msafara wake ukitokea Itilima kwenda Meatu, umesimama Mwandoya kusalimia na kuwaomba Oktoba 29, 2025 iwachague kwani wamejipanga kuendeleza miradi mbalimbali ya afya, elimu, barabara na maji.

Katikati ya kuomba kura, Dk Nchimbi akasema:”Mdogo wangu asiponipigia kura atakuwa amekosa adabu. Si nilikuja hapa akasema mimi ni kaka yake basi anipigie kura.”

Dk Nchimbi akiwa Katibu Mkuu wa CCM alifanya ziara mkoani Simiyu na kufika eneo hilo la Mwandoya kipindi ambacho Mpina alikuwa bado mbunge na kuwaeleza wananchi wa hapo kuwa Dk Nchimbi kwake ni kaka yake na wameshirikiana tangu Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Huku wananchi wakimsikiliza leo kwenye mkutano huo, Dk Nchimbi akaeleza jambo la pili kwa mdogo wake Mpina kwamba wamfikishe kuwa:”Kaka yako (Dk Nchimbi) alipita hapa, akirudi tena nitapokea kadi yake (ya ACT Wazalendo) na mimi nitaipokea mwenyewe kadi yake. Tunajua ukitoka harafu…unarudi.”

Miongoni mwa wana CCM waliowahi kutoka na wakarudi ni waliowai kuwa mawaziri wakuu, Edward Lowasaa na Fredrick Sumaye. Pia, yumo aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe. (Membe na Lowasaa kwa sasa ni marehemu).

Mara baada ya Dk Nchimbi kumaliza kutoa ujumbe wake huo, Mwananchi limemtafuta Mpina kwa simu. Alipoelezwa mambo hayo kwanza ameanza kwa kuoonesha mshangao.

“Sasa nampigiaje yeye na mimi ni mgombea,” amehoji Mpina.

Alipoulizwa suala la kurejea tena CCM, Mpina akasema:”Narejeaje CCM wakati mimi ni mgombea? Nafikiri umenielewa..”

Mwananchi limezungumza na Petro Njiluku, Mkazi wa Mwandoya ambaye alikuwapo kwenye mkutano huo ambaye amesema:”Mpina hawezi kumpigia, kwa sababu yaliyotokea sijui ila sidhani.”

Njiluku amesema:”Hapa hawana chuki na CCM bali wana chuki kwa sababu mtu aliyeenguliwa wanampenda.”

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi akamwita Kada wa chama hicho aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini 2010-2020 kupitia Chadema, Mchungaji Peter Msigwa kuwasalimia.

Mchungaji Msigwa amesema kazi kuhwa imefanyika ya kuwaletea maendeleo:”Na Mpina tulikuwa naye bungeni. Naamini atasikia wito wa Dk Nchimbi na atarudi.”

Mgombea ubunge wa Kisesa, Godfrey Mbuga amesema wamejipanga kufanya siasa za kistaarabu kwani:”Tumeshavunja makundi na tuwe kitu kimoja.”

Mbuga amesema utekelezaji wa ilani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ndio turufu yao kurudi tena kwa wananchi kuwaomba ridhaa.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua yanayotolea kwenye msafara wa Dk  Nchimbi akizisaka kura.