Dar es Salaam. Kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu zimefikia siku ya saba, huku wagombea urais wa baadhi ya vyama vya siasa wakisuasua kufanya mikutano ya kampeni kwa kile wanachodai wapo kwenye mipango ya kuibuka kwa kishindo.
Pamoja na mikakati hiyo ya kuibuka kwa kishindo, suala la ukata nalo wamelitaja kuwa miongoni mwa sababu za kusuasua kwao, wakisema wameamua kuanza na siasa za chini chini kabla ya kuanza mikutano mikubwa ya hadhara.
Pazia la kampeni za uchaguzi wa mwaka huu limefunguliwa Agosti 28, huku Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Kijamii (CCK), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Wakulima (AAFP), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na UDP ndivyo pekee vilivyozindua kampeni za urais mpaka sasa.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Philemon Mtoi amesema tofauti ya nguvu, uwezo na misuli kati ya chama kimoja na kingine ndiyo sababu ya hali inayoendelea kushuhudiwa.
Amesema katika siasa za Tanzania, kuna chama chenye nguvu ya rasilimali na uchumi, huku vingine vikitegemea ama kufadhiliwa au kudunduliza kidogo vinachokipata kufanya shughuli zake.
Katika mazingira hayo, amesema haishangazi kuona mgombea wa urais akishindwa kufanya mikutano ya kampeni, badala yake anaonekana huku na kule, ilimradi naye aonekane alifanya jambo wakati wa kampeni.
“Tuchukulie uwezo wa CCM haulingani na chama kingine chochote kwa sasa. Hupaswi kushangaa kuona mgombea wa chama hicho anaendelea na mikutano kwa mujibu wa ratiba, lakini chama kingine kinashindwa,” amesema.
Mtoi amesema kampeni zinahitaji uwezo wa kifedha kwa sababu kufanyika kwake kunatumika rasilimali nyingi.
“Huwezi kusema unafanya kampeni, huna fedha, huna rasilimali mfano magari, huna mafuta, huna wasaidizi kwa ajili ya mambo ya kawaida kwenye kampeni. Sasa kama chama kina uwezo duni kifedha, kinaamua kukaa kimya, kinavuta muda ili kifanye mikutano michache kulingana na uwezo wake,” amesema.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), chama cha NRA kilipaswa kufanya uzinduzi wa kampeni zake za mgombea urais Agosti 28, katika uwanja wa Kawawa mkoani Kigoma, lakini hakikufanya hivyo.
Siku mbili baadaye, mgombea urais wa chama hicho, Hassan Almas, alionekana katika Soko la Mbagala akizungumza na wananchi waliokuwepo sokoni hapo.
Alipoulizwa sababu za kutozindua kampeni hizo siku hiyo, mgombea huyo amesema ameamua kuanza na mikakati kwa ajili ya kuelekea siku ya uzinduzi.
Katika hatua ya sasa, amesema chama chake kimeamua kufanya siasa za chini chini na kukutana na viongozi kwa ajili ya mikutano ya ndani kuandaa mazingira.
“Tulianza Dar es Salaam kukutana na viongozi wa chama kutengeneza mikakati na sasa tunakaribia kuingia Kilimanjaro, na tutafanya mikutano ya ndani na kutengeneza mkakati wa kwenda,” amesema Almas.
Hata hivyo, mgombea huyowa urais amesema suala la fedha ni miongoni mwa mambo yanayosababisha waanze na mkakati huo.
“Fedha inaweza kuwa kikwazo, kila kitu kinahitaji fedha. Fedha ni lazima, ndiyo maana tunafanya mikakati hii kwa sababu ya masuala ya kifedha,” amesema.
Amesema Tanzania ni kubwa, ni vigumu kufika katika kila eneo, isipokuwa watafanya kila namna kuhakikisha wananchi wanafikiwa hata kwa njia ya mtandao.
Kama ilivyo kwa NRA, chama cha ADC nacho kilipanga kingeanza mikutano yake ya kampeni Agosti 28, mkoani Mwanza, lakini hakikufanya hivyo.
Hata hivyo, chama hicho bado hakijaanza kufanya mikutano ya kampeni, badala yake kimepanga kuanza kuifanya Septemba 7, mwaka huu, kama inavyoelezwa na mwenyekiti wake, Shaban Itutu.
Itutu amesema kinachoonekana kwenye ratiba ya INEC hakiwazuii kupanga siku wanayoona inafaa kuzindua kampeni, akisisitiza wataanza Septemba 7 na si vinginevyo.
“Sio sharti la lazima kwamba ukiwekwa kwenye ratiba kuwa utafanya mkutano leo, eti lazima ufanye, hapana. Kwa hiyo hatujashurutishwa,” amesema.
Alipoulizwa sababu za kutofanya siku hiyo, amesema ni masuala ya ndani ambayo yeye na viongozi wenzake ndiyo wanaopaswa kuyajua.
“Hayo ni mambo yetu mimi na viongozi wenzangu, wewe kama mwanahabari subiri siku tutakayozindua, tutakwambia uje uchukue habari,” ameeleza Itutu.
Kwa upande wa chama cha NLD, kwa mujibu wa ratiba ya INEC, mkutano wake wa kwanza wa kampeni ulipaswa kufanyika Septemba mosi, wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam, lakini haikuwa hivyo.
Badala yake, mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Hassan Doyo, alitangaza kuanza kampeni zake Septemba 4, mwaka huu mkoani Tanga na si Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi, Doyo amesema ratiba ya awali ilipangwa ili kuvuta muda kwa ajili ya kusubiri uzinduzi mkoani Tanga.
Lakini, amesema lengo lake ni kuanza kuzindua kampeni hizo, kisha aendelee na mikutano kama ratiba inavyoeleza, na kwamba bajeti siyo tatizo kwake.
“Pia, nilishindwa kufanya mkutano siku ya kwanza kwa sababu nilikuwa na ratiba ya kuja kwa mgombea urais wa Zanzibar, ikanichukua siku mbili pale, lakini kwa sasa nipo Tanga kwa maandalizi ya uzinduzi,” amesema.
Doyo amesema, tofauti na vyama vingine, chama chake kimelenga kufanya uzinduzi wa kampeni katika viwango zaidi ya CCM.
“Ukiangalia kati ya vyama vyote ambavyo tayari vimezindua kampeni, hakuna hata kimoja kilichojipanga kufanya mkutano unaokaribia viwango vya CCM. Sasa sisi tumejipanga na tutafanya mkutano wa viwango zaidi ya chama tawala,” amesema.
Alipoulizwa iwapo kukiukwa kwa ratiba hiyo kuna athari za kisheria, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, amesema hakuna matokeo hasi kuhusu hilo.
Amesema ratiba inabadilika kwa makubaliano kati ya tume na vyama vya siasa, hivyo wakati wowote lolote linaweza kutokea kutokana na mahitaji.
“Hata hii ratiba iliyopo sasa nadhani imebadilishwa, maana mara ya mwisho nimepitisha mabadiliko juzi. Kwa hiyo itaendelea kubadilika, na siyo lazima tarehe iliyopangwa eti chama kifanye siku hiyo hiyo,” amesema.
Lakini, amesema kama kuna mabadiliko ya ratiba, vyama vya siasa vinaomba kukutana na mkurugenzi wa uchaguzi na kujadiliana namna ya kubadilisha kulingana na inavyohitajika.