Chaumma yaahidi kuvalia njuga migogoro ya wakulima na wafugaji

Morogoro. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja ameahidi kuwa iwapo chama hicho kitaaminiwa kuunda Serikali, ndani ya siku 100 za kwanza, kitachukua hatua dhidi ya wale aliowaita mapapa wa ardhi waliomilikishwa maeneo makubwa na kusababisha migogoro kwa wananchi.

Akihutubia wananchi wa Jimbo la Kilosa mkoani Morogoro leo Jumatano Septemba 3, 2025, Devotha amesema hali ya ardhi mkoani humo imegeuka chanzo kikubwa cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa sababu maeneo makubwa yamehodhiwa na watu wachache, huku wananchi wengi wakibaki kwenye ardhi finyu isiyotosha.

“Mkoa huu umebarikiwa mabonde kila mahali, lakini leo hakuna ardhi ya kutosha. Wawekezaji wakubwa wameigeuza Morogoro shamba la bibi, maeneo makubwa yamehodhiwa na watu wachache na yaliyo salia ndio wakulima na wafugaji wanagombania,” amedai mgombea mwenza huyo.

Devotha ameongeza kuwa wakati wa uongozi wa hayati Rais John Magufuli, Serikali ilifuta umiliki wa baadhi ya wawekezaji na kuelekeza ardhi igawiwe bure kwa wananchi, lakini kwa sasa wananchi hao wanalazimika kukodishiwa maeneo hayo.

“Kote tunakoshuhudia watu wachache wakihodhi maeneo makubwa, Chaumma tukipewa ridhaa tutahakikisha yanarejeshwa kwa wananchi. Tutamshauri Rais achukue hatua ili kila mkulima na mfugaji apate ardhi ya kutosha,” amesema.

Aidha, alipokuwa akizungumza na wakulima wa mbaazi, Devotha amelalamikia tozo ya Sh450 kwa kila kilo ya zao hilo inayotozwa kwa stakabadhi ghalani, akieleza kuwa ni mfumo wa unyonyaji.

“Mkulima hajasaidiwa chochote tangu maandalizi ya shamba, ununuzi wa mbegu hadi mavuno. Serikali haijashiriki popote, hivyo haipaswi kuweka mifumo inayowaumiza wakulima,” amesema na kuahidi kuwa endapo Chaumma kitaingia madarakani, wakulima watakuwa huru kuuza mazao yao sehemu yoyote wanapotaka.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kilosa kupitia chama hicho, David Chiduo amesema jimbo hilo limebaki nyuma kimaendeleo kutokana na viongozi waliopita kukosa uchungu na wananchi.

Amesema migogoro mingi ya ardhi jimboni humo imesababishwa na watu wenye kipato kikubwa, kujimilikisha mashamba makubwa bila hata kuishi eneo hilo.

“Kuna watu hawakai Kilosa lakini wanavuna mpunga kutoka kwenye mashamba makubwa waliyoyahodhi, hali hii si sahihi na inawanyima wananchi fursa ya kutumia rasilimali zao,” amesema.