NRA yaja na ‘Mobile Campaign’ ikijiandaa kwa uzinduzi

Dar es Salaam. Baada ya kuwa nyuma ya ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa siku ya saba mfululizo, Chama cha NRA kimeamua kufanya ‘mobile campaign’ kikieleza lengo la mfumo wake huo wa kampeni ni kuwapa mbinu wagombea wake na kujiweka karibu zaidi na wananchi kabla ya uzinduzi rasmi.

Chama hicho, leo Jumatano Agosti 3, 2025 kwa mujibu wa ratiba ya INEC, kilipaswa kuendelea na kampeni zake mkoani Kigoma katika kata zote za Wilaya ya Kasulu na Buhigwe kwa mgombea wake wa urais na mgombea mwenza alipaswa kuendelea na kampeni katika Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

Katibu wa NRA, Hassan Almas ameiambia Mwananchi kwamba, wameamua kuanza kivingine kampeni zao kwa kufanya ‘mobile campaign’ ambazo tangu kuanza kwa ratiba yao Agosti 28, 2025, wameshafanya kampeni za aina hiyo katika mikoa mitatu.

“Tulianzia Dar es Salaam, kisha Kilimanjaro na leo (Septemba3) tutakuwa Pwani, tumeamua kuanza kampeni za chini chini kwa mtindo wa ‘mobile campaign’ kwa sababu mbili kubwa.

“Kwanza ni kuongea na watu physical (hana kwa hana) ili kuwaweka karibu wananchi, lakini kingine ni kuwafanya wagombea wetu kuwa aware (kuwa tayari) na kampeni, lazima tuwatengeneze, tuwapike na kuwapa mbinu kabla ya kuingia jukwaani,” amesema na kuongeza;

“Ukianza marathoni kwa spidi ni dhahiri hauwezi kumaliza, kama ukianza kwa nguvu lazima uwe na nguvu ileile hadi mwisho, sisi hatujataka hivyo.”

Kuhusu kutofanya kampeni kwenye mikoa saba kwa mujibu wa INEC, Almasi amesema katika ratiba mpya itakayotoka Oktoba, wataifidia mikoa hiyo ambayo ni Mtwara, Tanga, Ruvuma, Dar es Salaam, Mbeya, Kaskazini Pemba, Iringa, Morogoro na Kagera.

Amesema baada ya kufanya mobile campaign tangu Agosti 28, wanatarajia kuzindua rasmi kampeni zao mkoani Kigoma, Septemba 5, siku ambayo kwa mujibu wa ratiba ya INEC, inaonyesha mgombea wake wa urais atakuwa huko na mgombea mwenza, atakuwa mkoani Njombe.

“Sisi tumeamua kuzindulia kampeni zetu Kigoma Septemba 5, kesho (Septemba 4) tutakwenda Kigoma tukitokea Pwani ambako leo tunaendelea na ‘Mobile campaign’ katika wilaya za Bagamoyo na Kibaha,” amesema.

Katika Mobile Campaign ya Pwani, Almasi amesema wataanzia Msata, Chalinze, Mlandizi, Miembe saba, Mwendapole na kumalizikia Loliondo Sokoni kabla ya kufanya kikao cha ndani na baadaye kuanza safari ya kwenda Kigoma ambako kesho Septemba 4 wataendelea na Mobile Campaign kabla ya uzinduzi keshokutwa Ijumaa.

Mbali na NRA, vyama vingine vinaendelea na kampeni kwa mujibu wa ratiba ya INEC, ambayo inaonyesha leo Septemba 3, 2025 mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) atakuwa Tanga na Same mkoani Kilimanjaro, makamu wake atakuwa Morogoro, CCK watakuwa Dar es Salaam, CUF watakuwa Simiyu, UDP (Mara), Makini (Pwani) ADC (Mwanga, Kilimanjaro), NLD (Kigamboni, Dar es Salaam) na CCM, mgombea urais atakuwa mkoani Songwe mgombea mweza wake yuko mkoani Shinyanga.

Japo ADC, UPD na NLD havijaanza kampeni kama ilivyo kwa NRA, lakini Chama cha NLD kimesema kinatarajiwa kuzindua kampeni kesho Septemba 4, jijini Tanga na ADC watazindua Septemba 7 jijini Mwanza.

Tayari vyama vya CCM, Chaumma, AAFP, CUF, Demokrasia Makini na Chama cha CCK vimezindua kampeni zake kwa mujibu wa ratiba ya INEC.