Biashara ya mkaa yapaa, kuni ikiporomoka

Dar es Salaam. Katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeripoti kuwapo kwa ongezeko la fedha zinazotumika kununua mkaa kwa zaidi ya mara mbili.

Katika ripoti tofauti za uchumi wa Kanda za BoT, zinaonesha mauzo ya mkaa yaliongezeka kutoka Sh3.5 bilioni katika mwaka ulioishia Machi 2023, hadi Sh7.6 bilioni katika mwaka ulioishia Machi mwaka huu.

Hilo ni ongezeko mfululizo lililoshuhudiwa, kwani mwaka ulioishia Machi 2024, mauzo ya mkaa yaliyorekodiwa yalikuwa Sh5.96 bilioni.

Ongezeko hilo lililoonekana kupitia ripoti iliyochapishwa Agosti 25, 2025, linatajwa kuchochewa na ongezeko la watu linaloshindwa kuendana na uwezo wa kumudu gharama za nishati mbadala, ikiwamo gesi.

Hili linashuhudiwa wakati ambao Serikali inatekeleza mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa ifikapo mwaka 2034.

Hata hivyo, katika kipindi husika, mauzo ya kuni yalionekana kupungua kutoka Sh165.1 milioni mwaka ulioishia Machi 2023, hadi Sh125.9 milioni Machi 2025.

Akizungumza na Mwananchi jana, Septemba 2, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Donald Mmari amesema ongezeko la idadi ya watu ni moja ya sababu ya kuwapo kwa ongezeko hilo, wakati vyanzo mbadala vya nishati ya kupikia havijawa vingi.

“Licha ya kutokuwa vingi, gharama yake iko juu, kwa sababu wengi bado wanatumia gesi ya kupikia ya kwenye mitungi (LPG), ambayo inatokana na petroli. Sasa hii gharama yake iko juu na inategemea soko la dunia na lazima itasafirishwa,” amesema.

Dk Mmari amesema moja ya njia rahisi inayoweza kuondoa suala hilo ni kupigia chapuo matumizi ya mkaa mbadala unaotengenezwa kutokana na malighafi zisizoharibu mazingira.

Kwa sasa, utengenezaji wa mkaa mbadala upo kwa kiasi kidogo na haupatikani kwa urahisi.

“Wazalishaji hawana uwezo wa kuzalisha kwa kiwango kikubwa, hivyo ni vyema kuhakikisha wanakuwa wengi ili ufike maeneo mengi zaidi na, ikiwezekana, wawezeshwe vifaa kwa ajili ya uzalishaji,” amesema.

Amesema sababu nyingine inayofanya mauzo ya mkaa kuendelea kuongezeka ni kutokana na uwepo wa wateja, hali inayofanya wazalishaji wa mkaa unaotokana na misitu kuendelea kuzalisha kwa sababu wana soko la uhakika.

“Elimu ni muhimu, wazalishaji wa mkaa wa kawaida hawajapata fursa mbadala ya shughuli za kiuchumi, kwa sababu unakuta mtu ndiyo kazi yake miaka 20 hadi 30, wanaendelea kuzalisha,” amesema na kuongeza:

“Siku tukipigia chapuo mkaa mbadala na wengi wakautumia, hawa wanaokata miti wakikosa wateja wataacha kukata na kuhamia katika njia nyingine ya uzalishaji ili wajipatie kipato.”

Vilevile, ametaka kuangaliwa namna uzalishaji wa gesi ya kupikia unavyofanyika, ili kuwezesha gharama kushuka, kwani zilizopo zinawaelemea wateja.

Amesema kwa gharama kushuka, ni wazi kundi la watu wanaoweza kuzimudu litaongezeka.

Gharama ni changamoto kwa watu wengi, ambao huhitaji kununua kwa kadri ya matumizi (mfano wa Luku katika umeme), ili kila mmoja aweze kumudu.

Sabrina Mashaka, muuzaji wa gesi ya kupikia, amesema watu wengi wanaotumia mkaa wamekuwa na nafasi ya kununua kwa kiasi kidogo cha fedha, tofauti na wanaotumia gesi wanaohitaji fedha nyingi ya pamoja.

“Mtu akiwa na Sh1,500 au Sh2,000 anapata mkaa na anapika kutwa nzima, lakini gesi huwezi kupata. Kuna hii njia nilisikia inafanya kazi katika baadhi ya maeneo, nadhani Serikali ingeweka nguvu zaidi kuhakikisha inafika maeneo mbalimbali,” amesema.

Usambazaji wa gesi asilia ni jambo alilotaka liangaliwe, kwani linaweza kusaidia kushusha gharama na kufanya watu wengi kuhama kutoka kutumia nishati chafu.

Suala la bei kubwa limeanza kufanyiwa kazi na Serikali, kwani Februari 27, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza Serikali imekuja na mkakati wa kutoa ruzuku kwa wanaochakata gesi kuwa nishati na kuweka mazingira rafiki yatakayochochea ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli hiyo.

Ruzuku hiyo, kwa mujibu wa Rais Samia, inahusisha kugharimia asilimia 50 ya bei ya mtungi wa gesi, huku mwananchi akichangia asilimia 50 kwa maeneo ya vijijini.

Kwa upande wa mijini, alisema Serikali inatoa ruzuku ya asilimia 20, huku mwananchi akichangia asilimia 80 ya bei ya mtungi huo kwa mujibu wa sheria ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Samia alieleza mikakati hiyo baada ya kuzindua awamu ya pili ya mradi wa ugawaji wa mitungi 452,000 ya gesi kwa wananchi, alipokuwa ziarani Muheza, mkoani Tanga.

Baadaye Mei mwaka huu, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, alisema tayari Serikali imetoa ruzuku ya asilimia 20 hadi 50 kwenye mitungi ya gesi ya kupikia takribani 452,445 kwa watumiaji wa mwisho, ikiwa ni jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Alisema hayo akiwa bungeni jijini Dodoma, Mei 23, 2025, akijibu swali la mbunge wa viti maalumu, Grace Tendega, aliyetaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa muda mfupi wa kuhakikisha wananchi wa vijijini wanatumia nishati safi ya kupikia badala ya kuni na mkaa.

“Serikali, kupitia Rea, pia itasambaza majiko banifu 200,000 yenye bei ya punguzo la hadi asilimia 75 na kuwezesha ufungaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika taasisi za umma zinazohudumia watu zaidi ya 100,” alisema Kapinga.

Ili kupunguza gharama za gesi kwa wananchi, Agosti 2025, Serikali ilisema iko mbioni kuja na mpango wa uagizaji wa gesi ya kupikia kwa pamoja kupitia Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) baada ya miundombinu wezeshi kukamilika kujengwa.

Mfumo huo unatajwa kuwa utasaidia kupunguza bei ya gesi ya kupikia, jambo litakalowawezesha wananchi kumudu gharama yake na kuachana na matumizi ya nishati chafu.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa PBPA, Erasto Simon, alipozungumzia mafanikio ya ofisi yake katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina uliofanyika Agosti 7, 2025.

Uamuzi huo unakuja wakati ambao uagizaji wa mafuta kwa pamoja umeleta matokeo chanya, ikiwamo kuongeza kiwango cha mafuta kinachopokewa nchini, kuvutia nchi jirani kuagiza mafuta kupitia Tanzania na kuokoa kiwango cha mafuta kilichokuwa kikipotea awali.

Simon alisema miongoni mwa sababu za gesi ya kupikia kutoagizwa kwa kutumia mfumo wa pamoja ni miundombinu iliyopo kuruhusu meli ndogo pekee kuingia.

“Unapoingia mfumo kama huu, unalazimika kukusanya mahitaji makubwa ili kuagiza mzigo mkubwa, hivyo kinachofanyika sasa ni kujenga miundombinu ya meli kushusha mizigo na hifadhi kubwa. Hayo yatakapokamilika, gesi ya kupikia itaingizwa katika mfumo wa wakala wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja,” alisema.

Akielezea baadhi ya kazi zinazofanyika, alisema ni kujenga miundombinu ya ushushaji gesi ya kupikia, kujenga sehemu ambazo meli kubwa zitakaa na kutanua mabomba, ili yasukume mzigo mkubwa kwenda kwenye maghala.

“Miongoni mwa faida za kuagiza mzigo wa gesi ya kupikia kwa pamoja maana yake bei itakuwa ya chini, kwani gharama itapungua na wananchi wataweza kunufaika,” alisema.