Wahamiaji haramu 10,960 wakamatwa wakiingia nchini, RC Mwassa akerwa

Bukoba. Idara ya uhamiaji mkoani Kagera imefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 10,960 wakiingia nchini kinyemela kuanzia Januari hadi Septemba 2025.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Septemba 3, 2025 ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Mrakibu mwandamizi, Eleneus Kasimbazi amesema idara hiyo ya uhamiaji Mkoa wa Kagera kupitia doria mbalimbali walizozifanya kwenye maeneo muhimu ya mipaka ya nchi jirani na Tanzania za Burundi, Rwanda na Uganda wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwakamata wahamiaji haramu.

Kasimbazi amesema kati ya hao 10,960 wahamiaji 10,130 waliondolewa nchini na 576 wamefikishwa mahakamani.

Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa tatizo la wimbi la wahamiaji haramu lipo kwa ukubwa kwa nchi jirani ya Burundi ambapo kuanzia Januari mpaka Septemba 2025 wamekamatawa watu 9,056 wakiingia nchini bila vibali.

“Tatizo lipo kwa wahamiaji kutoka Burundi kwa wingi na mataifa mengine kama Rwanda tumekamata  523 pamoja na Uganda tumekamata 481. Raia kutoka Congo 53, Kenya wanne, Sudani tisa, Sudan Kusini mmoja, Pakistan wawili India mmoja na wote sisi kama Idara ya uhamiaji tumewachukulia hatua za kisheria,” amesema.

Mkuu wa mkoa Kagera,Fatma Mwassa akikabidhi gari aina ya Fortuner kwa Idara ya uhamiaji mkoa kutoka Mamlaka ya mapato Tanzania TRA ili kupambana na wahamiaji haramu.

Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwassa kupitia takwimu hizo za wimbi la wahamiaji haramu amekabidhi gari aina ya Fortuner kwa Idara ya Uhamiaji mkoa huo walilopewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuongeza ngumvu na kasi ya utendaji kazi.

Mwassa amesema hayo wakati akikabidhi gari hilo kwenye ofisi za mkoa kwamba pamoja na jitihada zote za kufanya doria kuwakamata wahamiaji haramu, amekili kuwa tatizo bado kubwa.

“Wamerudishwa zaidi ya 9,000 na wegine 500 kupelekwa mahakamani ila tatizo bado ni kubwa sana tumegundua wakihukumiwa kufungwa bado Serikali imekuwa ikiingia gharama za kuwatunza, hivyo kwa sasa tutawakamata na kuwarudisha kwao.

Mkuu wa mkoa Kagera,Fatma Mwassa akizungumzia kuhusu wahamiaji haramu.

“Hii haijakaa sawa tunaendelea na juhudi za kuwapunguza kwa mwezi Januari walikamatwa 502, Februari 988, Machi 785, Aprili 1,306, Mei 986, Juni 2,006, Julai 2,269, Agosti 2,118 hii namba ni kubwa yaani haiwezekani kwa mwezi watu wanajifungasha kutoka nchi yao kwenda nchi ya wengine  kuhamia bila makubaliano haiwezekani,” amesema.

Kwa upande wa meneja wa TRA Mkoa wa  Kagera, Castro John amsema wao kama mamlaka wameona kutoa gari hilo ni muhimu kuongeza nguvu ya kuendelea kudhibiti uhamiaji haramu ili kuwezesha nchi kukusanya mapato ambayo yangepotea bila sababu.