Tunduma. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kumaliza tatizo la msongamano wa magari katika mji wa Tunduma kupitia mradi wa upanuzi wa barabara ya Tanzam.
Samia amebainisha hayo leo, Septemba 3, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni alioufanya mjini Tunduma, mkoani Songwe, ikiwa ni siku ya kwanza ya kampeni zake katika mkoa huo.
Hata hivyo, awali Mwananchi ilizungumza na wananchi wa mji huo wa Tunduma kwa nyakati tofauti, wakitaja mambo wanayotaka yatekelezwe na mgombea atakayefanikiwa kuingia madarakani.

Miongoni mwa mambo hayo waliyoyataja ni kuwajengea barabara za ndani za lami ili kupunguza msongamano wa malori na vumbi, kuondoa utitiri wa kodi pamoja na kuwapatia vitambulisho vya Taifa.
Mkazi wa Tunduma, Eliud Mwashitete, amesema licha ya kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kwenye sekta za elimu na afya, bado wanakabiliwa na kero ya barabara mbovu na msongamano wa malori.
“Tunaomba pia barabara yetu kuu ya Tunduma-Mbeya ipanuliwe, kwa sababu imekuwa ikisababisha msongamano wa magari, hasa malori yanayokwenda Zambia,” amesema Mwashitete.
Mji wa Tunduma unakabiliwa na changamoto ya msongamano wa magari unaosababishwa na malori ya mizigo inayoelekea nchini Zambia, jambo ambalo limekuwa likitatiza shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii katika mji huo maarufu kwa biashara.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Samia amebainisha mikakati ya kumaliza foleni kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Tunduma – Igawa, yenye urefu wa kilomita 75.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, mgombea huyo wa urais wa CCM ameahidi kukamilisha ujenzi wa barabara ya Tanzam ya njia nne, akisema huo pia ni mwarobaini wa kumaliza tatizo hilo linalokwamisha shughuli za maendeleo kwa wananchi.
“Kazi ya ujenzi wa barabara hii imeanza, tunakwenda kuimaliza kabisa,” amesema Samia, huku maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza wakimshangilia.
Amesema Serikali imeanza kukarabati reli ya Tazara ili kuiongezea uwezo wa kusafirisha mizigo kwenda Zambia, jambo litakalosaidia kupunguza malori ya mizigo katika mji wa Tunduma.
“Tunakwenda kukamilisha ujenzi wa bandari kavu yenye ukubwa wa mita za mraba 1,800. Tunatarajia kuongeza maegesho ya malori ili yasipaki barabarani, bali yawe na eneo maalumu,” amesema.
Akizungumzia maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, Samia amesema yamefanyika kwa kiwango kikubwa, na sasa kiwango cha mizigo kinachopokelewa kimeongezeka kutoka tani milioni 15.8 hadi kufikia tani milioni 28 zinazopokelewa sasa.
Amesema kiwango cha mzigo kinachopita Tunduma pia kimeongezeka kutoka tani milioni 3.7 hadi tani milioni tisa, jambo linalosababisha msongamano wa malori katika mji huo unaopakana na Zambia.
Kuhusu umeme, amesema watajenga kituo cha kupoza umeme cha kilovolti 730, na kilovolti 400 zitatumika Tunduma na Rukwa, huku kilovolti 330 kikiuzwa nchi jirani ya Zambia.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo amesema Serikali inafanya mazungumzo na mamlaka za Zambia ili kuzishawishi pia kufanya kazi kwa saa 24, kama ilivyo upande wa Tanzania.

Wabunge waeleza mafanikio
Mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Tunduma, David Silinde, amesema Tunduma wamepokea Sh28 bilioni kwa ajili ya miradi ya elimu msingi na sekondari, na tayari wamejenga shule saba za ghorofa.
“Tumejenga shule inaitwa Dk Samia, imejengwa kwa thamani ya Sh6 bilioni, haijawahi kutokea. Huku Tunduma tunajenga shule za maghorofa tu,” amesema Silinde.
Kwenye sekta ya afya, amesema wakati Samia anaingia madarakani, Tunduma ilikuwa na kituo kimoja cha afya, lakini sasa vituo viko vitano, na kufanya mji huo kuwa na vituo sita vya afya vyote vinavyofanya kazi.
Ameongeza kuwa wakati anaingia madarakani walikuwa na kilomita 1.7 ya barabara, lakini Samia alipoingia madarakani miaka minne iliyopita, zimeshajengwa kilomita 10.1 za barabara ya lami.

Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Daniel Chongolo, ambaye pia ni mgombea ubunge wa chama hicho katika Jimbo la Makambako, ameshiriki mkutano huo wa kampeni, huku akieleza miradi ya maendeleo iliyotekelezwa.
Chongolo, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, amesema kabla ya mwaka 2021 wakulima hawakuwa na ruzuku ya pembejeo za kilimo, lakini alipoingia madarakani alianza kutoa ruzuku hiyo ili wananchi wasibebe mzigo wa gharama hizo.
“Matokeo yake tumeyaona, ukanda huu unaongoza kwa uzalishaji mkubwa wa mahindi. Wakulima wamenufaika na ruzuku ya pembejeo, sasa wameongeza uzalishaji,” amesema Chongolo.
Ameongeza kwamba mkoa wa Songwe umefunguliwa kwa barabara, walipokea Sh70 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara, ikiwemo ile ya Isongike – Ileje na Mlowo – Kamsamba.
“Kituo cha forodha cha Tunduma kilikuwa kinakusanya Sh130 bilioni, lakini mwaka wa fedha uliopita, ujumla ya Sh204 bilioni zimekusanywa katika kituo hicho. Umeweka mifumo ya kuwezesha ukusanyaji wa mapato,” amesema Chongolo.