Dk Nchimbi: Tutaimarisha demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari

Shinyanga. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo watasimamia vyema uhuru wa vyombo vya habari.

Pia, chama hicho kikipata ridhaa ya wananchi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kitasimamia kukuza demokrasia ili Watanzania wafanye siasa bila hofu wala mashaka.

Dk Nchimbi amesema hayo jana Jumatano, Septemba 3, 2025 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu ambapo alimwombea kura mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani.

Katibu Mkuu huyo wa zamani wa CCM ameanza kujenga hoja kuwa  wameimarisha demokrasia ndani ya chama hicho na viongozi wake wanapatikana kwa kujaza fomu na kupigiwa kura na wanachama wake.

“Chama bora cha siasa kinapimwa na muundo wake, ni chama pekee kilichojijenga kuanzia ngazi ya Taifa hadi shina,” amesema Dk Nchimbi.

Baada ya kujenga hoja hiyo amesema; “Tumedhamiria kama ambavyo tumeimarisha demokrasia ndani ya Chama cha Mapinduzi, tunataka demokrasia iedelee kuimarika na kushamiri katika nchi ili kila Mtanzania asikie, aone na atambue ana uhuru wa kufanya siasa, kwa uhuru kamili, bila vitisho na bila mashaka.”

Dk Nchimbi amesema, chama hicho tawala kitagakikisha:”Uhuru wa vyombo vya habari, unashamiri na kuneemeka, ili watu wetu  wawe na fursa ya kupata elimu na  mawazo mbalimbali kupitia vyombo vya habari.”

Amesema katika  miaka mitano hiyo watahakikisha amani, umoja na mshikamano unadumishwa.

Mkazi wa Maganzo, Samson Msafiri akizungumzia ahadi hiyo amesema kama wanachokiahidi kitatekelezwa itakuwa jambo zuri kwani watu wanapaswa kuwa huru kufanya mambo yao.

“Kuna mengi huko tunasikia mitandaoni, mara hivi mara vile, yule kabanwa, waandishi sijui nini, sasa kama wanasema wataweka uhuru itakuwa vizuri, ujue watu wanataka kuona demokrasia kubwa kwa vyama vyote na watu waishi kwa amani,” amesema Msafiri.

Awali, katika mkutano huo kada wa CCM, Mchungaji, Peter Msingwa amesema Chama cha Mapinduzi kinajulikana kwa sera, malengo na falsafa yake, yale yalioachwa na mtangulizi wake (Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli) Rais Samia Suluhu Hassan ameyakamilisha na anaendelea kukamilisha ikiwamo miradi mbalimbali.

“Yale aliyoacha mtangulizi wa Rais Samia yeye amekamilisha na anaendelea kukamilisha ikiwa ni pamoja na daraja la JPM Busisi, tumpe kura zetu akatekeleze Ilani ya chama, pamoja wabunge na madiwani wa CCM wakashughulikie shida zetu na kutafuta suluhu na faida ya kuwatumikia Watanzania,” amesema Msigwa.

Dk Nchimbi ataendelea kuzisaka kura Shinyanga akiwa Wilaya ya Kahama ambapo atafanya mikutano mitatu leo Alhamisi, Septemba 4, 2025 maeneo ya Isaka, Kagongwa na kumaliza Ushetu.

Kwa upande wa mgombea urais,  Samia Suluhu Hassan, leo Alhamisi ataebdelea kunadi sera mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambapo atakuwa  mkoani Mbeya katika majimbo ya Mbalizi na Mbeya Vijijini.

Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025 zilianza Agosti 28 na zitahitimishwa Oktoba 28 na kesho yake Jumatano ya Oktoba 29, 2025 itakuwa siku ya kupiga kura kuwachagua madiwani, wabunge na Rais ambao watakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2030.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari mbalimbali.