Dar es Salaam. Ni imani kuwa, mambo yanayohusu vijana yakizungumzwa na vijana wenyewe hueleweka zaidi.
Ndivyo anavyoamini Abdulkadir Thabit Massa, hivyo kuwekeza muda wake mwingi kuandika kazi za fasihi zinazohusu vijana.
Licha ya kuwapo sera na miongozo inayohusu kundi hilo, bado wenyewe wanapaswa kusimama kueleza wanayokabiliana nayo na kushirikishana fursa na mbinu za kutatua changamoto zinazowakabili.
Massa, mwandishi wa vitabu vya fasihi amendika ‘Hatima Iliyofutika’ na ‘Katika Kivuli cha Ulimbukeni’ ambavyo vinapatikana kwenye jukwaa la kidijitali la MwanaClick.

Akiwa mwanafasihi, ametumia sanaa ya uandishi kuzungumza na vijana kuwasilisha yanayowakabili kupitia vitabu hivyo ambavyo amevisambaza katika jukwaa linalofikiwa zaidi na hadhira yake.
“Kuna sera nyingi zinazohusu vijana lakini hiyo haitoshi, ni lazima sisi pia tuweke nguvu yetu kuhakikisha tunafunzana wenyewe kwa wenyewe kupitia njia zetu kama nilivyofanya mimi,” amesema.
“Mambo ya vijana yangeweza kuandikwa na mzee au mtu mzima kwa sababu yeye ameshapita kwenye hatua hizo, lakini sisi wenyewe tuko wapi? Kwa nini tusitengeneze uwanja wa kufanya majadiliano ya kifikra pamoja?” amehoji.
Amewataka vijana kujipambanua na kujitengenezea kesho iliyo bora na siyo kupoteza muda mwingi kufanya mambo yasiyokuwa na tija.
“Ujana upo lakini tusijisahau, nawasihi vijana wenzangu tusisahau kutenga muda kwa ajili ya kutengeneza mazingira mazuri ya kesho yetu na ya vizazi vyetu kupitia vitabu na tutapata fikra nje ya darasa,” amesema.

Amesema alitamani kuona vijana wengi wanapata fursa ya kusoma vitabu vyake na njia pekee ya kufanya hivyo kwa sasa ni kupitia majukwaa ya kidijitali.
“Siku hizi si watu wengi wanapata fursa ya kusoma maudhui yaliyo katika nakala ngumu, hususani vijana. Muda mwingi wapo kwenye simu. Pia nilitaka vitabu vyangu vifike kote duniani, ndipo nikaona ni vyema niwasilishe wazo langu Mwananchi Communications Ltd (MCL),” amesema na kuongeza:
“Nashukuru nilipokewa vizuri, walipitia maudhui ya vitabu na walipojiridhisha yako sawa vikapandishwa kwenye Mwanaclick. Kupitia jukwaa hilo mtu akiwa mahali popote duniani anaweza kusoma vitabu vyangu.”
Meneja Mradi wa MwanaClick, Amir Simbano amesema MCL imetoa jukwaa hilo kwa watunzi wa vitabu kuweka kazi zao bila gharama yoyote lengo likiwa kuwafikia watu wengi zaidi.
“Tulianzisha MwanaClick tukifahamu si watu wote wanaweza kupata nakala ngumu za magazeti, tukaona tuwe na jukwaa ambalo tunaweza kuweka magazeti mtandaoni. Hatukuishia hapo, tukaweka nafasi kwa kazi nyingine vikiwamo vitabu, majarida, picha, video na sauti,” amesema.
Simbano amesema: “Massa ameitumia fursa hiyo na vitabu vyake watu wananunua kupitia Mwanaclick, tunawakaribisha waandishi wengine na watunzi wa kazi za sanaa wazilete, jukwaa hili ni kwa ajili yao.”

Kuhusu uandishi wa vitabu
Massa, mwanafunzi wa shahada ya ufamasia katika Chuo Kikuu cha Selguk, nchini Uturuki amesema shauku yake katika uandishi ilianza akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kibaha.
Anasema alianza kuandika hadithi na kuzibandika kwenye mbao za matangazo, jambo lililowavutia wanafunzi, ndipo akaona kuna anachoweza kufanya.
Anasema alipomaliza kidato cha nne alifanya vizuri kwenye mchepuo wa sayansi, lakini aliamini anaweza kutumia muda wa ziada kwa kazi za fasihi.
Mwaka 2020 alipata wazo la kuandika kitabu cha kwanza baada ya kukusanya visa na mikasa vilivyotokea kipindi hicho ambacho dunia ilipa janga la Uviko-19.
“Mambo mengi yalibadilika kipindi kile, nikatamani kuyaweka kwenye maandishi ili hata vizazi vijavyo vije kusoma kilichojiri. Nilitengeneza kisa cha msichana aliyepambana katikati ya janga hilo baada ya kufukuzwa nyumbani kwako,” anasema.
Massa anaeleza: “Vuta picha wakati dunia inapambana na janga la Uviko kuna binti wa sekondari anafukuzwa nyumbani, hivyo anaingia mtaani akiwa mwenyewe, mambo aliyopitia kuna wakati alikata tamaa. Simulizi hii imebebwa kwenye kitabu cha Hatima Iliyofutika.”