Babati. Wadau wa kilimo nchini watanufaika na teknolojia ya ndege nyuki shambani, ikiwamo kunyunyizia dawa, kupanda mbegu, kupima maeneo na kusafirisha mazao, hivyo kuongeza tija katika kilimo.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni za Mati Group, David Mulokozi akizungumza mjini Babati mkoani Manyara, Septemba 4 mwaka 2025 amesema shughuli za kilimo kupitia ndege nyuki zitalenga kuongeza tija, kupunguza gharama na kurahisisha kazi kwa wakulima na taasisi mbalimbali nchini.
Mulokozi amesema kampuni hiyo imewekeza katika teknolojia ya ndege nyuki zitakazotumika kunyunyizia dawa shambani, kupima maeneo, kupanda mbegu, kusafirisha mizigo na katika ukaguzi.

Amesema ndege hizo zilizotengenezwa nchini zitauzwa kuanzia Sh17 milioni kulingana na mahitaji ya mteja. Amesema gharama hiyo wakulima wataweza kumudu kulinganisha na uagizaji bidhaa hizo nje ya nchi.
“Tunaendelea na mazungumzo na benki ziweze kuwapatia wakulima mikopo kuwawezesha kununua ndege hizi ili kuimarisha shughuli za kilimo,” amesema.
Amesema uzalishaji wa ndege nyuki nchini utatoa ajira kwa wahandisi wa Kitanzania, huku wachache kutoka nje wakihusishwa katika programu za mafunzo na uhamishaji wa teknolojia.
“Tumeona changamoto inayowakabili wakulima hasa kwenye unyunyiziaji dawa, jambo linalopoteza muda na kuhatarisha afya zao, kwa drone (ndege nyuki) hizi, ekari moja inaweza kunyunyiziwa dawa ndani ya dakika saba tu,” amesema.
Godamen Merinyo, Ofisa ushirika kutoka ofisi ya mrajisi msaidizi Mkoa wa Manyara, amesema teknolojia hiyo ni mkombozi kwa wakulima, hususani katika mazao kama mbaazi ambayo mara nyingi hukua kwa urefu na kufanya upuliziaji dawa kuwa mgumu na wa gharama kubwa.
“Hii itasaidia kuongeza uzalishaji kwa gharama nafuu na kuimarisha vyama vya ushirika, sisi kama viongozi wa ushirika tutaanza kutoa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia hii,” amesema.

Mkurugenzi wa makampuni ya Mati Group David Mulokozi (kulia) akipongezwa na mkuu wa wilaya ya Kiteto, Remidius Mwema, kwenye uzinduzi wa ndege nyuki zitakazotumika kwa kilimo mjini Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo
Ofisa Kilimo Mkoa wa Manyara, Paulo Eugine amesema ndege nyuki hizo zitasaidia kuwalinda wakulima dhidi ya madhara ya kiafya yaliyokuwa yanawapata kutokana na kutumia pampu za mgongoni.
“Sasa mkulima ataweza kutumia kitendea mbali (remote control) bila kuingiwa na sumu, jambo linaloimarisha usalama na afya zao,” amesema.
Amesema tekmolojia hiyo inatarajiwa kuwa chachu ya mapinduzi ya kilimo nchini na kuunga mkono jitihada za Serikali katika matumizi ya teknolojia za kisasa kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo.
Mkulima wilayani Babati, Abdalah Ramadhan amesema uwepo wa ndege nyuki hizo utaongeza tija kwa wakulima wa eneo hilo.