Profesa Muhongo ampigia debe Samia akitaja yaliyofanywa na Serikali Musoma Vijijini

Musoma. Mgombea ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wakazi wa jimbo hilo kumpigia kura za ushindi kwa asilimia 95 mgombea urais kupitia chama hicho, Samia Suluhu Hassan kwa maelezo kuwa sababu ya kufanya hivyo wanayo.

Profesa Muhongo ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 4, 2025 katika Kijiji cha Kiriba wakati wa uzinduzi wa kampeni katika jimbo hilo.

Amesema Serikali ya CCM kupitia kwa Samia, inayafahamu mahitaji ya wakazi wa jimbo hilo na hivyo katika kipindi kilichopita imeleta maendeleo makubwa katika vijiji vyote 68 vilivyopo jimboni humo.


Amesema kitendo cha chama hicho kukosa wapinzani katika kata 11 ni ishara tosha kuwa wakazi wa jimbo hilo wanakikubali chama hicho na wagombea wake ngazi ya udiwani hadi urais.

Amesema huduma zote za kijamii zimesogezwa karibu na wananchi na kwamba mpango wa kusogeza na kuboresha zaidi huduma hizo hasa katika ngazi ya vitongoji upo na unaweza kutekelezwa na chama hicho pekee

Ametolea mfano wa huduma za maji, katika vijiji vyote 68 vya jimbo hilo kuna miradi ya maji safi na salama huku mpango uliopo ni kuhakikisha kuwa vitongoji vyote 374 vya jimbo hilo vinapata miradi ya maji.

“Kwenye umeme sasa ndio usiseme kwani vijiji vyetu 68 vyote vina miundombinu ya umeme na hadi kufika Desemba mwaka huu vitongoji 100 pekee ndivyo vitakuwa havijafikiwa na umeme lakini habari njema ni kwamba kati ya hivyo vitongoji 100, kuna vitongoji 50 ambavyo vimeingizwa kwenye bajeti ya mwaka huu hii ina maana tunadaiwa vitongoji 50 tu,” amesema

Amesema katika sekta ya elimu jimbo hilo tayari limevuka sera ya kuwa na shule moja ya Sekondari kwa kila kata badala yake hivi sasa wanaendedelea na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa shule za sekondari katika kila kijiji huku akisema  ndani ya miaka mitano ijayo kila kijiji kitakuwa na shule ya Sekondari.


“Kwenye huduma za jamii tuko vizuri sana maana hata kwenye afya tuko vizuri tukianzia hospitali yetu ya halmashauri yenye vifaa vyote vya kisasa ikiwepo X-Ray mbili sasa nguvu tunazihamishia kwenye uchumi na hili litawezekana tukikichagua Chama cha Mapinduzi,” amesema.

Profesa Muhongo amesema kutokana na kata 18 kati ya 21 za jimbo hilo kuwa pembezoni mwa Ziwa Victoria nguvu kubwa ataielekeza kwenye ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba badala ya uvuvi wa kutegemea samaki kutoka ndani ya ziwa hilo.

Ameongeza kuwa baada ya kuanzisha miradi ya ufugaji wa vizimba mchakato wa ujenzi wa kiwanda cha kusindika samaki utaanza ili kuwa na mnyororo wa thamani kwa mazao yatakayotokana na miradi ya uvuvi wa vizimba.

“Chama cha Mapinduzi kina mipango mizuri sana na sisi wananchi wa Musoma Vijijini hilo halina ubishi kwani tayari kimeanza kutekeleza mipango yake kwa vitendo tuachane na hawa wanaotaka kufanya majaribio, tuhakikishe Rais Samia anapata kura si chini ya asilimia 95 hizo tano ziwe za wale wagonjwa watakaoshindwa kupiga kura Oktoba 29,” amesema Profesa Muhongo.

Kada wa CCM, Yohana Mirumbe amewataka wana CCM jimboni humo kushikamana na kuwa wamoja ili kutafuta kura za ushindi kwa chama hicho.

“Profesa amefanya mambo makubwa, Musoma Vijijini ya sasa sio ile ya miaka mitano iliyopita na kwa kazi aliyofanya tunatembea kifua mbele na ingekuwa ni amri yangu angekaa nyumbani akisubiri kupigiwa kura lakini lazima tutafute kura za mafiga matatu,” amesema Mirumbe.

Amesema umoja na mshikamno wa wana CCM matika jimbo hilo utasababisha chama hicho kushinda kwenye kata zote 21 pamoja na kura nyingi za ubunge na urais.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Vijijini,  Denis Ekwabi amesema lengo la chama chochote cha siasa ni kushika dola hivyo wamejipanga kuhakikisha wanashinda katika kata zote 21, nafasi ya ubunge pamoja na kura nyingi za urais kwa Samia.

“Tumejipanga kuchukua kata zote 21 ikiwepo Kata ya Bwasi ambayo imekuwa upinzani kwa miaka 10 sasa, wagombea wetu wote wana uwezo mzuri kujenga hoja na kusimamia hoja zao kwa manufaa ya jimbo letu,” amesema.

Mbunge Mteule wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Ghati Chomete amewaomba wakazi wa Jimbo la Musoma Vijijini kukupigia kura chama chake ili kiweze kuwaletea maendeleo kama ambavyo ilikiwshaanza.

“Bahati nzuri mgombea ubunge wetu Profesa Muhongo alipitisha bajeti ya serikali mwezi wa saba sasa tusifanye kosa tumpe kura za zote ili akasimamie utekelezaji wa bajeti hiyo ili fedha zote zilizotengwa zije kwenye jimbo kwa ajili ya maendeleo yetu,” amesema.