BADO mawazo ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024 hayajaisha kichwani japo mashindano yamemalizika na Morocco imechuka ubigwa.
Hayahusu sana kisa timu yetu ya taifa ‘Taifa Stars’ iliishia robo fainali maana timu iliyotutoa ndio ilimaliza ikiwa kinara wa mashindano hayo na ni taifa kubwa hasa.
Namba ndogo ya mashabiki ambao walikuwa wanaingia viwanjani kutazama mechi za mashindano hayo kwa hapa Tanzania ndiyo inayotufanya tuwe na mawazo sana hapa kijiweni kwani limeenda tofauti na matarajio.
Bado tunaumia kwa sababu Tanzania tulishaaminisha Afrika na dunia kijumla sisi ni nchi ya kisoka na mashabiki hawana mbambamba katika uingiaji wa uwanjani kwenda kutazama mechi.
Kwa kutoingia maana yake tunawapa watu taswira ya tofauti kuwa yale yaliyokuwa yanafanyika nyuma tulikuwa tunabahatisha ama yalitokea kwa sababu ya mihemko na siyo kwamba sisi ni watu wa mpira.
Jambo la pili ni tunajiweka katika hatari ya kupewa mechi ya ufunguzi au fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, mashindano ambayo tutayaandaa tena kwa pamoja kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Sasa leo hii ni Septemba 2025 tumebakiza zaidi ya mwaka mmoja na nusu kabla ya kuandaa mashindano hayo ambayo ni makubwa zaidi kwa timu za taifa Afrika.
Tusione na kudhani muda huu wa takribani mwaka na nusu uliobakia kabla ya AFCON 2027 ni mrefu na tukajisahau bali tunatakiwa tuanze sasa maandalizi ili yale yaliyotokea katika CHAN 2O24 yasijirudie.
AFCON 2027 tuitumie kurudisha heshima yetu kama taifa la kimpira ambayo iliyumba katika CHAN 2024 badala ya kuiporomosha.