Pamba yazifuata mechi tatu Kenya

KIKOSI cha Pamba Jiji kinaondoka nchini leo Ijumaa kwenda Kenya kwa ajili ya kucheza mechi tatu za kirafiki za kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2025-26.

Kwa mujibu wa ratiba ya klabu hiyo inayonolewa na kocha Mkenya, Francis Baraza ni kwamba kesho Jumamosi itaanza kutesti mitambo dhidi ya Mara Sugar, ikiwa ni mechi ya kwanza ya kirafiki kujiweka tayari kwa msimu mpya wa ligi, huku akiweka wazi wachezaji wa timu hiyo wapo kamili.

“Kesho (leo) Ijumaa timu inatoka Mwanza kwenda Kisii na Jumamosi tutakuwa na mechi ya kirafiki ya kwanza itakayotoa picha ya utimamu wa mwili kwa wachezaji kwa dakika 90,” alisema Baraza na kuongeza;

“Jumapili tutacheza dhidi ya Shabana na mechi ya mwisho taarifa itatolewa ni lini itachezwa lakini naamini mechi hizo mbili zitatoa picha ni namna gani tunaanza msimu wa Ligi Kuu.”

Baraza alisema timu yake ipo tayari kwa ushindani na matarajio yake ni makubwa kuona timu hiyo inaonyesha ushindani wa kimbinu na ubora wa mchezaji mmoja mmoja.

Kocha huyo aliyetua hivi karibuni akipokea mikoba ya Fred Felix ‘Minziro’, alisema wachezaji wanaendelea kuzoea mifumo na mbinu zake kutokana na kuanza msimu na timu hiyo.

“Kuna wachezaji wapya na mimi ndio kwanza nimejiunga na timu msimu huu hivyo naamini kila mchezaji anahitaji kuwa na usahihi wa kusikiliza na kufanyia kazi mbinu ambazo tumekuwa tukipeana kwenye uwanja wa mazoezi.”