Shinyanga. Bila shaka umewahi kusikia kuhusu udukuzi mtandao ambao mara nyingi umekuwa ikihusishwa na mifumo ya intaneti kufika data ambazo mwenyewe hakutaka zifikiwe na mtu mwingine.
Na pengine utakuwa umesikia kuhusu hatari ya kutumia WiFi za bure ambazo hazina ulinzi (unencrypted WiFi) na namna zinavyogeuka kuwa mawindo ya wadukuzi wenye nia tofauti.
Ukiachana na hiyo, sasa mbinu za udukuzi wa taarifa za watu zinazidi kuchukua sura mpya kila kukicha na mojawapo ikihusisha waya maarufu wa USB, ambao unatumiwa kuchajia simu wakati mwingine kuhamisha taarifa (data transfer).
Japokuwa wizi au upekuzi kwa kutumia USB haufahamiki sana, unashauriwa unapokuwa maeneo ya umma jitahidi kutumia chaja yako binafsi au power bank kama kuna ulazima wa kuchaji simu yako.

Watafiti kutoka Graz University of Technology, Austria wamebaini mbinu hiyo ya udukuzi inayojulikana kama ChoiceJacking.
Hii ni pale ambapo ‘USB charger’ inakubali yenyewe chaguo la “data transfer” wakati mwingine bila idhini ya mmiliki wa simu, hivyo kuhamisha taarifa zako.
Ingawa zipo baadhi ya simu kama Apple: iOS/iPadOS 18.4 na Android kuanzia 15 ambazo huhitaji uthibitisho wa alama za vidole au nywila kabla ya kuruhusu “data transfer.”
Kwa mujibu wa ripoti ya taarifa za ulinzi binafsi duniani takribani nchi 144 zimepitisha sheria za ulinzi wa data binafsi, zikihusisha watu bilioni 6.64, sawa na asilimia 82 ya watu duniani na karibu asilimia 83 ya idadi hiyo iko chini ya sheria za ulinzi wa data.
Mtaalamu masuala ya usalama mtandaoni kutoka JamiiAfrika, Emmanuel Mkojera anasema athari anazoweza kukumbana nazo mtu kutokana na kutumia mfumo wa kuchaji simu kwa kutumia USB pekee, ni pamoja na udukuzi huo wa taarifa binafsi.
“Kama hamna ulazima sana wa mtu kuchaji simu maeneo ya umma kwa kutumia waya wa USB, ni bora asichaji kwa sababu mbali na kuchaji, USB hutumika kuhamisha mafaili ya mtu kutoka kwenye kifaa kimoja hadi kingine mfano simu, kompyuta mpakato” ameeleza Mkojera.
“Mara nyingi taarifa za watu binafsi husambaa kwa namna, hivyo mtu anachukua taarifa zako bila kujua na kuzitumia kwa namna isiyofaa kama kulaghai watu wengine,” ameongeza Mkojera.
Mtaalamu wa teknolojia, Francis Nyonzo yeye anasema katika mfumo wa simu zetu ukiweka USB waya inauliza moja kwa moja kama mtu anaruhusu kuhamisha mafaili.
Hivyo, mtu anatakiwa kuweka simu katika mfumo huu na kama mfumo unaruhusu moja kwa moja kuhamisha mafaili bila kuuliza, hapo ndipo taarifa binafsi zinaweza kuchukuliwa bila kujua.
“Wizi huu unafanyika kupitia USB pale ambapo simu inaruhusu kuhamisha mafaili moja kwa moja bila kuuliza, ndio maana unakuta watu wanatumia ‘power bank’ kama hatua ya kujikinga kuliko kuchaji maeneo ambayo yana mwingiliano wa watu,” amesema Nyonzo.
Pia ameongeza kuwa, “kwa simu za zamani hakukuwa na mfumo wa simu kuuliza kama inaruhusu kuhamisha mafaili, wizi wa taarifa binafsi ulifanyika sana na baada ya teknolojia kukua mfumo huu ukaongezwa kwenye simu kudhibiti udukuzi huu” ameongeza Nyonzo.
Aidha, amesema kuwa uelewa watu juu wa wizi huu hasa kwa Tanzania bado uko chini sana.
“Watu wengi hawana uelewa, yawezekena ukiona mtu anatumia ‘power bank’ wanashangaa lakini hiyo haijaunganishwa na kitu chochote na Afrika zaidi ya asilimia 70 vifaa vyetu vya elektroniki viko hatarini, ndio maana watu wanaonunua software ni wa kutafuta sana,” amesema Nyonzo.
Baadhi ya watumiaji wa mfumo wa kuchajia simu katika maeneo ya umma wamekuwa na uelewa tofauti juu ya hali hiyo.
Katika hoja hiyo Aneth Chamba anaeleza: “Binafsi sijui kama kuna madhara, ninachokiona ni faida kwa watumiaji wa mabasi, treni au wanaosafiri kwa ndege huwa hii suluhisho bora katika dharura, pengine mtu anapokwenda ni mgeni alafu simu imezima anaweza kuchaji kutumia USB,” amesema Aneth.
Robert Nnko ameeleza kuwa, “kwa uelewa nilionao kuchaji maeneo ya umma kwa kutumia USB kunachangia kukosekana usalama wa taarifa binafsi kwa sababu unapochaji pale hujui nyuma yake wameunganisha nini, japo sijui wanafanyaj, wabobezi wanajua” ameeleza Nnko.
Jambo muhimu kwa watumiaji
Mkojera ameeleza kitu pekee mtu anatakiwa kufanya ni kukagua mpangilio wa mfumo wa simu yake anapotumia USB hasa katika maeneo ya umma kwa sababu haitakiwa kuamini chochote unachotumia kwenye kifaa chako.
“Kama mtu anatumia waya wa USB pekee katika kuchaji anatakiwa kuangalia simu kama inaruhusu kuchaji tu au pia kuhamisha mafaili kuepuka kupekuliwa taarifa binafsi, pia tunashauri ni vizuri mtu akatumia kichwa cha chaji wakati wa kuchaji ili kuwa salama zaidi,” ameeleza Mkojera.
Unapaswa kutumia chaja yako binafsi au power bank kama kuna ulazima. Tumia USB data blocker, kifaa kinachoruhusu umeme tu kupita bila data.
Tumia waya wa kuchaji pekee hakikisha kwanza haichukui data kwenye kompyuta unayoamini.
(Update) Huisha simu yako hadi toleo jipya la iOS au Android.
Ukilazimika kuchaji kwenye kituo cha umma, chagua “charging only” na usikubali chaguo lolote la “data transfer.”
Hata hivyo mashambulio ya ChoiceJacking bado hayajaripotiwa sana duniani , lakini yanaonyesha jinsi ilivyo rahisi kudukua simu kupitia USB zisizo salama. Kinga ni bora.