MABINGWA wa Ligi Kuu ya Wanawake, JKT Queens imeanza kwa kishindo michuano ya CECAFA kwa Wanawake ya kuwania tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa JKU Princess mabao 5-0 kwenye mchezo wa Kindi C.
Mechi hiyo imepigwa mchana huu kwenye Uwanja wa Ulinzi Complex Kenya ambako mashindano hayo yanaendelea kufanyika kuanzia jana hadi Septemba 16.
JKT ilionekana kumiliki mpira tangu dakika ya kwanza ikigawanya mabao, matatu kwa kipindi kwa kwanza na mengine kipindi cha pili.
Katika mechi hiyo mshambuliaji kinda Jamila Rajabu aling’ara akifunga hat-trick ikiwa ya kwanza kwenye mashindano hayo yaliyoanza jana kwa zikipigwa mechi mbili, Rayon Sports ikishinda 2-1 dhidi ya mabingwa watetezi C.B.E na wenyeji Police Bullets ikishinda bao 1-0 dhidi ya Kampala Queens.
Mabao mengine yalifungwa na winga Chipukizi, Winifrida Gerald na mkongwe Asha Mwalala ambaye alijiunga na timu hiyo akitokea Simba Queens.
JKU ambayo ilisheheni nyota kibao waliotoka Bara walionekana kuingia uwanjani kwa kutoiheshimu JKT ambayo ilionyesha mechi nzuri na kutumia kila nafasi iliyopata.
Matokeo hayo yanaifanya JKT kuandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kwenye michuano hiyo kufunga mabao mengi na kutoruhusu bao dakika 90.
JKT ambayo inatafuta nafasi nyingine ya kunyakua taji hilo kwa mara ya pili baada ya kuchukua mwaka 2023 mbele ya C.B.E ya Ethiopia kwa mikwaju ya penati 5-4 kufuatia sare ya bila kufungana mashindano yaliyopigwa Uganda.
Michuano hiyo itaendelea kesho KQ FC itaikaribisha Denden Queens kwenye Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi.