Bajana atua jeshini na mzuka

BAADA ya kuagana na uongozi na wechezaji wenzake wa Azam FC,  kiungo Sospeter Bajana ametua JKT Tanzania akiwa na mzuka mwingi, akisema yupo tayari kwa ushindani ndani ya kikosi hicho anachoamini kitamrudisha katika ubora aliokuwa nao awali.

Bajana amemalizana na Azam baada ya kuitumikia kwa miaka 15 na msimu ujao atakuwa na kazi jeshini kuitumikia JKT iliyomaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya sita.

Kiungo mkabaji huyo, alisema alikuwa na misimu bora tangu alipojiunga na Azam na kwamba kuondoka kwake ni mwanzo wa maisha mengine nje ya timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bajana alisema ni uamuzi sahihi na anaamini kuna maisha mengine bora nje ya Azam, huku akiweka wazi kuwa yupo tayari kwa changamoto nyingine mpya ndani ya JKT Tanzania.

“Ni kweli nimemalizana na JKT Tanzania hawa ndio waajiri wangu wapya, nipo tayari kwa changamoto hii mpya na naamini timu hii ni chaguo sahihi kwangu, itanirudisha kwenye ushindani,” alisema Bajana na kuongeza;

“Nipo fiti tayari kwa mapambano, naomba ushirikiano kwa wachezaji wenzangu tujenge JKT Tanzania bora ambayo itatoa ushindani.”

Akizungumzia miaka 15 ndani ya Azam alisema ilikuwa mizuri isipokuwa msimu wa 2024/25 ambao ameutaja kuwa ulikuwa mchungu kwake kutokana na kukaa nje akiuguza jeraha lake la nyonga.

“Sikuwa uwanjani kwa msimu mmoja na nusu kama sijakosea kwani niliumia msimu wa nyuma kabla ya uliopita unajua kazi yangu ni mpira hivyo haiwezi kuwa sahihi mimi kutokucheza msimu mzima na nikashindwa kuutaja msimu huo kuwa ulikuwa mgumu kwangu.

“Hakuna kitu kigumu kama kukosekana sehemu ya kazi kwa miezi 12. Nilipitia wakati mgumu sana licha ya uongozi wa timu kuwa karibu na mimi lakini kuna vitu vingi nilikuwa navikosa hasa mambo ya soka.”

Bajana tangu alipopata majeraha Desemba 11, 2023 kwenye Uwanja wa Azam Complex katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo Azam ilishinda 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kutokana na kukaa nje muda mrefu.

Kiungo huyo alipata majeraha ya mifupa ya nyonga ya kulia na ya kushoto yaani ‘Pubis Symphysis’, ambapo mnamo Mei 2024, alipelekwa Afrika  Kusini katika Hospitali ya Life Vincent Pallotti jijini Cape Town kwa ajili ya matibabu yake zaidi.

Majeraha hayo kwa nyota huyo, ndio yaliyofanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu,, ingawa hata aliporejea hakuwa na wakati mzuri wa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza mara kwa mara, jambo lililochangia kuachwa na Azam inayonolewa na kocha mpya Florent Ibenge.