Arusha inajiandaa kujipanga kuwa kitovu cha michezo na utalii kwa kuwaleta pamoja wawekezaji na mashabiki wa kimataifa kabla ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027.
Maandalizi ya mashindano hayo hayana kasi tu, bali pia yanatoa fursa ya kudumu kwa Arusha kuendeleza sekta ya michezo ambayo ni hatua muhimu katika kuanzisha jiji hilo kuwa kitovu cha michezo na utalii, huku timu za hapa zikipatiwa msaada kutoka kwa jamii na wadau mbalimbali.
Ili kufanikisha hilo, Wilaya ya Arusha imezindua kamati ya michezo yenye wajumbe wanane wenye jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli zote za michezo kuanzia shule, mitaa, kata hadi ngazi ya taifa.
Wajumbe hao ni Haruni Kidungu, Petro Lucumay, Ashura Ramadhan, Nicholaus Malima, Anna Mdoe, Hassan Abdallah, Geoginal Matagi na Issa Kadeghe.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amewahimiza wanakamati hao kufanya kazi kwa uadilifu, mshikamano na bidii kwa kuwa michezo ni jukumu la jamii.
“Nawasisitiza wajumbe wa kamati kufanya kazi kwa bidii na mshikamano na bidii, pia tunawaomba wadau na sekta binfasi kuunga mkono juhudi hizi, kwani michezo ni chombo cha kuibua vipaji, kuimarisha afya, kutoa ajira na kuhamasisha utalii,” amesema Mkude.
Kamati pia itahakikisha uwekezaji katika miundombinu na kutoa mafunzo kwa michezo yote kwa lengo la kukuza vipaji vya muda mrefu.
Mkude amesisitiza kuwa maandalizi mapema ya Afcon 2027 ni muhimu kufanya Arusha iwe kivutio cha michezo kinachovutia mashabiki na kuendeleza vipaji vya ndani.
“Tukiangalia historia yetu, mazingira na nguvu kazi iliyopo, Arusha ina kila sababu ya kufanikisha hili, hivyo ushirikiano wa jamii na wadau ni msingi wa kufanikisha malengo haya,” ameongeza Mkude.
Katibu wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Arusha (ARWFA), Yasinta Amos amesema wanataka wanawake pia washiriki kikamilifu kwenye michezo.
“Kamati hii ni hatua muhimu ya kuimarisha soka la wanawake na kutoa fursa za mafunzo kwa wachezaji wa kike,” amesema Yasinta.
Kwa upande wake, Fredrick Lyimo ‘Deco’ ambaye ni katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Arusha (ADFA), ameeleza kuwa hiyo ni fursa kubwa ya kuibua vipaji vipya akiongeza kuwa wana mipango ya kuhakikisha wanatumia kuipa kipaumbele mashindano ya vijana na kujenga timu zenye ushindani wa Ligi.