Messi apewa mmoja Polisi Tanzania

TIMU ya maafande wa Polisi Tanzania, imefikia makubaliano ya kumsajili aliyekuwa winga wa Namungo ‘Wauaji wa Kusini’, Issa Abushehe ‘Messi’ kwa mkataba wa mwaka mmoja kukitumikia kikosi hicho, baada ya pande zote mbili kufikia uamuzi huo.

Abushehe ameachana na Namungo aliyojiunga nayo katika dirisha dogo la Januari 2025, ikiwa ni muda mfupi tu tangu nyota huyo avunje mkataba wake wa miezi sita na KVZ inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar kwa makubaliano ya pande hizo mbili.

Nyota huyo alijiunga na KVZ msimu wa 2024-2025, akitokea Biashara United ya mkoani Mara iliyokuwa inashiriki Ligi ya Championship, japo ameitumikia kwa miezi sita tu, kisha kuvunja mkataba wake uliobakia kwa makubaliano ya pande mbili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Abushehe alisema ni kweli amefikia makubaliano na Polisi Tanzania kwa ajili ya kuichezea timu hiyo kwa msimu wa 2025-2026, akiamini ni sehemu nzuri kwa aina ya nyota wengine wakubwa na wazoefu waliosajiliwa.

Nyota huyo anakumbukwa zaidi Septemba 19, 2022, wakati akiwa na Coastal Union, ambapo alipata dili la kujiunga na Al Mokawloon Al Arab inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri, japo alirejea nchini na kujiunga na Biashara United ya mkoani Musoma.

Abushehe anakuwa nyota mpya wa tisa baada ya Ramadhan Kapera (TMA Stars), Hamad Nassoro (KenGold), Naku James (Mbuni), Lazaro Mlingwa, Ibrahim Isihaka, Jamal Mtegeta (Pamba Jiji), Rajab Athuman (Stand United) na Joseph Majagi (Geita Gold).

Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza katika nafasi ya 15 kwa pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.