Rasmi Fadlu afunuliwa faili la Bajaber

WAKATI mashabiki wa Simba wanasubiri kwa hamu kumuona Mohammed Bajaber akiichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza katika mechi za mashindano, kocha wa zamani aliyewahi kumnoa wakati akiwa Polisi Kenya, amempa ‘code’ kocha Fadlu Davids aweze kumfaidi vyema kikosini.

Bajaber ni kati ya nyota sita wapya wa kigeni waliosajiliwa na Simba katika dirisha linalotarajiwa kufungwa rasmi kesho Jumapili, akichomolewa katika kikosi cha timu ya taifa ya Kenya, kilichokuwa kikijiandaa na fainali za CHAN 2024 zilizomalizika mwishoni mwa mwezi uliopita.

Hata hivyo, bado mashabiki hawajamuona kiungo mshambuliaji huyo uwanjani akiliamsha, lakini kocha Etienne Ndayiragije ameibuka na kufichua mambo kuhusu nyota huyo wa Msimbazi.

Msimu uliopita akiwa na Polisi Kenya chini ya Ndayiragije, kiungo huyo alifunga mabao 11 na kutoa asisti nne, akiongoza kikosi hicho kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu wakiwavua taji watetezi, Gor Mahia.

Ndayiragije, aliyewahi kuinoa pia Taifa Stars, Mbao FC, Azam FC na KMC, amesema Simba imepata mchezaji mwenye kipaji kikubwa.

Kwa mujibu wa Ndayiragije ni kwamba Bajaber sio mchezaji mwenye kasi na nguvu pekee, bali pia ana uwezo wa kuisoma mechi na kubadilika haraka kulingana na mazingira ya mchezo.

“Najua kwa sababu mimi ndio niliamua kumpandisha na kuanza kumpa nafasi. Bajaber ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, nilipofanya kazi naye Polisi niliona namna alivyo makini na mwenye kiu ya mafanikio,” alisema kocha huyo na kuongeza;

“Ni kijana ambaye haogopi changamoto na mara zote hutafuta namna ya kuamua mechi, kitu ambacho wachezaji wachache wanacho.”

Kwa mujibu wa Ndayiragije, Simba inachohitaji sasa ni kumpa Bajaber nafasi na kuamini uwezo wake. 

“Nilipokuwa naye Police, nilimpa nafasi kubwa na majukumu mazito kwa sababu niliona ndani yake kuna kitu. Kila mara alijibu kwa vitendo uwanjani. Simba ikimwamini, naamini atafanya makubwa sana,” aliongeza kocha huyo aliyepo nchini kwa sasa na kikosi hicho kwa ushiriki wa michuano ya Kombe la Kagame 2025.

Kwa sasa, Simba inajiandaa kwa msimu mpya chini ya Fadlu Davids, na ujio wa Bajaber pamoja na wachezaji wengine wapya kwenye kikosi hicho unaonekana kuongeza chachu ya ushindani katika karibu kila nafasi.

Simba itacheza mechi ya kirafiki ya kutambulisha kikosi kipya dhidi ya Gor Mahia siku ya Septamba 10, kisha kuvaana na Yanga katika pambano la Ngao ya Jamii Septemba 16 kabla ya kusafiri hadi Gaborone, Botswana kuumana na Gaborone United katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mbali na Bajaber, Simba imeshusha pia nyota wengine 11 wapya wakiwamo wageni Jonathan Sowah, Rushine De Reuck, Nabu Camara, Alassane Kante na Neo Maema, huku wazawa wakiwa ni Morice Abraham, Charles Semfuko, Seleman Mwalimu, Wilson Nangu, Yakoub Suleiman na Anthony Mligo.