Singida yapata ushindi wa kwanza Kagame,  Chama akiliamsha

MSHAMBULIAJI wa kati, Elvis Rupia amewaumiza ndugu zake Wakenya kwa kuifunga Polisi, akiibeba  Singida Black Stars kupata ushindi wa kwanza katika michuano ya Kombe la Kagame 2025viliyopigwa leo, Ijumaa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

Rupia aliyekuwa na jukumu la kuongoza safu ya ushambuliaji ya Singida BS alifunga bao moja wakati timu hiyo ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Kenya, huku Clatous Chama akiitumikia kwa mara ya kwanza Singida BS.

Singida ilianza mashindano hayo kwa suluhu dhidi ya Ethiopia Coffee ilipata bao la kwanza kupitia Rupia dakika ya 13 lilidumu hadi mapumziko.

Singida BS ilirejea na nguvu zaidi katika kipindi cha pili hasa kuanzia dakika 74 baada ya kufanya mabadiliko kadhaa ikiwemo kuingia kwa Clatous Chama aliyechukua nafasi ya Rupia.

Chama aliyeenda kucheza namba 10 huku Mishamo Daud ambaye naye aliingia akisimama kama mshambuliaji wa mwisho.

Ndani ya dakika chache Singida BS ilipata bao la pili kupitia Andre Kofii  baada ya Polisi kufanya makosa wakiwa eneo lao.

Katika dakika 26 alizocheza Chama alionyesha ubunifu wake kwa kurahisisha kazi katika eneo la mwisho la ushambuliaji, alionekana akipiga pasi za kwenda mbele.

Mwamba huyo wa Lusaka  kidogo awafunge Polisi akiwa ndani ya eneo la hatari aliangushwa wakati akitaka kuuweka vizuri mpira katika himaya yake, hata hivyo haikuonekana kuwa ni faulo.

Katika dakika ya 81, Polisi ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Charles Ouma. Katika mechi ya mapema mchana iliyopigwa uwanjani hapo leo, Ethiopa Coffee iliichapa Garde-Cotes mabao 6-0.

Garde-Cotes ambayo imeruhusu mabao 10 ndani ya mechi mbili, itacheza dhidi ya Singida BS, huku Ethiopia Coffee ikicheza dhidi ya Polisi kufunga hesabu ya Kundi A.